Mkandarasi mkuu wa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka (BRT), Strabag International ametangaza mabadiliko ya matumizi katika makutano ya barabara za Morogoro na Kawawa.
Mabadiliko hayo yanaanza Jumatatu tarehe 17 hadi tarehe 30 mwezi huu. Akitangaza mabadiliko hayo leo jijini Dar es Salaam, Afisa uhusiano wa kampuni hiyo, Bw. Yahya Mkumba alisema mabadiliko hayo yanatokana na matengenezo yatakayokuwa yanafanyika eneo hilo.
Akielezea zaidi, alisema magari yatakayokuwa yanaelekea Ubungo kutokea Jangwani yatalazimika kutumia mchepuko uliopo kabla ya kituo cha Magomeni Mapipa kwa kuingia barabara ya mabasi yaendayo haraka.
Pia magari yatakayokuwa yanatokea Ilala Boma kuelekea Morocco, Ubungo na Jangwani yatalazimika kutumia barabara moja ya upande wa kushoto. “Wananchi watuvumilie katika kipindi hiki na tunaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaotokea,” alisema.
Mradi wa BRT unalenga kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam. Kilomita 20.9 za mradi huo awamu ya kwanza zipo mbioni kukamilika na kwa mujibu wa ratiba, zabuni za kupata watoa huduma zinatarajia kutangazwa mapema mwakani.
Mradi huu ni moja ya miradi mikubwa duniani katika mfumo huo ambao unatarajiwa kuwa mfano katika eneo hili la Afrika ya Mashariki na kati.
Katika siku za hivi karibuni, viongozi na makundi ya watu mbalimbali yameeleza kuridhishwa kwao na maendeleo ya mradi huo na kutoa mapendekezo ya kuuboresha zaidi.
0 comments:
Post a Comment