Na Salma Said – Zanzibar
Ni mwenye furaha usoni mwake, huwezi kuamini kama ni mgonjwa huwezi
kukubali kama ana machungu ndani ya moyo wake kwa kuwa sura yake ni ya
kutabasamu wakati wote na kuonesha matumaini ya kuishi kwa amani lakini
utagundua tu pale utakapomsikiliza kwa umakini sana katika maelezo yake
na ukimtulizia jicho ndipo utakapogundua kama kweli kijana Mansoor Hamad
Saleh (21) ana majonzi na maumivu makali anayoyapata katika kiwiliwili
chake.
Ni miaka mitatu sasa tokea Mansoor alipoanza kulala kitandani kutokana
na matatizo ya kupooza miguu yake yote miwili chanzo chake khasa cha
ulemavu huo kilikuwa ni kuanguka juu ya mnazi huko Maangwe Wete Pemba
alipokuwa amepanda kwa ajili ya kuangua nazi kwa ajili ya matumizi ya
nyumbani kwao.
Mansoor ni mwanafunzi wa kitatu cha pili ambaye alikuwa akijitayarisha
na kufanya mitihani lakini kwa bahati mbaya sana kabla ya kuanza tarehe
za mitihani alipata mtihani mkubwa wa kuanguka kutoka juu ya mnazi hadi
chini na kusababisha matatizo makubwa ya kumlaza kitandao hadi leo hii
akiwa hana matumaini tena katika maisha yake.
Hata hivyo Mansoor anajipa moyo kwamba iwapo atatibiwa na atafanikiwa
kupata fedha za kumfikisha nchini India ataweza kurejea katika hali yake
ya kawaida na amekuwa akiomba apate matibabu hayo ili aweze kurejea
shuleni kuendelea na masomo yake kama kawaida.
Awali Mansoor alipoanguka kutoka juu ya mnazi miaka mitatu iliyopita
alikimbizwa katika hospitali ya Chake Chake Kisiwani Pemba na alilazwa
hapo kwa muda wa mwaka mmoja chini ya uangalizi wa Daktari Shaaban wa
hospitali hiyo kabla ya kusafirishwa na kuletwa Unguja katika Hospitali
Kuu ya Mnazi Mmoja kwa amtibabu zaidi lakini licha ya matibabu hayo ya
mwaka mzima hakuweza kupata nafuu na bado yupo kitandani.
Kwa kuwa ni kijana mdogo hapendi kulala muda wote na amekuwa akipenda
sana kujishughulisha ingawa hawezi lakini anajilazimisha kukaa ingawa
kwake yeye ni vigumu kukaa katika kiti muda mrefu lakini amekuwa
akijaribu kukaa na kulala mara kwa mara.
“Napenda niendelee kusoma lakini siwezi kwenda skuli na hiki kigari
changu kwa sababu kila wakati naumia sana mgongo wangu kwa hivyo
inanibidi kila wakati nilale kidogo ninyanyuke nikae kidogo nikale
kidogo hivyo hivyo kutwa nzima na nikijilazimisha basi naumia sana”
alisema huku akionesha kukunja uso kwa maumivu.
“Sehemu ya kiuno hadi miguu kwenye nyayo iliathirika na kutofanya kazi
na Ex Rays zinaonesha kuwa ameumia maeneo ya uti wa mgongo” imesema
ripoti yake ya hospitali.
Licha ya matibabu aliyofanyiwa Mansoor alipatiwa madawa mbali mbali ya
kuamsha hisia za mwili wake na kuondosha maumivu, kulazwa katika sehemu
maalumu ili kunyoosha mgongo wake vile vile kufanyiwa mazoezi mepesi ya
kusimamishwa ili viungo vyake viweze kufanya kazi katika kipindi chote
cha kuumwa kwake lakini matibabu hayo hayajaweza kuleta mafanikio.
Mansoor baada ya kufanyiwa vipimo vya Computer Tomography Scan (CT SCAN)
vinaonesha athari aliyoipata katika mgongo wake anahitajika
kusafirishwa na kupelekwa India kwa matibabu kwani ameumia katika uti
wake wa mgongo.
Kwa mujibu wa maoni ya madaktari wameshauri Mansoor kupelekwa India
kufanyiwa operesheni kwa kuwa operesheni yake haiwezi kufanyika hapa
ncini Tanzania na hivyo kila anapoendelea kukaa madhara yanaweza
kuongezeka zaidi.
Mansoor anahitaji kusafirishwa kupelekwa nchini India kwa matibabu na
kwa mujibu wa madaktari waliomchunguza wanasema ni jumla shilingi
millioni 20 zinahitajika kwa makisio ya matibabu yake ya kumfikisha
nchini humo.
Makisioa ya fedha hizo ni pamoja na gharama za usafiri kutoka Zanzibar
hadi India, vipimo vya uchunguzi, matibabu na gharama za malazi na fedha
ya kufuatana na Daktari dhaZ Q1 mana atakayeweza kuondoka naye hapa
nchini hadi India.
Matatizo yake makubwa kwa sasa Mansoor ni kuwa hawezi kusimama kwa vile
amepata athari katika viungo vyake vya chini (Nyayo) kukosa hisia na pia
hawezi kuzuwia choo kutokana na kuathirika kwenye uti wa mgongo.
Wazazi wa Mansoor wamekuwa wakitafuta misaada mbali mbali kutoka kwa
watu lakini bado hawajafanikiwa kukusanya kiasi chochote cha fedha licha
ya kuandika barua kadhaa kwa wafadhili “Sisi wazee wake Mansoor baba na
mama wazazi sote ni masikini sana hatuna uwezo wa kumsafirisha mtoto
wetu kwa ajili ya matibabu, mtoto wetu anakabiliwa na ulemavu wa kudumu,
tunaleta kilio chetu kwa lengo la kupata msaada wa tiba ya mtoto wetu
huyu wa kwanza” imesema moja ya barua yao ya maombi wazee hao ya hivi
karibuni ambayo iliandikwa 15/9/2013.
Bi Farashuu Mansoor Mohammed ni mama mzazi wa Mansoor mwenye familia ya
watoto wanane kati yao ni wanawake wawili na Mansoor ndio mtoto wake wa
kwanza anashukuru kuona mwanawe upo hai bado licha ya hali mbaya na ya
kusikitisha kutokana na maumivu ayapatayo mwilini mwake.
“Mwanangu alikuwa akijitayarisha na mitihani ya darasa la kumi na mbili
lakini akapata mtihani huu maana na huu ni mtihani mwengine mkubwa zaidi
ya huo mtihani wake wa darasani” alisema Mama Mzazi wa Mansoor, Bi
Farashuu
Bi Farashuu mwenye watoto saba kati ya hao wanawake ni wawili anasema
amefanya juhudi mbali mbali za kutafuta misaa kwa ajili ya kumuokoa
mwanawe ili aweze kurejea katika afya yake lakini ameshindwa kutokana na
familia yao kuwa masikini sana na haina uwezo wa kuchangishana fedha
kwa ajili ya matibabu ya mwanawe huyo.
“Jamaa zangu wanataka kunisaidia lakini jambo kubwa wamenambia wao hata
familia nzima ikichangishana haitaweza kupata hata milioni tano na ndio
maana nakuwa napata wakati mgumu na wakati mwengine nachanganyikiwa
nikimuona mwanangu anavyoteseka na maumivu” alisema huku akiwa na uso wa
huzuni sana.
Bi Farashuu anasema mwanawe amekuwa akitaja mara kwa mara kufanya kazi
iwapo atakosa matibabu na kushindwa kuendelea na kusoma hivyo
angependelea kufanya kazi gereji kutengeneza magari.
Mansoor anapoletewa supu kwa ajili ya kunywa ili kurejesha afya yake
amekuwa akisema bora hao kuku anaoletewa kwa ajili ya supu apewe
mwenyewe aweze kuwafuga waweze kuendeshea maisha yao yeye na ndugu zake
wengine.
“Mwanangu ameshakata tamaa kama baba yake na ndio maana nakhisi kama
hatokuwa tena na akili ya kuendelea na masomo na ndio maana anakuwa
anataja sana kutaka kufanya kazi gereji kutengeneza magari” alisema Bi
Farashuu.
Ameongeza pia kusema “Aanapoletewa supu anywe basi anawaambia nileteeni
hao kuku nitafuga mwenyewe kwa sababu akifuga atapata pia kuuza na
watazaa wengine na hivyo atapata kuendeleza mifugo na pia atasaidia
ndugu zake” alisema ambapo hivi sasa ameshapata makoo wawili kwa ajili
ya kuwafuga.
Mansoor anahitaji kupata banda la kuku dogo ili aweze kuwaweka kuku wake
ambao wameletewa na jamaa zake baada ya kukataa kupikiwa supu kwa ajili
ya kuimarisha afya yake “Nikifuga kuku nitapata kuchinja nipate supu
lakini pia nitapata pesa kwa ajili ya kuwasaidia wenzangu” alisema
Mansoor.
Baadhi ya majirani wanasema maisha ya Bi Farashuu na Mume wake Bwana
Hamad Saleh ni magumu wakati mume hana kazi ya kufanya Bi Farashuu
anahangaika na kupika maandazi kwa ajili ya kuendeleza maisha yake na
familia yake.
“Mwanadishi ngoja mimi nikuambie ukweli maana yeye mwenyewe anaona aibu
kusema kwa kweli maisha yake ni magumu sana kuliko unavyomuona hapa
maana ananunua unga na kukanda maandazi 20 kila siku na maandazi hayo 10
anauza na maandazi 10 anakula na wanawe kila mtoto anakula andazi moja”
alisema Sada Hamed Rashid ambaye ni jirani yake.
Kufuatia hali yao ngumu ya maisha na wanataka kumtibu mtoto wao wameamua
kuuza nyumba yao kwa tahamani ya shilingi millioni 30 lakini tokea
wameanza kutangaza bei hadi leo hii haijanunuliwa huku baadhi ya jamaa
zao wakikataa nyumba hiyo isiuzwe kutokana na kuwa watapata tabu na
kukosa sehemu ya kuishi.
“Jamaa zangu wengi wamenishauri tusiiuze nyumba yetu wanasema tutapata
tabu ya makaazi ya kujisitiri mimi na wanangu lakini hali ndio ngumu
mtoto anateseka kwa hivyo lazima tutafte namna ya kutatua tatizo hili
lakini pia ni mtihani maana hiyo nyumba pia hatujapata mteja” alisema Bi
Farashuu.
Idadi ya watu wenye kupata ulemavu imekuwa ikiongezeka kufuatia kuanguka
juu ya minazi lakini zaidi wanaoanguka juu ya mikarafuu ambapo baadhi
yao huvunjika viungo vya miili yao na wengine kupooza na kuwa walemavu.
Kwa mujibu Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui
amesema ni kweli wapo watu ambao huanguka mikarafuu lakini idadi haifiki
200 kwani baadhi yao kati ya hao wanaotajwa ni wameanguka mikarafuu,
Minazi na wengine wamepata ajali mbali mbali ikiwemo Vespa na Gari hivyo
ndio maana idadi inaonekana ni kubwa zaidi lakini katika kipindi cha
mwaka jana wizara yake imeshuhudia watu watatu walioanguka mikarafuu
ambao wamepata majeraha na ulemavu.
Msomaji wa Makala hii kumbuka kwamba kutoa ni moyo na sio utajiri kwa
hivyo utakachoweza kutoa wewe toa tu na kitasaidia hata kama ni shilingi
elfu tano (5,000) utakuwa umemsaidia Mansoor katika matibabu yake kwani
hii ni sadaka yako na utakuwa unamkopesha Mwenyeenzi Mungu na bila ya
shaka utakikuta mbele ya safari Inshallah.
Mtu ambaye ataguswa na matatizo ya Mansoor awasiliane na Mwananchi
Communications Ltd kwa simu nmba +255754780647 au wasiliana moja kwa
moja na Mwandishi wa Makala hii Salma Said kwa email muftiiy@yahoo.com
au simu +255777477101 au Tigo Pesa +255657570000 Amour Ali Muhsin au
Hassan Khamis London kwa simu +44 7588550153, Paypal
hassan.mussa@gmail.com
0 comments:
Post a Comment