Na Mwandishi wetu
=====
Dar es Salaam: May 29,
2015: SHIRIKA la ndege la taifa (ATCL) limetangaza uamuzi wake wa
kuongeza idadi ya safari zake kuelekea visiwa vya Comoro hatua
inayolenga kuendana na ongezeko la mahitaji ya huduma za shirika hilo
hususani katika kuelekea kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kwa sasa shirika hilo
linatoa huduma zake kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma na Mtwara kila
siku. Sambamba na kutoa huduma hizo hapa nchini, shirika hilo lina
mpango mpya utakaoanza rasmi tarehe mosi ya mwezi Juni mwaka huu kwa
kuongeza safari zake kuelekea visiwa vya Comoro hadi kufikia mara nane
kwa wiki ikiwemo mara mbili siku za Alhamisi.
Akizungumza na waandishi
wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Bw.
Johnson Mfinanga alisema shirika hilo ndilo pekee linalotoa huduma ya
safari za anga kati ya Tanzania na Visiwa vya Comoro huku akibainisha
fursa za kibiashara zilizopo kati ya nchi hizi mbili jambo
linalosababisha uwepo wa ongezeko la mahitaji ya huduma za ATCL.
Pia amewaasa watanzania
hususan wakazi wa mtwara kuchangamkia fursa hizo kwa kuwa shirika hilo
kwa sasa linatoa huduma zake kati ya Mtwara na visiwa vya Comoro kwa
siku za Jumatano na Ijumaa kila wiki.
“Siku zote tumekuwa
tukihakikisha kwamba tunabadilika kuendana na mahitaji ya wateja wetu.
Ni dhahiri kwamba katika kipindi hiki kuna hitaji kubwa la usafiri wa
anga kuelekea visiwa vya Comoro kwa sababu za kibiashara, mapumziko na
sherehe mbalimbali, hivyo ATCL imejipanga kuchangamkia fursa hiyo,’’
alibainisha.
Akizungumzia ufanisi wa
shirika hilo katika safari nyingine ikiwemo zile za Kigoma na Mtwara,
Bw. Mfinanga alisema wamekuwa wakihudumia idadi kubwa ya abiria kutokana
na ndege za shirika hilo kusafiri kwa mwendo kasi wa kuridhisha
sambamba na huduma nzuri zinazotolewa kwa wateja wakati wa safari.
“Zaidi tunaamini kwamba
huduma tunazozitoa kati ya Tanzania na Comoro zimekuwa zikichangia
kuongeza ushirikiano baina ya nchi hizi mbili na tunaamini kuwa hata
hili ongezeko la safari zetu kwenye mataifa haya mawili zitatoa fursa
kwa wateja wetu kufaidi fursa zinazopatikana ndani ya nchi hizi,’’
aliongeza Bw. Mfinanga
Kuhusu mpango wa shirika
hilo kujipanua zaidi kihuduma, Bw. Mfinanga alisema: “Ndege yetu aina
ya De-Havilland Dash 8 Q300 kwa sasa inafanyiwa marekebisho makubwa
kwenye karakana yetu iliyopo kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA) na itakapokamilika tutaendelea na huduma zetu
katika mikoa ya Mwanza, Tabora, Kilimanjaro na Mbeya,’’
Bw. Mfinanga aliongeza
kuwa kwa kufanya safari zake kuelekea visiwa hivyo shirika hilo limekuwa
likiwezesha wateja wake kunufaika na fursa zilizopo kwenye visiwa hivyo
huku pia akitoa wito kwa watanzania wengine kujitokeza kushiriki katika
kuchangamkia fursa hizo.
Chanzo Full Shangwe
0 comments:
Post a Comment