Mwanamuziki maarufu wa Bongo Fleva, Rehema Chalamila ‘Ray C’ akiwa hoi hospitali.
Na Joseph Shaluwa na Musa Mateja
MARADHI yanayomsumbua mwanamuziki maarufu wa Bongo Fleva, Rehema Chalamila ‘Ray C’ ni tishio, Gazeti la Mastaa, Amani limeelezwa.
Ray C anaugua ugonjwa wa Homa ya Dengu ambao kitaalam hujulikana kama Dangue Fever. Ulibainika baada ya kufanyiwa uchunguzi na madaktari wa Hospitali ya Mkoa wa Kitabibu wa Kinondoni, Mwananyamala jijini Dar na baadaye kulazwa hospitalini hapo.
Staa huyo wa muziki ambaye pia hujulikana kama Kiuno Bila Mfupa alifikishwa hospitalini hapo, Jumapili iliyopita mchana baada ya hali yake kuwa mbaya.
KUTOKA KWA CHANZO
“Ni kweli Ray C amelazwa hapa Mwananyamala. Ameletwa leo (Jumapili) saa tano mchana,” alisema mtoa habari wetu ambaye aliomba hifadhi ya jina lake.
Mtoa habari huyo, naye alikuwa mgonjwa alilazwa katika wodi namba tano, hospitalini hapo ambayo Ray C alikuwa amelazwa.
“Afya yangu si nzuri sana, lakini nimeweza kumtambua. Namfahamu sana Ray C. Nina hakika ndiye aliyelazwa hapa,” aliendelea kusema lakini hakueleza ugonjwa anaougua.
MAPAPARAZI WAINGIA KAZINI
Baada ya timu yetu kunasa taarifa hizo, Jumatatu jioni mapaparazi wetu walitinga hospitalini hapo na kuthibitishiwa kuwa Ray C alikuwa mgonjwa na kulazwa.
Hata hivyo, juhudi za kuingia wodini kuonana naye hazikuzaa matunda kwa vile muda wa kuwaona wagonjwa ulikuwa umekwisha kwa siku hiyo.
Hata pale walipojitambulisha kuwa ni waandishi, wahusika walijibu kwa kifupi: “Haiwezekani, anatakiwa kupumzika.”
DAKTARI ATHIBITISHA
Mmoja wa madaktari wanaoshughulikia afya ya msanii huyo alithibitisha kuwa Ray C ana dalili zote za ugonjwa huo, akasema: “Ni kweli ana dalili zote za dengu, lakini siruhusiwi kutoa taarifa za mgonjwa, labda kwa ruhusa yake mwenyewe au mama yake mzazi.”
AMANI TENA
Waandishi wetu hawakuchoka, siku iliyofuata, Jumanne asubuhi na mapema, mapaparazi walidamkia hospitalini hapo kwa lengo la kumjulia hali staa huyo lakini walipoingia wodi namba tano alipokuwa amelazwa, hakuwepo!
Ilikuwa ni muda wa kuwaona wagonjwa, waandishi wakakuta kitanda kitupu, walipouliza kulikoni wakaelezwa amehamishiwa wodi maalum.
“Amehamishiwa kwenye chumba maalum kwa sababu waandishi walikuwa wanasumbua sana kutaka kumuona. Kama unavyojua tena, wodi ya kawaida inakuwa haina uangalizi mkubwa.
“Mtu yeyote anaweza kuingia ikiwa tu muda wa kuwaona wagonjwa utakuwa umefika. Jambo hilo limewakera sana ndugu ndiyo maana wamezungumza na madaktari na kumhamisha,” mtoa habari mwingine alisema kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini.
UFAFANUZI
Daktari mwingine aliyezungumza na Amani hospitalini hapo kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini kwa vile si msemaji alisema: “Kuhusu kulazwa, ni kweli amelazwa na anaumwa, lakini kumuona ni ngumu.
“Unajua Ray C ni maarufu, kumuacha kwenye wodi ya kawaida ni kumsababishia usumbufu usio na maana, wengi wanataka kumuona hasa waandishi kama ninyi. Anahitaji kupata muda wa kutosha kupumzika.”
KWA NINI TISHIO?
Homa ya Denge (Dengue Fever) kama ilivyoelezwa hapo juu ni tishio. Virusi vya ugonjwa huu husabazwa na mbu aina ya Aedes ambaye yupo katika mgawanyiko wa jamii tisa; Aedes Australis, Aedes Albooictus, Aedes Aegypti, Aedes Contator, Aedes Cinereus, Aedes Ructcus, Aedes Polynesiensis, Aedes Scutellaris na Aedes Vexans.
Mbu wa kike aina ya Aedes anapomng’ata binadamu mwenye maambukizi ya Homa ya Dengu huanza kuathirika mwenyewe na baada ya siku 8-10 huathirika zaidi kiasi cha mate yake kubeba virusi vya homa hiyo.
Dengu pia husambazwa kwa njia ya kuongezewa damu au kupewa viungo vya mtu aliyeathirika. Inawezekana kwa mama kumwambukiza mtoto wakati wa ujauzito au kwenye kujifungua.
Yapo maambukizi ya mtu na mtu wakati wa kujamiiana au mwingiliano wa damu lakini kitaalam inafafanuliwa kwamba si kawaida hali hiyo kutokea.
Ugonjwa huo unadhibitiwa kwa kumpa mgonjwa dawa ili kuzuia kutapika, maumivu ya mwili na kupewa dripu za maji lakini hakuna dawa maalum za tatizo hilo na mgonjwa akipona huweza kuugua tena siku yoyote.
TAARIFA ZAIDI ZA KIDAKTARI
Gazeti hili liliwahi kufunga safari hadi Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni, Dar na kufanikiwa kuzungumza na mganga mkuu wa hospitali hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Alithibitisha kuwepo kwa gonjwa hilo baya ambapo wakazi wengi wa jiji wameugua na wapo wanaoendelea kuugua.
“Huu ugonjwa haujaanza leo, inaonekana kama hospitali hii inahusika kwa kiasi kikubwa na tatizo hilo kwa sababu mimi niliamua kuachana na habari za kuwatibu watu malaria tu nikawa makini kutazama na ugonjwa huu ambao wengi hawautilii mkazo,”alisema.
Daktari huyo alizidi kusema kuwa, ugonjwa huo unaenezwa na mbu weusi wanaorandaranda ambao wanapenda kukaa sehemu zenye uchafu na majimaji.
“Wale mbu weusi wanaeneza kwa kasi ugonjwa huu ni tofauti kabisa na wale wanaoneza ugonjwa wa malaria,” alisema.
Akielezea dalili za ugonjwa huo mganga huyo alisema zinafanana na zile za ugonjwa wa malaria, mtu kuhisi joto kali mwilini, maumivu ya kichwa, kutapika, tumbo, maumivu ya mwili na misuli.
Alisema ugonjwa huo ulizidi kushika kasi mwaka huu katika kipindi cha mafuriko hivyo idadi ya wagonjwa aliowatibu kwenye hospitali yake ikaongezea, kutoka wagonjwa 4 mwaka jana mpaka kufikia wagonjwa 20 tangu Januari, 2014 kutokana na mvua iliyosababisha kuwepo kwa madimbwi kila kona.
MPAKA SASA HAUNA TIBA
Ugonjwa huu mpaka sasa hauna tiba ya uhakika, kinachifanywa kwa wagonjwa wanaogudulika kuwa nao ni kutibiwa tu dalili ili usizidi kusambaa mwilini.
WALIOATHIRIKA
Taarifa kutoka kwa wataalamu wa afya zinasema kuwa, mpaka sasa takribani watu milioni 100 duniani kote wameambukizwa ugonjwa huo na wengine milioni 2 wamefariki dunia baada ya kuugua.
TUMUOMBEE
Hata hivyo, jambo muhimu kwa Watanzania wote na wapenda burudani ni kumuombea Ray C apate nafuu haraka na kurejea kwenye majukumu yake kama kawaida.
KUMBUKUMBU MUHIMU
Ray C kwa muda mrefu alikuwa na matatizo ya kiafya lakini hivi karibuni afya yake ilitengemaa na usiku wa Jumamosi ya Mei 3, mwaka huu (kuamkia siku aliyolazwa) alionekana akiwa mwenye afya njema katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar kwenye shughuli za tuzo za muziki za Kilimanjaro Tanzania Music Awads (KTMA).
Ilikuwa mara ya kwanza kwa msanii huyo kuonekana hadharani baada ya kujificha kwa muda mrefu kufuatia matatizo yake ya kuugua kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya ‘unga’.
GLOBAL ILISHAANDIKA KUHUSU DENGU
Kuibuka kwa ugonjwa wa Homa ya Dengu kuliripotiwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Risasi Jumamosi ya Mei 3,2014 likiwa na kichwa cha habari ukurasa wa mbele kisemacho:GONJWA LISILO NA TIBA YA UHAKIKA LAIBUKA.
Ray C aliruhusiwa kutoka hospitali juzi saa 9:50 baada ya afya yake kuimarika.