Ndege
ya Shirika la ndege la Air Tanzania aina ya CRJ-200, yenye uwezo wa
kubeba abiria 50, ikiwa imetua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa
Songwe mkoani Mbeya hivi karibuni
===== ======= ===
SHIRIKA
la Ndege la Air Tanzania limeweka rekodi ya ongezeko la abiria kwa
asilimia 57 wiki chake baada ya kupokea ndege ya kukodi yenye uwezo wa
kubeba abiria 50 aina ya CRJ-200 pamoja kuiongezea uwezo wa kuruka kwa
wakati kwa asilimia 98.
Aidha,
shirika hilo limeweza kutoa nauli maalum kwa sikukuu za Pasaka kwa
abiria wa mkoani Mtwara ambao kwa sasa watakuwa wakilipa shilingi
250,000/- ikijumuisha kodi zote, kwa tiketi ya kwenda na kurudi.
Hayo
yalidhihirishwa jana jijini Dar es Salaam na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu
wa Shirika la Air Tanzania (ATCL), Kapteni Milton Lazaro, wakati
akitathmini utendaji wa kipindi kifupi wa ndege hiyo iliyokodishwa
pamoja na kuangalia mchango wake wakibiashara katika shirika hilo.
Kapt.
Lazaro alisema kwa ujumla, ujio wa ndege ya CRJ-200 mapema mwezi Machi
mwaka huu umesaidia kuboresha utendaji na kufikia kiwango cha juu, hali
inayoipa uongozi wa shirika sababu za kujivunia kwa maamuzi yao ya
kukodisha ndege hiyo.
“Inabidi
nikubali kuwa ndege imepokelewa vizuri na wateja wetu. Ndani ya wiki
chache tu ikiwa inafanyakazi, tumepata ongezeko kubwa la abiria wetu na
huduma zetu zimeweza kuaminika zaidi na wateja wetu wengi. Kwa maana
hiyo, matokeo yamekuwa ni mazuri sana,” alisema Kapt. Lazaro.
Alibainisha kuwa kinyume na taarifa zilizotolewa
na baadhi ya vyombo vya habari vikidai
kwambandege iliyokodishwa ya CRJ-200 ni mzigo kwa shirika ikilinganishwa
na ndege yake aina yaBombardier Dash-8, ndege hiyo mbali na
kuimarisha utendaji wa ATCL, pia imeisaidia shirika kuokoa fedha na
muda.
“Hatutajitendea
haki sisi wenyewe au kwa waliyotukodishia ndege hiyo kama tukiruhusu
sisi wenyewe tujiingize kwenye mjadala wa muundo wa gharama au mchango
wake wa kimapato, kwa muda huu mfupi. Inatosheleza kusema kuwa lengo
letu la kukodisha ndege hii ambalo lilikuwa ni kubwa kuliko mengine
limefanikiwa,” Ofisa Mtendaji huyo mkuu alisema.
Kapt.
Lazaro aliongeza kuwa, kuongezeka kwa idadi ya abiria wanaosafiri na Air
Tanzania kumetokana na ukweli kuwa muda inayotumia ndege ya CRJ-200
kusafiri umekuwa mchache zaidi ukilinganisha na ndege nyinginezo
zinazosafiri njia hizo, kwa hivyo uokoa muda wa abiria na pia abiria
wengi ufurahia huduma za ATCL wakiwa safarini.
“Mbali
na muda mfupi wa kusafiri, ndege hiyo imeboresha zaidi utendaji wa
shirika kwa asilimia 98. Ujio wa ndege hii umerudisha imani miongoni mwa
abiria wetu ambao sasa wanauhakika wa kusafiria kwa kufuata muda
uliyopangwa,” alisema.
Hivi
karibuni shirika hilo la ndege la Air Tanzania lilizindua safari za
kwenda katika mkoa wa Mbeya kwa kupitia uwanja mpya wa kimataifa wa
ndege wa Songwe ikitumia ndege yake ya CRJ-200.
Dakika
58 za safari kati ya Dar es Salaam na Mbeya, ambayo imepangwa kuwa siku
nne kwa wiki; Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumapili, imepokelewa
vizuri na abiria na wafanyabiashara wanaosafiri toka Mbeya kwenda jijini
Dar es Salaam.
Taarifa
za awali kutoka katika shirika hilo zilisema kuwa abiria sasa
watafurahia safari za kila siku za kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza,
mara nne kwa wiki kwenda Mbeya na itakuwa inasafiri kwenda Comoro katika
siku za Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumamosi.
Shirika
hilo pia limefuta adhabu zinazotozwa kwa abiria wanaoshindwa kusafiri
na wale wanaobadilisha safari zao, ili kuwasaidia abiria wao kutoingia
gharama za ziada pale wanapopatwa na dharura kabla ya kusafiri.
“Hatuamini kabisa katika kuwaadhibu abiria wetu wapendwa,” alisema Kapt. Lazaro.
Mkakati
wa utanuzi wa shirika hilo la ndege la taifa ni pamoja na kufungua njia
ya Tabora – Mpanda pamoja na kurejesha njia zake zote za zamani.
Kwa
sasa ATCL inasafiri katika maeneo 8 nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na
Mtwara, Mwanza, Tabora, Kigoma, Dar es Salaam, Mbeya, Bujumbura na
Moroni nchini Comoro.