SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Tuesday, February 28, 2012

Amani Millanga:Vijana na Maandamano, Polisi na Mauwaji: Tunaelekea Wapi?

Ndugu zangu,
Naomba nitwae fursa hii kuwapa pole wale waliofiwa na ndugu zao waliouwawa na Polisi huko Songea. Poleni sana.
Tunaelekea Wapi?
Amani ya Tanzania sasa inatikiswa na hali si shwari nchini. Hali hii inatia hofu na mashaka makubwa kwa mtanzania mzalendo kwani matukio ya mauwaji yanayotokana na wananchi kuaandamana na kuuwawa na Polisi yanadizi kuongezeka. Polisi wamewauwa raia wasio na hatia katika sehemu mbalimbali nchini zikiwemo Arusha, Mbeya, na sasa Songea. Mauwaji haya ni kinyume na maadili na wajibu wa Polisi kwani kazi ya siku zote ni kulinda usalama wa raia na mali zao. Iweje leo Polisi wanawauwa raia na kuharibu mali zao? Chuki inayopandikizwa na ukiukwaji huu wa haki za binadamu ni kubwa dhidi serikali na pia kwa Chama Cha Mapinduzi. Chuki hii ni kubwa sana miongoni mwa vijana na hata watu wazima, na jambo la hatari zaidi ni kwamba inasambaa kwa kasi zaidi kila pembe ya nchi - mijini na vijijini. Katika makala haya nitawaongela vijana kwani hawa ndio wamekuwa wakipambana na Polisi.

Wasifu wa VijanaVijana ninaowaongelea hapa wana umri wa miaka kati ya 16 na 40 (ingawa ujana unaanzia miaka 18) na ndiyo walio wengi katika nchi yetu. Pili, ndiyo nguvu kazi ya taifa. Tatu, wengi wao hawana hata elimu ya msingi, na wale waliobahatika kupata elimu ya sekondari wengi wao wamesomea katika sekondari za kata ambazo zimewakata. Nne, wengi wao hawana ajira rasmi yenye pensheni na mafao mengine. Tano, wamekulia katika mazingira ya ulimwengu wa utandawazi (Profesa Shivji anauita UTANDAWIZI) naTanzania inayokumbatia sana siasa za uliberali mamboleo zilizojaa unyonyaji, dhuluma na uonevu. Sita, ni wahanga wa soko huria ambalo limewaacha wanalia. Saba, wengi wao hawaijui kwa dhati historia ya nchi yetu na siasa yake ya kuthamini UTU na HAKI ilivyokuwa. Nane, wengi wao si waoga pale wanapokuwa wadai haki zao. Tisa, wengi wao wamekulia katika familia zenye hali ngumu ya maisha inayozungukwa na umasikini uliokithiri na magonjwa katika mitaa ya miji yetu na vijiji vyetu. Kumi, wengi wao wana afya zilizodhohofika kutokana na kutokupata lishe ya kutosha na matibabu ya uhakika lakini wanafanya kazi ngumu sana tena kwa muda mrefu na kulipwa ujira mdogo.
Mtu anaweza kuwadharau vijana hawa kwamba kwa kuwa wengi wao si wasomi na wanadhiki, basi ni rahisi kuwadanganya au kuwatisha wakanyamaza kwa dhana kwamba: hawazijui haki zao za msingi; hawaujui mfumo wa uchumi wa dunia unavyofanya kazi na unavyowaathiri; hawajui athari za kupanda kwa bei ya mafuta; hawajui athari za mfumuko wa bei; na hawajui maana halisi ya demokrasia kwani zipo tuhuma kwamba wengi wao hawapigi kura au wanauza shahada zao. Na kwamba wanachojua ni kupata mlo wao na siku ikapita. Lakini si hivyo hata kidogo. Vijana hawa wanazijua haki zao na mahitaji yao msingi ya kuehishimiwa na kuthaminiwa utu wao, ya chakula, malazi na mavazi.
Kama ilivyo kwa binadamu yeyote awaye, vijana hawa hawataki kuishi katika maisha duni ya kimaskini. Wanataka ustawi na maisha bora kwao na vizazi vyao. Pia tufahamu kwamba vijana hawa, kwa jitihada zao binafsi, ni wajuzi katika fani mbalimbali kuanzia ufundi mekanika hadi ujenzi wa nyumba. Wana maarifa ya kuendesha biashara tena kwa faida. Wanajua fika wafanye nini ili wastawi. Ni wafanyakazi hodari ndio maana wanaweza kujilisha na si wezi. Lakini ni bahati mbaya sana katika safari yao ya maisha, njia yao imejaa vikwazo vya kila namna - dhuluma na uonevu; rushwa na ufisadi. Kutokana na hali hii vijana hawa wamekata tamaa.
Wengi wao hawana tena tumaini la maisha bora. Ndoto zao zimekufa. Sasa wanazivuta hisia na wameanza kuandamana wakiungwa mkono na wazee, wafanyakazi maofisini na jamii inayowazunguka wanawake kwa wanaume. Nilifuatilia maandamano ya Mwanza na taarifa nilizozipata zinasema kwamba wanawake katika maeneo ya jiji hilo walikuwa na ndoo za maji tayari kuwapatia vijana wanawe nyuso zao pindi mabomu ya machozi yakipingwa. Mapambano ya Mbeya nasikia yalikuwa ni makali kweli. Katika maandamano ya vijana kudai haki zao tumeiona ‘NGUVU YA VIJANA’ ikitembea. NGUVU hii ya vijana ikiachwa bila kupewa majibu na suluhisho la matatizo yao ITAUMA NA TAIFA LITAUMIA. Tumeiona mifano duniani kote na hivi karibuni katika nchi za Kiarabu. Tusifike huko.
Kuwauwa Waandamanaji ni Kuitia Amani Kitanzi
Kuwauwa waandamanaji ni sawa na kuiwekea kitanzi amani. Hali hii inaweza kusababisha maandamano yenye ghasia kuibuka nchi nzima. Nayo serikali ikajikuta inatumia mabavu zaidi kuyazima maandamano haya. Katika kuyazima maandamano ipo nafsi kubwa sana ya watu wengi kupoteza maisha. Watu wakipoteza maisha chuki itaongezeka na damu nyingi zaidi itazidi kumwagika kutokana na mapambano kati raia na vyombo vya dola. Huo ndio wakati ambao unasubiriwa kwa hamu kwa wasioitakia mema Tanzania. Hapo litatolewa tamko katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu umwagaji damu huo na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Serikali itaingia katika mgogoro mkubwa ndani na nje katika jumuiya ya kimataifa. Matamko yatatolewa na wananchi ndani ya nchi na pia mataifa makubwa ya nje kwamba serikali ijiuzulu na CCM kama chama tawala kiachie ngazi. Hatujui nini itakuwa ni hatima hali hii. Lakini ukweli ni kwamba amani haitakuwepo tena. Watu wengi wasio na hatia watauwawa na wengine watakuwa wakimbizi. Uchumi na ustawi utavurugika. Kwa hiyo basi Polisi ijitahidi sana kuepuka kuuwa raia wasio na hatia. Itumike busara zaidi na nguvu za kadri na kadri za “piga lakini chunga usiuwe” na si risasi za moto. Tukumbuke kuwa Tanzania ni katika nchi chache sana Afrika ambayo hijaingia katika machafuko. Na yapo mataifa yanataka siku moja Tanzania itikiswe ili waone nini kitatokea. Mungu atuepushe balaa hili.
Nini Chanzo?
Wengi watakubaliana nami kuwa kiini hasa cha watu kuandamana ni kukithiri kwa umaskini nchini, ukosefu wa ajira kwa vijana, uonevu, kutokuthaminiwa kwa UTU wa watu na kuheshimiwa HAKI zao, maisha kuwa ghali, unyonyaji na dhuluma. Katika hotuba yake ya “Wasia wa Mwalimu Nyerere kwa CCM” Hayati Baba wa Taifa aliyachambua vema mambo haya aliposema hivi: “Tanzania isikosee ikaacha msimamo wake wa kuhakikisha kwamba uko usawa wa binadamu, kuna usawa wa msingi katika hali ya maisha ya kila mtu, na kwamba kuna heshima ya binadamu kwa kila raia wa Tanzania.
Tukifanya kosa kama hilo tutavuruga msingi wote wa utulivu na amani katika nchi yetu. Maana yake ni kwamba tutaruhusu na kuimarisha tabaka na fikira za ‘Sisi’na ‘Wao’. Tutaacha watu wachache wawe na mali nguvu, na fidhuli ya kuwa na mali na nguvu; watu wengi wawe ni maskini na wanyonge; na wana maning’uniko na ghadhabu za umaskini na unyonge.
Mgawanyiko wa namna hiyo ni hatari sana. Utaratibu wa vyama vingi katika mazingira na hali fulani unaweza usiathiri utulivu. Lakini tofauiti kubwa sana za mapato na hali ya maisha au hata matumaini tu ya maisha mema ya baadaye haziwezi kuzaa utulivu. Mimi siamini hata kidogo kwamba mnaweza kujenga amani na utulivu wa kudumu katika nchi masikini bila kuheshimu misingi ya haki na usawa. Na ‘unyang’au’ kwa hulka yake hauheshimu misingi ya haki na usawa.”
Suluhisho
Hatima ya maisha ya vijana si suala dogo la kuacha lijimalize lenyewe. Linataka kutafutiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu. Suluhisho la kweli ni kurudi katika miongozo ya Mwalimu Nyerere ya kuthamini UTU na USAWA wa watu na kuheshimu HAKI zao. Tuonyeshe kwa vitendo kwamba kweli tunazijua, tunazitambua na kuguswa na shida za watu. Na kwamba kwa uhakika kabisa kabisa tunazifanyia kazi. Na matunda au matokeo ya kazi hiyo yanaonekana. Shaaban Robert aliandika, “Matendo hukidhi haja maridhawa kuliko maneno.” Vijana wanataka matendo. Wanataka ajira. Wanataka huduma bora ya afya. Wanataka elimu bora kwao na vizazi vyao. Wanataka kunufaika utajiri wa raslimali za nchi. Wanataka rushwa idhibitiwe. Dhuluma, uonevu na unyonyaji vikomeshwe.
Kazi hizi zinafanywa na serikali. Lakini serikali ina wajibu wa kuyafanyia kazi mambo haya na kuleta majibu ya kuwaridhisha vijana na wananchi. Matokeo yake imani ya vijana na wananchi kwa CCM na serikali yake itarudi. Nayasema haya kwa upendo na moyo mweupe kabisa kama mfuasi wa siasa na mafunzo ya Mwalimu ya Nyerere na kada wa CCM (nje ya chama ndani ya umma). Chama Cha Mapinduzi kiliijengea Tanzania heshima katika Afrika na kote duniani. Chama kilisimamia na kutetea haki za wanyonge ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Wakati umefika sasa wa kuirejesha hadhi ya CCM.
Kinyume chake basi kauli aliyoitoa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ya “Bila CCM Madhubuti Nchi Itayumba” itatimia siku si nyingi. Pia nitumie fursa kuwasihi vijana na wananchi kwa ujumla kuepuka matumizi ya nguvu, jaziba na hasira pale wanapoandamana kwani hasira haimalizi hasira. Amani ikishapotea ni vigumu sana kuirejesha.
Hitimisho
Nimalizie kwa kusema kwamba kuiuwa nafsi isiyo na hatia ni dhambi kubwa sana mbele ya Mwenyezi Mungu muumba wa mbigu na ardhi. Katika Quran Mwenyezi Mungu anasema katika SURAT AL MAIDA (Sura ya 5: Aya 32) kwamba: “Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi (ufisadi) katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote. Na hakika waliwajia Mitume wetu na hoja zilizo wazi. Kisha wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika nchi.” Pia katika Biblia Mwenyezi Mungu katika Amri ya sita anasema “USIUWE”. Iweje leo tunaanza kuuwana? Tutaiua Tanzania.
Namuomba Mungu azidi kuibariki Tanzania. Adumishe Uhuru na Umoja kati ya wanawake, wanaume na watoto wa Tanzania kwani Uhuru na Umoja wetu ndizo ngao zetu za kuilinda na kuikinga amani yetu isitoweke.
Ndugu yenu
Amani Millanga

1 comments:

Anonymous said...

Mwandishi umesema kweli.

Post a Comment