Jerusalem:
Israel imesema itawaachia raia wote wa kigeni, ambao walikamatwa
na jeshi la nchi hiyo siku mbili zilizopita katika shambulio la umwagaji
damu lililofanywa dhidi ya meli iliyobeba misaada kuelekea Gaza.
Israel imechukua uamuzi huo kutokana na matakwa ya viongozi
duniani, ambao pia wametaka kufanyika kwa uchunguzi juu ya
shambulio hilo la Jumatatu, ambao ulisababisha vifo vya
wanaharakati tisa.
Katika mkutano uliofanyika mjini New York Marekani, wanachama
wengi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa waliilaani Israel na
kuitaka nchi hiyo kuondoa vizuizi ilivyoweka Gaza.
Msafara huo mdogo wa meli, ulikuwa umeandaliwa kwa pamoja na
kundi linalowaunga mkono Wapalestina pamoja na Shirika la Haki za
Binadamu la Uturuki.
Uturuki imesema watu wanne miongoni mwa watu tisa waliouawa, ni
raia wake na kuliita tukio hilo kama ugaidi wa kitaifa.
Wakati huo huo Serikali ya Israel imesema imewaachia kutoka
gerezani ilikokuwa ikiwashikilia wanaharakati wapatao 50 wa Uturuki
waliokuwa katika meli hiyo iliyobeba msaada na kwamba
watarudishwa kwao.
Waziri mkuu wa Japan atangaza kujiuzulu: Tokyo
Waziri Mkuu wa Japan Yukio Hatoyama ametangaza kuwa atajiuzulu
nafasi hiyo ya uwaziri mkuu, baada ya miezi isiyozidi tisa tangu
kushika wadhfa huo.
Hatoyama amekuwa katika shinikizo kutoka katika chama chake
kumtaka ajiuzulu kuelekea katika uchaguzi wa bunge unaotarajiwa
kufanyika nchini humo mwezi Julai.
Habari zinasema kuwa kutokana na kutotimiza ahadi yake ya wakati
wa kampeni, kuhamisha kituo cha jeshi la Marekani katika kisiwa cha
nchi hiyo cha Okinawa inafikiriwa kuwa ni sababu kubwa moja wapo
ya kumuangusha kisiasa Waziri Mkuu huyo wa Japan.
Deutsche Welle
0 comments:
Post a Comment