Sifael Paul na Erick Evarist
SAKATA la maridhiano kati ya Mkurugenzi wa Uzalishaji Vipindi wa Clouds Media Group, Rugemalila Mutahaba na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi a.k.a Sugu au Mr II, limeibua gumzo kubwa miongoni mwa wadau wa burudani Bongo, Ijumaa lina full stori.
TUJIKUMBUSHE
Jumanne wiki hii, Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu walicheza kama Pele walipofanikisha makubaliano kati ya Ruge na Sugu ambao wamekuwa wakisuguana kwa muda mrefu.
Ilifahamika kitambo kuwa wawili hao wana mgogoro wa kimaslahi hasa kuhusiana na haki za wasanii wa muziki wa Bongo Fleva ambapo Sugu alikuwa akimtuhumu Ruge kuwanyonya.
Pia sababu nyingine ya kutibuana kwa wawili hao ni studio iliyotolewa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete na kupewa THT pamoja na hatua ya Kituo cha Redio cha Clouds kutopiga nyimbo za baadhi ya wasanii.
WAZIRI NCHIMBI
Akizungumza katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo mara baada ya makubaliano hayo yaliyofikiwa kwenye ofisi ya Dk. Nchimbi, waziri huyo alisema:
“Wamekubaliana na kusaini kumaliza tofauti baada ya kufanyika kikao cha mwisho cha upatanishi ambapo katika zoezi hilo, pande zote ziliridhika kuwa msingi wa mgogoro wao ni kuamini kwamba upande mmoja hauutendei haki upande mwingine.
RUGE
Kwa upande wake Ruge alikuwa na haya ya kusema:
“Tumepanga mikakati ya jinsi tutakavyokuwa tunakutana kuendelea kusaidia sanaa yetu hii, ni kweli kabisa tumekubaliana bila shinikizo lolote, tunaamini sasa ni hatua ya kusogea mbele, tuachane na yaliyopita.”
SUGU
Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Sugu alifunguka:
“Tulikuwa katika vita na vita lazima ifike mwisho labda iwe ni vita isiyo na malengo ndiyo haitaki suluhu, lakini kama ilikuwa na malengo, ina maana inapopatikana fursa ya suluhu kama kweli ulikuwa na dhamira ya dhati kwa kile unachokipigania, lazima ukubali kukaa chini na kutafuta suluhu ili tusonge mbele.”
SUGU ASAMBAZA TAARIFA KWA MASHABIKI WAKE
Hata hivyo, baadaye Sugu ambaye ni kiongozi wa Vinega (wasanii walio nyuma ya harakati za Sugu) alisambaza taarifa kwa mashabiki wake akiwataka kuelewa kile kilichotokea na kuwa ni matunda kwa sanaa hapa nchini.
WARAKA MZITO WA VINEGA
Jumatano wiki hii Kundi la Vinega kupitia chama cha TUMA chini ya mwenyekiti wake, Fredy Malick ‘Mkoloni’, walitoa waraka wao uliosomeka:
“Tunapenda kupongeza mafanikio yaliyotokana na mixtapes za Anti-Virus kwani ndiyo yaliyosababisha muafaka uliokuwa umetugawa wasanii na kutufanya tukose haki yetu ya msingi kama chombo pekee chenye dhamana ya kupokea misaada kutoka ndani na nje ya nchi na badala yake chama cha TUMA kinakwenda kuwa chombo cha wasanii kwa wale waliopo na watakaoendelea kujisajili.
“Tunafurahi sana na kupongeza jitihada za makusudi zilizochukuliwa na serikali kupitia wawakilishi wake, yaani Dk. Nchimbi na Mhe. Lissu kwa kutambua hoja za Vinega zilikuwa za msingi.
“Tunasisitiza umoja na kujiamini bila kuyumbishwa na kwa kuzingatia hili tunapenda watu wajue kuwa vita yoyote lazima iwe na malengo.”
HUKO NYUMA
Sekeseke la Sugu na Ruge lilianza kitambo hata kabla ya mbunge huyo kulalamika kuibiwa mradi wa Malaria No More akimtuhumu Ruge kuhusika kwani wakati akizindua albamu yake ya Veto alilalama tena kubaniwa na jamaa huyo, lakini sasa mambo shwari.
PONGEZI
Baada ya upatanisho huo, baadhi ya watu waliozungumza na Ijumaa kwa nyakati tofauti waliwapongeza Mhe.Nchimbi na Lissu na wangine waliochangia kufikia hatua hiyo.
Aidha, wadau hao waliwapongeza Sugu na Ruge kwa kuamua kufungua ukurasa mpya utakaokuwa na manufaa kwa vijana wengi hapa nchini.
KUTOKA IJUMAA
Maneno ya Sugu yanagusa wengi kuwa vita lazima ifike mwisho labda iwe ni vita isiyo na malengo, hivyo tunawapongeza wawili hao kwa hatua waliyofikia na sasa kazi ni moja tu, kuendeleza sanaa yetu inayotoa ajira kwa jamii pana. Hongera Ruge, hongera Sugu-Mhariri.
CHANZO: GPL
0 comments:
Post a Comment