Marais wa Urusi na Ukraine wamekuwa na mazungumzo ya
kwanza ya moja kwa moja kuhusu mgogoro wa eneo la mashariki mwa Ukraine,
lakini inaonekana hakuna welekeo wa mgogoro huo.
Kiongozi wa Ukraine Petro Poroshenko amesema
"mpango" utaandaliwa haraka iwezekanavyo kumaliza mapigano kati ya
majeshi ya Ukraine na waasi wanaotaka kujitenga.
Rais Vladimir Putin wa Urusi amesema
nchi yake itasaidia katika mazungumzo, lakini suala la usitishaji
mapigano ni la Ukaraine yenyewe.
Ukraine imekuwa ikiishutumu Urusi kwa kuwapatia silaha waasi, madai ambayo yanakanushwa na Urusi.
Kabla ya mkutano wao wa ana kwa ana katika mji
mkuu wa Belaruse, Minsk, viongozi hao wawili pia walishiriki katika
mazungumzo na afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton.
Mkutano huo unakuja baada ya askari kumi wa Urusi kukamatwa mashariki mwa Ukraine.
Mwanadiplomasia Ashton ameyaelezea mazungumzo
yaliyowashirikia viongozi mbalimbali wa Ulaya kuhusu mgogoro wa Ukraine
kuwa una mwelekeo"sahihi".
Umoja wa Ulaya pamoja na Marekani zimeiwekea Urusi vikwazo vya uchumi kwa kushindwa kuwadhibiti waasi.
Zaidi ya watu 2,000 wameuawa katika mapigano kati ya majeshi ya Ukraine na waasi katika majimbo ya Donetsk na Luhansk.
Majimbo hayo mawili yamejitangazia uhuru kutoka
Kiev kufuatia hatua ya Urusi ya kujinyakulia eneo la kusini la Crimea
kutoka Ukraine mwezi March 2014.
Mazungumzo kati ya Bwana Poroshenko na Bwana Putin yalidumu kwa takriban saa mbili bila kuruhusu vyombo vya habari.
HABARI NA BBC
0 comments:
Post a Comment