SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Tuesday, June 21, 2016

MAPENDEKEZO YA JOPO LA JK YAANZA KUTEKELEZWA- BAN KI MOON

Na Mwandishi Maalum, New York
Umoja wa Mataifa  na Shirika la Afya Duniani  ( WHO), ni baadhi ya   Taasisi za Kimataifa  ambazo zimeanza kutekeleza kwa vitendo sehemu  ya  mapendekezo na ushauri uliotolewa na Jopo  la  Ngazi ya Juu kuhusu Mwitikio wa Kimataifa wa Majanga ya Kiafya.
“ Tumeanza kutekeleza baadhi ya mapendekezo ya   Jopo lililokuwa chini ya  Uenyekiti wa Rais Mstaafu wa Tanzania, Mhe, Jakaya Mrisho Kikwete. Mhe. Rais nakushukuru sana kwa uongozi wako, ushiriki wako na mchango wako.  Nimefarijika kwamba umeweza kuungana nasi katika mkutano huu kutokea Senegal, kuzungumzia  mapendeko ya  Jopo lako”. Akasema   Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Ban Ki Moon, ameyasema hayo, jana  (  jumatatu) wakati wa  mkutano  usio  rasmi wa Baraza   Kuu la Umoja wa Mataifa, ulioandaliwa na Rais wa Baraza hilo, Bw Mogens Lykketoft kwa lengo la  kupokea   Ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu uimarishaji na usanifu wa huduma za Afya Kimataifa: utekelezaji wa mapendekezo ya  Jopo la Ngazi ya juu kuhusu  Mwitikio wa Kimataifa wa Majanga ya Kiafya.
Baadi ya  mambo  ambayo yameanzwa kutekelezwa kwa  mujibu wa Katibu Mkuu  yanahusu Shirika la Afya Duniani  ambapo katika mapendekezo yake,  Jopo limeainisha kutambua kuwa WHO   inabaki kuwa taasisi  kiongozi linapokuja suala   la afya wakati wote na hususani wakati wa  majanga ya dharura ya  milipuko ya magonjwa.
 “ Jopo  limependekeza  kuwa uwezo wa  WHO katika kuitika yanapotokea majanga ya  dharura ya  kiafya unatakiwa kuimarishwa wakati wote  na   kutokana na mapendekezo ya Jopo WHO  imeanzisha mpango wa dharura, unaokipa chombo  hicho  uwezo wa  kuwajibika kwa haraka na kwa wakati pale unapotokea mlipuko wa  ugonjwa”. Amebainisha  Ban Ki Moon.
Pendekezo la pili mbalo limeanza kufanyiwa kazi na  Umoja wa Mataifa ni lile la  kuimarisha  mifumo ya Umoja wa  Mataifa hususani wakati wa matukio ya  dharura  yanayohusu milipuko ya magonjwa hivyo kuwa na  uwajibikaji   wa pamoja kupita  Taasisi zake.
“ Tatu nimeridhishwa na hatua ya Banki ya Dunia  ya kuzindua mpango wa dharura wa uwezeshaji wa kifedha pale  yanapotokea  majanga ya dharura ya kiafya, ni mpango ambao utatoa uhakika  fedha dhidi ya  majanga  na utafanya kazi  kwa ushirikiano wa karibu na WHO”. Ameeleza Ban  Ki  Moon.
Akielezea zaidi kuhusu  mapendekezo  yaliyopendekezwa na Jopo lililoongozwa na  Rais  mstaafu Kikwete. Ban Ki Moon amesema. 
“ Mwezi  April mwaka  jana, niliunda  Jopo la  Ngazi ya Juu   kuhusu ya  Mwitikio wa Kimataifa wa  Majanga ya Kiafya   ili  litoe mapendekezo  ya namna ya kuimarisha mifumo ya  kitaifa na kimataifa katika  kuzuia na kudhibiti changamoto za  majanga ya kiafya katika siku za baadaye.Mwezi februari mwaka huu,   Jopo   liliwasilisha  Ripoti yake ikianisha mapendekezo 27   yanayotakiwa kufanyiwa kazi  kuanzia ngazi ya  taifa,  kanda na kimataifa”.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa,  ameyataja  baadhi  ya maeneo   ambayo yamesisitizwa na   Jopo kuwa ni pamoja na,  kuifanya mifumo  na miundo mbinu ya  utoaji wa huduma za afya kuwa  imara  na katika hali ya  utayari  wakati wote  kukabiliana na majanga ya dharura,  umuhimu wa tafiti za kisayasi, uhakika wa raslimali fedha ya kutosha na uwezeshaji kupitia miradi ya maendeleo.
  Kwa mujibu wa Ban Ki Moon,  mapendekezo ya  Jopo hilo  yamepitiwa kwa uangalifu mkubwa kupitia majadiliano  miongoni mwa, na  baina ya  Taasisi za Umoja wa Mataifa. 
Na  baada ya majadiliano hayo,  Mkuu huyo wa UM ameandaa  taarifa yake ambayo imepewa kichwa cha : Uimarishaji wa Mifumo ya  Afya ya Kidunia: Utekelezaji wa    Mapendekezoya Jopo  la Ngazi  ya  Juu kuhusu Mwitikio wa Kimataifa wa Majanga ya  Kiafya.
“ Jopo  lililongozwa na  Mhe  Kikwete limetupatia mapendekezo ya msingi na yenye tija ambayo  kwayo ni kwa namna gani mifumo ya  kijamii,  kitaifa na kimataifa itakavyoweza kwa njia sahihi kujiandaa kukabiliana na majanga ya dharura ya kiafya katika siku  za usoni. Mimi binafsi ninataka kujihusisha kikamilifu katika utekelezaji wa mapendekezo ya Jopo hili” akasisitiza  Katibu Mkuu.
 Na katika kuhakikisha kwamba utekelezaji wa mapendekezo ya Jopo  yanasimamiwa na kufuatiliwa  kwa ukaribu, Ban Ki Moon  ameunda  Kikundi kazi  kitakachojulikana kama Global Health Crises Task Force ambacho moja ya majukumu  yake makuu yatakuwa ni  pamoja na  kufuatilia,  ku- ratibu na  kuunga mkono utekelezaji wa mapendekezo ya   Jopo.
Kikundi kazi hicho  kitaongozwa na  Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw, Jan Eliasson,  Mkurugenzi Mkuu wa WHO.  Dr. Margareth Chan, Dr. Jim Yong Kim Rais wa Banki ya Dunia, na  Dr. David Nabarro, ambaye ni  Mshauri  Maalum wa Katibu Mkuu  kuhusu utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ( Agenda 2030) na  Makubalino kuhusu  Mabadiliko ya Tabia nchi  ( Paris Agreement ).
Kwa  upande wake, akiongea kwa njia ya  mtandao video ( Video   Conference) kutoka nchini Senegal,Mwenyekiti wa Jopo, Rais Mstaafu  Jakaya Mrisho Kikwete   pamoja na kumshukuru, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kwa  kumkabidhi jukumu hilo  pia alianisha baadhi ya  mambo kadhaa ambayo  Jopo lake   liligundua wakati wa utekelezaji wa  hadidu za rejea.
Baadhi ya   mambo ni pamoja na, WHO  kuchelewa kutamka haraka na kwa wakati kwamba kuibuka kwa ugonjwa wa Ebola  kulikuwa ni janga la   kimataifa na lilotakiwa kuchukuliwa  hatua  za haraka  kuzuia maafa yaliyojitokeza.
Kwamba, WHO haina  raslimali fedha  jambo ambalo   inabidi  itegemee zaidi michango na hisani za  mataifa makubwa.
 Kwamba,  nchi nyingi hususani zile zinazoendelea mifumo  na   miundo mbinu ya  utoaji wa huduma za afya zikiwamo za afya ya msingi bado ni dhaifu mno  kiasi kwamba   kwa vyovyote vile ilishindwa , inashindwa na itashindwa  kukabiliana na   changamoto  za  majanga  ya dharura ya  milipuko ya magonjwa kama vile ilivyokuwa kwa Ebola na sasa  Zika na tishio la Homa   ya ugonjwa wa manjano.
Rais Mstaafu Kikwete katika  maelezo  yake,  amesititiza kwamba,  udhaifu huo   hauishi katika nchi   moja moja bali pia unakwenda hadi   ngazi ya Kikanda na Kimataifa.
“ Jopo letu   limegundua kwamba,  maisha ya mamilioni ya  watu yatakuwa katika hatari kubwa sana  na dunia itakuwa katika mashaka makubwa pale ambapo   janga  kubwa la  magonjwa ya dharura yatakapoibuka na kukuta  mifumo  na miundo mbinu ya utoaji wa huduma za afya  haijaimarishwa  vya kutosha kukabili changamoto hiyo”. Amesisitiza   Rais Mstaafu
 Akaongeza  Kikwete kwa kusema “ Ni matumaini yangu kuwa mapendekezo 27 yaliyotolewa na  Jopo nililoliongoza yatatusaidia kufika huko tunakotaka kufika. Uungaji mkono wako binafsi  Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  ukichagizwa na utashi wa kisiasa wa viongozi mbalimbali  katika ngazi ya juu kadri itakavyowezekana utasaidia sana katika ufanya mambo yaende”.
Ni katika kutambua uzito wa  dharura  itokanayo na magonjwa ya  milipuko,   MwenyeKiti wa Jopo   Kikwete amesema  Jopo  limependekeza pia kwamba kwanza,  kuanzishwe Baraza la   Ngazi ya Juu Kuhusu  Majanga ya Dharura ya  Afya ya Jamii, na  pili,  kuitishwa kwa  Mkutano wa  Ngazi ya Juu kuhusu  Majanga ya Kiafya mwaka 2018.

0 comments:

Post a Comment