Whitney Houston.
Bobby Brown.
******
Sifael Paul na Mtandao
KIFO cha staa wa muziki wa Pop, RnB na muvi za Hollywood, Marekani, Whitney Houston (48), kimeibua gumzo kubwa katika ulimwengu wa burudani, huku aliyekuwa mumewe kati ya mwaka 1992 hadi 2007, Boby Brown akihusishwa.
Kwa mujibu wa msemaji wa Whitney, Kristen Foster, Whitney alifariki dunia Jumamosi iliyopita katika Hoteli ya Beverly Hilton jijini Los Angeles, saa chache kabla ya ‘kupafomu’ kwenye sherehe za maandalizi ya Tuzo za Grammy, bado uchunguzi wa kifo chake unaendelea.
Pamoja na jeshi la polisi Beverly Hills kupitia mkuu wake, Luteni Mark Rosen kuthibitisha kukutwa kwa aina fulani ya vidonge vya kutuliza maumivu katika chumba alichofia mwanamuziki huyo, mashabiki wa Whitney aliyezaliwa Agosti 9, 1963, wameendelea kumng’ang’ania Boby kuwa ndiye aliyembadili Whitney na kumfanya abobee kwenye matumizi ya madawa ya kulevya ambayo kwa vyovyote yamechangia kuondoa uhai wake.
Mashabaki hao katika mitandao ya kijamii waliukosoa uamuzi wake wa kuolewa na Boby aliyesifika kwa kubwia ‘unga’ na matokeo yake kuyumba kwa afya na sauti yake huku akisoteshwa rumande mara kwa mara kwa ishu hiyo.
Katika hilo, Whitney aliyezaa mtoto mmoja wa kike na Boby aitwaye Bobbi Kristina aliwahi kusema: “Unapompenda mtu, unapenda kweli, je, unaweza kuacha kumpenda mtu kwa sababu ana taswira mbaya katika jamii? Nampenda Boby.”
Whitney ambaye alikuwa gumzo miaka ya 80 na 90 kutokana na sauti yake ya kumtoa nyoka pangoni na baadaye kwenye ushiriki wake katika muvi za The Body Guard na Waiting to Exhale, aliwahi kukiri kuandamwa katika maisha: “Nina shetani mkubwa ananiandama, kama siyo marafiki zangu, basi ni maadui zangu.”
Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, ratiba ya mazishi ya staa huyo aliyetikisa dunia na albamu zake kali za Whitney Houston (1985), Whitney (1987), I’m Your Baby Tonight (1990), My Love Is Your Love (1998), Just Whitney (2002), One Wish: The Holiday Album (2003) na I Look to You (2009), haikujulikana huku watu wakiwa na shauku ya ripoti ya polisi ili kujua kilichomuua.
Habari na GPL.
0 comments:
Post a Comment