Tarehe 5 Juni,2012, mfanyakazi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), ambaye amelemaa baada ya kupata ajali ya gari, Bwana Athumani Hamisi (pichani), aliitisha mkutano wa waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Maelezo, Dar es Salaam, na kutoa taarifa iliyojenga taswira kuwa ametelekezwa na TSN pamoja na Serikali.
TSN inapenda kufafanua kuwa Serikali na kampuni hii, ambayo ilimwajiri Athumani tarehe 1/09/2006 kama Mpiga picha Mwandamizi, wamemhudumia mfanyakazi huyo kikamilifu tangu alipopata ajali tarehe 12 Septemba, 2008 hadi sasa, na huduma hiyo inaendelea.
Baada ya kutokea ajali hiyo, TSN kama mwajiri ilisimamia matibabu yake ya awali katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili Kitengo cha Mifupa (MOI) mpaka Serikali, kwa kupitia Wizara ya Afya ilipomhamishia Netcare Rehabilitation Hospital nchini Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.
Serikali ililipia gharama za matibabu yake yote akiwa Afrika Kusini kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi saba, ambayo yanazidi shilingi milioni mia moja.Gharama hizo ni pamoja na ununuzi wa kigari maalum ambacho Athumani anatumia sasa.
TSN kama mwajiri ililipa nauli ya ndege kwenda na kurudi pamoja na posho ya kujikimu ya mgonjwa pamoja na ndugu wasindikizaji ambao ni Bw. Hassan Hussein na Bi. Mirriam Malaquias.Posho ya kujikimu ilikuwa USD 6,210 sawa na Shilingi 9,315,000, na nauli kwa watu watatu ilikuwa ni Shilingi 3,535,869.92. Athumani aliendelea kupatiwa huduma akiwa huko Afrika Kusini kwa gharama za Serikali na TSN mpaka aliporejea nchini tarehe 08/05/2010. Gharama zilizolipwa na kampuni kwa mfanyakazi huyu hadi sasa ni takriban shilingi million 52.
Athumani aliporejea nchini alilakiwa na wafanyakazi na viongozi wa TSN na kupangiwa chumba hoteli ya Holiday Inn wakati utaratibu wa kumtafutia nyumba ya kupanga ukikamilishwa. Kampuni ilitumia kiasi cha Shilingi 1,756,979.50 kulipia hoteli. Baadaye alipelekwa kwenye nyumba ambayo alipangiwa na Kampuni katika eneo la Sinza Vatican ambapo ndipo bado anaishi hadi hivi sasa. Gharama ya nyumba kwa mwaka wa kwanza 2010 ilikuwa ni Shilingi 4,200,000 au Shilingi 350,000 kwa mwezi. Mwaka 201 mwenye nyumba alipandisha kodi hadi 400,000 kwa mwezi ambapo Kampuni ililipia Shilingi 4,800,000. Kodi hiyo imeishia Mei mwaka huu na kampuni imeshafanya mazungumzo na mwenye nyumba ili Athumani aendelee kuishi hapo kwa muda wakati mipango endelevu ya ustawi wake inafanywa kwa kuzingatia taratibu za ajira.
Mnamo tarehe 8/12/2010 Athumani alirudi tena Afrika Kusini kwa ajili ya uchunguzi wa maendeleo ya afya yake na matibabu yaligharimiwa na Serikali wakati TSN iligharamia nauli yake na ya muuguzi wake, pamoja na posho ya kujikimu Shilingi 6,300,000/-.
Pamoja na bwana Athumumai kulala kitandani kwa muda wote huo ameendelea kulipwa mshahara kamili bila kukatwa kama mfanyakazi wa kawaida ikiwa ni msaada wa kampuni kwa kuzingatia ulemavu alioupata.Mshahara aliolipwa kwa muda wote aliokuwa anaugua ni kiasi cha shilingi 26,773,000. Vile vile kampuni ilimlipa muuguzi toka Afrika Kusini ambaye alikuwa anamhudumiaa Athumani Rand 12,500 kama mshahara wake.
Kuanzia Januari 2011, mshahara wa Athumani umejumuisha asilimia 15 kama posho ya nyumba ambayo wafanyakazi wote wanalipwa. Aidha Athumani yupo kwenye mpango wa bima ya afya anayolipiwa na kampuni, ambayo inamwezesha yeye na familia yake kuweza kutibiwa katika hospitali yoyote hapa Tanzania. Kampuni inamlipia Shilingi 68,449.20 kila mwezi na bima hiyo ndiyo inayogharamia matibabu yake yote hapa nchini.
Bwana Athumani anapatiwa usafiri na TSN mara mbili kwa wiki kumtoa nyumbani hadi Muhimbili na kurudi kwa ajili ya mazoezi ya viungo.
0 comments:
Post a Comment