Na Magreth Kinabo, Dodoma
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba,
ambaye pia ni Mwanasiasa mkongwe, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru ameeleza
siri iliyomsukuma kutoa mapendekezo yake ya sura mpya juu ya lengo la
mageuzi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kujitegemea kuwa ni
unyonge wa watu wengi ili waweze kuondokana na umasikini.
Aidha Mzee Kingunge ambaye ni mjumbe
wa Bunge hilo kutoka kundi la 201 alisema alijifunza katika semina ya
Dk. Amos Wako ambaye alikuwa Mwansheria Mkuu wa Kenya kwamba ili kuweza
kuwa na usawa wa binadamu ni lazima kujali haki za makundi mbalimbali.
Aliyataja baadhi ya makundi hayo, kuwa ni wafugaji, wavuvi, wakulima vijana na mengineyo.
" Haki zote hizi zilikuwepo katika
Katiba ya mwaka 1977 na Katiba za nchi mbalimbali, lakini wanaofaidi
haki hizo katika nchi hizo ni wale wenye nacho," alisema Mzee Kingunge
Aliongeza kwamba watu wanaishi lakini hawana uhakika wa kuwa na chakula cha kesho.
" Mimi nimependekeza kwenye Kamati
yangu Namba Nane, mawazo yangu yamepelekwa katika Kamati mbalimbali na
wengine walelezea vizuri kuliko mimi," alisema.
Mzee Kingunge alisema hayo huku akitoa
mfano wa Hayati wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa
kilichomsukuma kugombania uhuru ni unyonge wa mwafrika, lakini yeye ni
unyonge wa watu wengi.
"Sisi ni waafrika lazima tujitambue
Sisi nani...sisi ni watu kama wengine, wenzetu wa Mashariki wameendelea
kwa sababu ya maarifa ya kisasa ya Sayansi na Teknolojia na sisi maarifa
tunayo na sasa hivi tunaweza kuyapata hata ambayo hatuna.
"Ninapendekeza jambo kuu moja kujenga
uchumi wa kisasa wa taifalinalojitegemea, maana yake ni tujikite katika
maarifa ya kisasa ya Sayansi na Teknolojia,tufanye mapinduzi bora ya
elimu, kilimo, ufugaji, uvuvi ili yawe ya kisasa," alisisitiza.
Alisema pili ni kuanzisha mchakato wa
mapinduzi ya viwanda,ambayo ni kujenga sekta muhimu za nishati,
mawasiliano na miundombinu kwa kuwa yote hayo yanatuelekeza kwenye
kujenga taifa linalojitegemea.
Mzee Kingunge alisema ni vema kujenga
nchi yenye maendeleo linganifu ya kiuchumi na kijamii katika taifa,
uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na kijamii, upangaji wa maendeleo ya
kiuchumi na kijamii na kujitegemea, rasilimali za nchi na matumizi yake
na utafiti wa maendeleo
"Katika kujenga dhamira ya kujenga
uchumi wa kisasa wa taifalinalojitegemea, mafanikio katika jambo
yatategemea mambo matatu, ambayo ni wananchi kufanya kazi kwa bidii, kwa
maarifa na nidhamu," alisema.
Alisema kufanya hivyo ni kuwaondoa
asilimia 65 ya wakulima wanao tumia jembe la mkono, kuhibiti ufugaji wa
kuhamahama na kuhakikisha wana malisho na maji kwa ajili ya mifugo yao
jirani na makazi yao.
Aliwataka wajumbe wa Bunge hilo, walisoma ili waweze kufanya maamuzi ya kihistoria.
Alifafanua kuwa umasikini hautaondoka
kwa miujiza, bali kwa misingi kama hiyo, kwa kuwa haki nyingine
zinategemea uchumi, huki akitoa mfano China waliweza na kuweka historia.
0 comments:
Post a Comment