Robo fainali ya kwanza ya Kombe
la Dunia nchini Afrika Kusini itakutanisha mabingwa mara tano Brazil na
Uholanzi siku ya Ijumaa mjini Port Elizabeth, baada ya timu hizo kufuzu
kufuatia ushindi wa Jumatatu.
Brazil iliendelea kudhihirisha azma yake ya
kulitwaa kombe hilo kwa mara ya sita ilipowafunga Chile mabao 3-0 katika
uwanja wa Ellis Park mjini Johannesburg.
Awali katika uwanja wa Moses Mabhida mjini
Durban, Arjen Robben na Wesley Sneider walifunga mabao yaliyoiwezesha
Uholanzi kuishinda Slovakia 2-1 na hivyo kujiandikishia nafasi miongoni
mwa nane bora.
Mabao ya Brazil dhidi ya Chile yalipatikana
kupitia mlinzi Juan aliyefunga kwa kichwa katika dakika ya 38, kabla ya
Luis Fabiano kuongeza la pili dakika 4 baadaye.
Robinho alifunga bao la tatu na la ushindi kwa
Brazil katika dakika ya 59 kufuatia pasi kutoka Ramires.
Uholanzi walionekana kuelekea kupata ushindi wa
mabao 2-0 dhidi ya Slovakia hadi muda wa ziada, wakati mlinda mlango
Maarten Stekelenburg alipomwangusha Martin Jakubo kwenye eneo la hatari,
na hivyo Slovakia wakapata penalti iliyofungwa na Robert Vittek.
Uholanzi haijapata kushinda Kombe la Dunia na
imeshafikia hatua ya fainali mwaka 74 na 78, na wakati huu wanajitahidi
kutimiza hamu ya kutwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza.
Robo fainali nyingine siku ya Ijumaa itakuwa
kati ya Ghana na Uruguay katika uwanja wa Soccer City mjini
Johannesburg, hii ikiwa ni mara ya tatu katika historia ya Kombe la
Dunia kwa timu kutoka Afrika kufikia hatua ya nane bora.
Siku ya Jumamosi itafanyika robo fainali ya tatu
kati ya Ujerumani na Argentina katika uwanja wa Green Point mjini
Cape Town.
Timu zitakazochuana kwenye robo fainali ya
mwisho zitafahamika Jumanne, baada ya mechi za mwisho za raundi ya pili,
Paraguay ikicheza dhidi ya Japan mjini Pretoria huku Uhispania na Ureno
zikipambana mjini Cape Town.
****************************
Blatter aomba radhi kwa makosa ya waamuzi
Rais wa shirikisho la soka duniani Sepp Blatter
ameomba msamaha kwa ajili ya makosa yaliyofanywa na waamuzi kwenye Kombe
la Dunia, ambapo bao llilofungwa na Frank Lampard wa England dhidi ya
Ujerumani lilikataliwa, na pia kukubaliwa kwa bao la kuotea lililofungwa
na Carloz Tevez wa Argentina dhidi ya Mexico.
Bwana Blatter amesema mdahalo kuhusu haja ya
kutumia teknolojia kubaini iwapo mpira umevuka mstari wa goli au la
utaanzishwa upya kwenye mkutano wa bodi ya kimataifa ya vyama vya soka
utakaofanyika mwezi Julai.
Mkutano wa bodi hiyo uliofanyika mwezi Machi
uliamua kukataa kutumika kwa teknolojia hiyo kwenye Kombe la Dunia, kwa
tetesi kwamba kusimamisha mechi kwa ajili kuthibitisha kwenye video
ikiwa mpira umevuka mstari au la kutaathiri mtiririko wa mchezo na pia
kuzinyima timu fursa ya kufunga.
Mjadala kuhusu haja ya kutumika kwa teknolojia
hiyo uliibuka tena siku ya Jumapili wakati Ujerumani ilipoifunga England
mabao 4-1 mjini Bloemfontein na kuiondoa kwenye mashindano.
Kwenye mechi hiyo, mwamuzi kutoka Uruguay Jorge
Larriando na msaidizi wake walikataa kutambua kwamba mpira uliopigwa na
Frank Lampard katika dakika ya 38 ulivuka mstari wa lango la Ujerumani
na kuingia kabla ya mlinda mlango kuuondosha.
Bao hilo lingeiwezesha England kusawazisha kabla
ya mapumziko.
Baadaye siku hiyo katika uwanja wa Soccer City
mjini Johannesburg kulitokea utata mwingine kwenye mechi kati ya
Argentina na Mexico.
Mwamuzi aliruhusu bao la kwanza la Argentina
lililofungwa na Carlos Tevez akionekana kuwa ameotea.
Kulitokea mabishano makali uwanjani wakati wa
mapumziko baada ya tukio hilo kuonyeshwa tena kwenye skrini kubwa ndani
ya uwanja.
Blatter amesema amezungumza na vyama vya soka
vya England na Mexico na kuomba msamaha.
0 comments:
Post a Comment