MGOMO wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kilichopo mkoani Dodoma umeingia siku ya pili leo. Mgomo huo umeanza jana baada ya wanafunzi kuamua kuacha masomo yao wakiishinikiza Bodi ya Mikopo kulipa pesa zao za mikopo kwa ajili ya kujikimu.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alilazimika kumtuma Naibu Waziri wa Afya Steven Kebwe na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa ili kuwatuliza wanafunzi hao waliokuwa wakidai kuishi katika mazingira magumu baada ya kukosa pesa za kujikimu na kufanya kushindwa kufuatilia masomo yao.
Hali hiyo ilionekana kama kutulia kwa muda, lakini leo yameibuka mapya baada ya wanafunzi hao kugoma tena wakiendelea kudai pesa zao za mkopo.
Akizungumza na mwandishi wetu, mwanafunzi mmoja wa UDOM (hakutaka kutajwa jina lake) alisema kuwa, "asubuhi ya leo tumegoma kuingia madarasani tukidai haki yetu, pesa zetu za mkopo hatujapata, tunaishi katika mazingira magumu.
"Maisha ya hapa chuo yamekuwa magumu sana, kwa mfano mimi nimekopa pesa kama laki moja mpaka sasa tangu hali hii ya kukosa 'boom' ianze lakini bado maisha yamekuwa magumu kwa upande wetu. Tunalazimika kula mara moja kwa siku. Tunaomba serikali isikilize kilio chetu tunapata shida sana, tunashindwa kufuatilia masomo yetu kwa kutumia muda mwingi kuwaza tutakula nini, tutaishi vipi na mpaka lini kwa hii hali."
Taarifa zimeendelea kueleza kuwa wanafunzi hao pia wamepigwa mabomu ya machozi na Jeshi la Polisi likiwataka kutawanyiaka eneo walilokuwa wamekusanyika na kwa sasa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kimezingira eneo lote la chuo na wanafunzi wapo mabwenini.
(HABARI NA GLOBAL WHATSAPP 0753 715779
0 comments:
Post a Comment