Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF),Bw. Godfrey Simbeye
akizungumza katika warsha ya kutathimini, kuongeza kasi na ubora katika
Utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji
nchini jana jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Dkt. Florens Turuka na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani, Bw.
Mbarak Abudulwakil (katikati).
Katibu
Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Florens Turuka akizungumza katika
warsha ya kutathimini, kuongeza kasi na ubora katika Utekelezaji wa
mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini jana
jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta
Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali
imewahakikishia wafanyabiashara kuwa itaendelea kuboresha mazingira ya
biashara za mipakani ili kuvutia uwekezaji kwa ustawi wa jamii na
uchumi.
Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Florens Turuka aliwaambia waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam jana kuwa swala hilo ni la muhimu na la
msingi sana kama nchi inataka kuzidi kuboresha mazingira ya uwekezaji na
kufikia maendeleo endelevu. “Katika utaratibu wa soko huria ni wajibu
wa serikali kuweka mazingira mazuri ya biashara na kuleta ustawi na
ushindani kwa sekta binafsi kwa ajili ya maendeleo,” alisema.
Alisema
sekta binafsi inapokuwa na mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji
inasaidia kukuza uchumi, kuongeza ajira na upatakanaji wa mapato ya
serikali.
Alifafanua
kwamba mazingira ya biashara na uwekezaji yanapokuwa magumu wanaoteseka
ni wananchi wa kawaida kutokana na kukosa ajira na huduma muhimu.
Alisema
pamoja na kwamba mazingira yaliyopo bado hayakidhi vigezo vya
kimataifa, serikali inashirikiana na sekta binafsi katika kuboresha
mazingira hayo.
Alisema
maboresho yaliyofanywa yamesaidia biashara na uwekezaji kufanya vizuri
na hatua zaidi zinachukuliwa za kuboresha sera na sheria ili hata uchumi
uweze kukua kwa asilimia 10 kwa mwaka. Alisema azma hiyo ni ya dhati
katika kuhakikisha mazingira yanakuwa wezeshi, na kuchochea wananchi
kutumia fursa na rasirimali zilizopo kuchangia uchumi wa taifa.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania
(TPSF), Bw. Godfrey Simbeye alisema mpango wa kuimarisha biashara
mipakani ukizingatiwa utasaidia sana kuimarisha biashara na uwekezaji.
Mpango huo unawaleta pamoja wataalamu kutoka sekta ya umma na
wawakilishi wa sekta binafsi kuchambua, kupanga na kutathmini hatua za
kuboresha mazingira ya biashara katika maeneo ya mipaka.
Alisema
lengo lake ni kuainisha vikwazo na hatua ambazo wizara na taasisi za
serikali zinahitajika kuchukua kwa kipindi cha muda mfupi, muda wa kati
na muda mrefu kuboresha mazingira hayo. Akitoa mfano alisema biashara za
mipakani imekuwa na vikwazo vingi ambavyo vinajadiliwa kupata ufumbuzi
ili bidhaa kutoka bandari ya Dar es Salaam ziweze kwenda nje ya Tanzania
bila vikwazo.
Alisema
Wizara ya Mambo ya Ndani imejitahidi kurekebisha mazingira hayo na sasa
warsha hii itasaidi sana kupata ufumbuzi zaidi wa biashara za mipakani.
Alisema
sekta binafsi, imeunda vikosi kazi vinne ambavyo kazi yake ni
kufuatilia utekelezaji wa mpango huo kuanzia kuanzisha na Kufunga
Biashara, Biashara za Mipakani, Upatikanaji wa Vibali vya Ujenzi na
Kuandikisha Raslimali.
Alisema
tathmini iliyofanyka Machi mwaka 2012 na mshauri elekezi kuhusu
utekelezaji wa mpango huo inaonyesha kuwa kati ya hatua 193 zilizotakiwa
kuchukuliwa, ni 43 tu ikiwa sawa na asilimia 22 tu zilizotekelezwa
kikamilifu.
Alisema
taarifa za Benki dunia zinazotolewa kila mwaka zinaonyesha Tanzania
bado ipo chini katika kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji
ukilinganisha na nchi 185 duniani. Alisema Rais wa Jakaya Kikwete
alianzisha mchakato wa Tanzania kuboresha nafasi yake kimataifa katika
wepesi wa kufanya biashara kutoka nafasi ya 120, hadi chini ya 100
ifikapo 2011.
Alisema
pia hadi kufikia mwaka huu Tanzania bado haijapiga hatua ya kuridhisha
na kwamba bado kuna changamoto zinazohitaji utelekezaji kufikia hatua
hiyo. Washa hiyo ya siku mbili ilishirikisha washiriki toka sekta ya
umma na binafsi kufanya tathimini, kuongeza kasi na ubora katika
utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
0 comments:
Post a Comment