Nyota
wa muziki wa bongo flava nchini Diamond Platinumz amewataka wasanii wa
Tanzania kusambaza nyimbo zao kwa njia ya teknolojia kama vile Mziiki
iliyozinduliwa hivi karibuni ili ziweze kuwafikia watu wengi na kwa
wakati huohuo wanamuziki pia kunufaika na jasho lao.
Diamond
anasema kuwa ameamua kazi zake kuziingiza sokoni tofauti na kazi zake
za nyuma ambapo baada ya kushauriana na wadau anaoshirikiana nao kikazi
ameamua aingie sokoni kwa njia ya kidigitali kupitia programu ya Mziiki
iliyozinduliwa hivi karibuni ambayo pia yeye ni balozi anayeitangaza.
Anasema
Tanzania ina wanamuziki wengi wenye vipaji lakini wamekuwa wakikabiliwa
na changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikiwafanya wasifike mbali zaidi
ya muziki wao kusikika hapa nchini na wengi wao kutamba kwa muda mfupi
na kupotea katika ulimwengu wa muziki huku wakiwa hawajanufaika na kitu
chochote kimaisha na kushauri kuwa wasibaki nyuma kiteknolojia hasa
wakati wa kupeleka kazi zao sokoni iwapo watataka kujikwamua.
“Licha
ya kuwepo na changamoto kubwa kama vile kutokuwepo sheria ya hakimiliki
inayopelekea wasanii kuibiwa kazi zao na kazi za muziki kutumiwa na
vyombo vya habari kama redio na televisheni bila kuwalipa wahusika
chochote. Tatizo lingine linalodumaza muziki wa Tanzania ni uoga wa
wanamuziki kubadilika na kuogopa teknolojia za kisasa kama hii
programu ya kupakua muziki kwenye simu kwa kupitia Mziiki” Alisema.
Amesema
sababu kubwa iliyopelekea kuamua kufanya biashara ya muziki kupitia
progamu hii ni kwamba nyimbo zake ziweze kuwafikia washabiki wake popote
na muda wowote kwa urahisi kupitia simu zao za mkononi na anakuwa na
uhakika wa kupata mapato tofauti na kama zinavyosambazwa na wasambazaji
wa mtaani.
“Duniani
kwa sasa hivi kuna ushindani mkali katika nyanja zote. Sisi kama
wanamuziki wa Tanzania tunapaswa kuhakikisha tunatoa muziki wa viwango
vya juu na kuhakikisha tunalenga zaidi katika masoko ndani na ya nje
kama wenzetu wanavyofanya kusambaza kazi zao kupitia kampuni zinazotumia
teknolojia ya kisasa na kumnufaisha msanii kama ilivyo program hii ya
Mziiki. Kuna umuhimu mkubwa wa kujiamini, kufanya vizuri ili tuweze
kutangaza Tanzania, kutangaza lugha ya Kiswahili na kupata mapato ya
kutosha kutokana na kazi ya muziki ambayo ikifanywa kitaalamu inalipa
kwa kiasi kikubwa” anasema Diamond Platinumz
Aliwaomba
wapenzi wa muziki nchini kuwaunga mkono wanamuziki wa hapa nchini kwa
kupakua nyimbo zao kwenye Mziiki kwa kuwa njia hii iko wazi na
inamuwezesha mwanamuziki kujua kirahisi jinsi kazi zake zinavyokubalika
sokoni na inamuwezesha kujua mapato yake tofauti na njia nyingine kama
uuzaji wa CD kwenye maduka na mitaani.
Programu
ya Mziiki ambayo ilizinduliwa na Vodacom kwa kushirikiana na Spice VAS
Africa imeanza kufanya kazi na wanamuziki wa hapa nchini na nje ya
nchi na katika kipindi cha muda mfupi tayari imesajili wanamuziki
wapatao 1,000 ambao kazi zao hususani zile mpya zitasambazwa kwa njia
ya kidigitali na malengo yake makubwa ni kuhakikisha wanamuziki
wanapeleka kazi zao sokoni kwa haraka na kunufaika na jasho lao hususan
pale ambapo wananchi wengi watatumia mtandao kwenye simu zao kupakua
nyimbo wazipendazo za wanamuziki ambao wamejiunga kwenye tovuti ya
kampuni hiyo ambayo inapatikana kwa kubofya tovuti ya www.mziiki.com.
0 comments:
Post a Comment