SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Wednesday, July 16, 2014

DAMAS LYASSA ATANGAZA RASMI VIPAUMBELE KATIKA UCHAGUZI WA URAIS TUCTA

Imetolewa leo tarehe 16 Julai 2014
Na Dismas Lyassa
Mgombea Urais wa TUCTA; Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi
Salaam
Wapendwa ndugu zangu wana habari…Asalam Aleikum…Tumsifu Yesu Kristo… Bwana Yesu Asifiwe…!

Shukrani
Ndugu wanahabari
Nawapenda kuwashukuru kwa ujio wenu. Nichukue fursa hii niwatambulishe walioko mbele yenu ili kufahamiana. Nianze kwa kujitambulisha mimi mwenyewe, naitwa Dismas Lyassa, ni mwandishi wa habari mwenzenu…nimekuwa katika hii kazi kwa miaka 20 sasa na nimewahi kufanyia kazi katika magazeti mbalimbali yakiwamo Alasiri, Financial Times, Leo ni Leo na tangu 2005 nimekuwa nikifanyia kazi katika gazeti la Mwananchi hadi sasa nikiwa mhariri anayeshughulikia masuala ya biashara na uchumi. Pia toka mwaka 2012 nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa COTWU tawi la Mwananchi Communications Limited, nafasi ambayo kisheria mtu anapaswa kudumu kwa miaka mitano, lakini akitaka anaweza kugombea.
Utambulisho
Ndugu wanahabari
Wengine niliombatana nao ni mke wangu Mchungaji Rightess Lyassa wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Kawe -Dar es Salaam, Mussa Mwakalinga Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Usafirishaji (COTWU) kanda ya Dar es Salaam, wakili wangu Jebra Kambole kutoka kampuni ya Uwakili ya Law Guards ya Jijini Dar es Salaam, na meneja kampeni Khamis Tembo.
Ndugu wanahabari
Lengo hasa la kuwaiteni mahali hapa ni kutoa taarifa kwenu kuwa ninagombea Urais wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania, uchaguzi ambao unatarajiwa kufanyika Agosti 4-5, Dodoma. 
Vipaumbele vyangu ni vyangu
Ndugu wanahabari
Nina malengo ya kuifufua na kuleta TUCTA yenye uhai na mabadiliko ya kweli kwa kufanya yafuatayo;
Ndugu wanahabari
1. Kupigania na kulinda haki za wafanyakazi;
Katika kipaumbele hili lengo hasa ni kuondoa matatizo sugu ya wafanyakazi yakiwamo-:
i.             Kulipwa ujira/mishahara duni isiyoendana na uhalisia wa maisha.
ii.           Ucheleweshaji wa upatikanaji wa ujira/mishahara
iii.          Ucheleweshaji fedha za kujikimu kwa waajiriwa wapya/ kiwango kidogo cha fedha za kujikimu
iv.          Uhaba au kutokuwepo kabisa makazi kwa wafanyakazi wapya
v.            Rushwa na kuajiri kwa misingi ya kujuana kwa mfano katika Halmashauri ya Siha, wilaya ambayo imegawanywa kutoka Hai, kuna pori kubwa la West Kilimanjaro mlimani kabisa, hakuna maendeleo…ni suala la kawaida kuona watu wakiongea kilugha ofisini kama lugha ya Taifa
vi.          Wakubwa yaani mabosi kujifanya Mungu kwa kuwaendesha wafanyakazi kwa kadri wanavyotaka wao, sivyo inavyosema sheria.
vii.         Uwepo wa mpangilio usio sawa wa ujira/mishahara.
viii.       Kutopewa posho au kupewa kidogo au kutopewa kwa wakati
ix.          Fedha za uhamisho na likizo; kwa mfano kuna walimu ambao wameanza kazi 2004 NIT Shule ya msingi Dar es Salaam wamelipwa fedha za likizo mara moja mwaka 2012, mfano halisi ni mwalimu Ruth Natumwa, huyo ni kati ya walimu hao. Matatizo ya walimu kimsingi ni janga la taifa, yapo Taifa zima, kwa mfano katika shule ya Sekondari Kizota, Dodoma kuna walimu wengi  wana madai yao dhidi ya Serikali, waliajiriwa mwaka jana Machi, wakaanza kupata mshahara mwenzi wa tisa…walilipwa mshahara wa mwezi wa tisa tu na kuendelea,  ile mingine wanaendelea kudai.
x.            Mazingira magumu ya kazi mijini na vijijini (tunapozungumzia mazingira magumu inahusisha kutokuwepo vitendea kazi au kuwa vichache, miundo mbinu duni nk).
xi.          Waajiri kutochangia mifuko ya jamii
xii.        Fedha za makato ya wafanyakazi kupitia mifuko ya jamii zimekuwa zikikopeshwa watu wengine wasio wanachama wakiwamo wanasiasa huku wafanyakazi wenyewe wakiendelea kuwa na maisha duni
xiii.       Kufanya kazi kama kibarua kwa miaka mingi jambo ambalo ni tofauti za sheria za kazi
xiv.       Huduma za kifedha kuwa mbali na maeneo ya kazi, hali inayosababisha wafanyakazi kutumia fedha nyingi kufuatilia mishahara kwa vile ni mbali na eneo wanalofanyia kazi.
xv.         Kutokuwa na mfumo unaoeleweka wa upandishaji vyeo na ujira/malipo kwa wafanyakazi/vibarua
xvi.       Waajiri hasa binafsi kufukuza wafanyakazi hovyo/no job security…kufanya kazi bila mikataba
xvii.      Kupambana na tatizo la kodi kubwa kwa mishahara (PAYE)
xviii.    Tatizo la mabosi kutoa upendeleo wa wazi kwa baadhi ya wafanyazi kwa sababu zisizo za kitaalamu; wakati mwingine ni kwa sababu ya ngono; kuwataka kimapenzi wafanyakazi ili waendelee kuwepo kazini au kupandishwa vyeo…tatizo hili linaonekana kuwa sugu, wanawake wengi maofisini hawako huru sana, wamekuwa wakitakwa kimapenzi mno na mabosi wao, wengi wanashindwa kujizuia, tunataka kuona kunakuwa na sheria kali dhidi ya mabosi wa aina hii kama ilivyo katika nchi nyingine.
Ndugu wanahabari
Tatizo la ajira kuporwa na wageni
 Ingawa sheria/sera za ajira zinaeleza wazi kwamba hairuhusiwi wageni kuingia nchini zaidi ya watano kwa kazi ziziso na ujuzi, baadhi ya makampuni yamekuwa yakiingiza wageni kwa kazi ambazo Watanzania wengi wanaweza kuzifanya.
Ndugu wanahabari
Nitahakikisha wazawa wanapewa fursa ya kufanya kazi nchini; hii ni pamoja na kuomba CV za wageni ili tuone kama ni kweli hakuna Watanzania wenye sifa za kufanya hiyo kazi hiyo.
        -: Kumekuwa na taarifa za uwepo wageni katika makampuni kadhaa yakiwamo mahoteli, migodi, viwanda vya sarufi nk ambao baadhi wanalipwa malipo makubwa tofauti na wazawa japo hawana elimu au ujuzi wa kuwazidi wazawa. Nitakuwa na kamati maalumu ya kufuatilia waajiriwa wote Tanzania hasa wageni ili kujua kama wanazo sifa za kufanya kazi au wanapora nafasi za Watanzania.
Ndugu wanahabari
Nitapigania kuhakikisha tabia ya waajiri kulazimisha waajiriwa lazima wawe na uzoefu mkubwa inapungua au kukoma kabisa
  Kigezo cha kupata ajira kiwe ni uwezo wa mtu wakati huo baada ya kufanyiwa usaili, siyo lazima awe na uzoefu  wa miaka mitatu au mitano kama ambavyo waajiri wengi wanalazimisha; tunahitaji kuona Serikali inasimamia hili. Kama hali ni hii, wahitimu wanawezaje kupata ajira? Ni suala ambalo nitakuwa mkali nalo mno kwa sababu lina athari kubwa kwa jamii ya Tanzania, limekuwa ni sababu ya rushwa ikiwamo ya ngono…walioko vyuoni wengi hawana uhakika wa ajira, kwa sababu ya tabia hii. Ni lazima tubadilike, watu waajiriwe kulingana na uwezo wao wa kazi, siyo uzoefu.
Ndugu wanahabari
Wanafunzi shule ya Msingi/Sekondari nk wapatiwe elimu ya kujiajiri.
Kwa nafasi nitakayokuwanayo nitaishawishi Serikali iingize elimu ya ufundi/utengenezaji bidhaa na ujasiriamali kama mojawapo ya masomo ya ziada kama njia ya kupambana na tatizo la ajira ambalo linaonekana kukua nchini. Kama ambavyo kumekuwa na masomo ya dini katika shule zenu, tuwe pia na masomo ya ujasiriamali. Nitaangalia namna ya kuzishawishi taasisi zingine za ndani na nje kuhakikisha hili linafanyika; lengo ni kuhakikisha hata mhitimu wa msingi au sekondari nk awe ana uwezo wa kufanya ujuzi anaotaka kama kujenga, kushona, kufuma, kufuga, kutengeneza batiki, vikoi, sabuni, mishumaa nk.
Ndugu wanahabari
Nitaanzisha idara mbili mpya na kuboresha zilizoko;
     i. Idara ya walemavu
Hii itahusika kuangalia hali ya maisha ya wafanyakazi walemavu nchini ikiwamo kuwasaidia kupata baiskeli na huduma zingine muhimu.Nitatumia uzoefu wangu kwa kushirikiana na rafiki zangu wa nje kuhakikisha hili linafanikiwa. Tutaangalia namna ya kushirikiana na mashirika mbalimbali yakiwamo Free Wheelchair Foundation
www.wheelchairfoundation.org.
Ndugu wanahabari
Kutakuwa ni mikakati mbalimbali kuhusu wafanyakazi walemavu na wale wanaopata ulemavu wakiwa kazini, kwa mfano Mwenyekiti wa Wasioona mkoani Tanga amekuwa ni mtu ambaye ameumia kazini, lakini aliishia kulipwa Sh150,000 na bandari ambako alikuwa anafanya kazi kama kibarua.  Kitendo kitakuwa na jukumu la kufuatilia kwa ukaribu hali za wafanyakazi walemavu, kuangalia kama wanavyotoka vyuoni wanapewa ajira au wanaishia kunyanyapaliwa? Utafiti unaonyesha kuna wanafunzi wengi wanaohitimu masomo wakiwa na ulemavu, hata hivyo hawaonekani kwenye maofisi wakifanya kazi. Wanakwenda wapi? Litakuwa ni jukumu la hicho kitengo.
Ndugu wanahabari,
    Idara ya pili ni
Idara ya fursa/Career Development Department na Mafunzo
 Nimetembea katika nchi tofauti Duniani ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Mauritius, India, Thailand, Sweden na Marekani…nimeona fursa kadhaa ambazo zimenishawishi kuanzisha idara maalum ya kusaidia wafanyakazi kufahamu fursa zinazoendelea Duniani na hapa nchini. Fursa hizo zitakuwa zinapatikana katika tovuti za TUCTA na ofisi za vyama vya wafanyakazi mikoani. Baadhi ya fursa ni namna gani mtu anaweza kusoma nje ya nchi bila kulipa ada kwa kozi za muda mrefu na mfupi, fursa ya mashirika ambayo yanatoa misaada kwenye sekta mbalimbali.
-Kwa mfano kuna mashirika kama www.nuffic.nl au vyuo ambavyo mtu anaweza kusoma bure bila kulipa chembe ya ada kama www.berea.edu  ya Marekani na fursa nyingine nyingi. Nimegundua Watanzania wengi hawanufaiki sana na fursa hizi. Ziko pia taasisi nyingine zinatoa.
Ndugu wanahabari
Idara hii itakuwa na majukumu ya kutoa elimu kwa wafanyakazi kuzifahamu sheria za kazi, hali kadhalika itakuwa inawasiliana na waajiri ili zaidi ya barua ya ajira au mkataba wanaompa mwajiriwa, ampe pia na  chapisho letu ambalo mwajiriwa anapaswa kupewa siku ya kuajiriwa kwake ili ajue kwa uhakika sheria za kazi zinasemaje; haki ya mwajiriwa kwa mwajiri au ipi na haki ya mwajiri kwa mwajiriwa ni ipi; tutashawishi hili liwe ni suala la lazima. Tutakuwa na vituo maalum vya msaada wa kisheria mikoani kote au kwenye kanda. Tutakuwa na vipindi kwenye televisheni angalau kila mwezi mara kuelezea masuala ya sheria za kazi. Tutaitumia tovuti ya TUCTA  kuwa ya kisasa zaidi.
Ndugu wanahabari
 Kulifufua gazeti la Mfanyakazi ndani ya siku 90 ili liwe sauti thabiti ya wafanyakazi
Haijalishi kama TUCTA itakuwa na fedha au la, nitahakikisha ndani ya siku 126  litakuwa mitaani likiandika habari mbalimbali hasa likitumika kama sauti ya wafanyakazi na yote ambayo yataonekana ni ya maana kwa ustawi wa taifa. Nina uzoefu zaidi ya miaka 20 katika sekya ya habari kama Mhariri, na hata sasa ni Mhariri wa Biashara gazeti la Mwananchi, nitahakikisha tunatafuta fedha ndani na nje ya TUCTA ikiwamo kuwatumia wafanyabiashara kwa kubadilishana msaada kwa matangazo kwa muda, ili hatimaye liweze kuwa mitaani. Ni aibu kubwa kuona nchi ina wafanyakazi wengi, lakini gazeti kama hili la wafanyakazi haliko mitaani.
Ndugu wanahabari
 Kuimarisha uhusiano wa vyama vya ndani na vyama vya nje
Nitahakikisha nafanya mawasiliano na mashirika mengine yakiwamo International Trade Union Confederation, Secretary General Sharan  Barrow na mashirika mengine ili kuona namna gani vyama vya wafanyakazi vya nchini vinanufaika na ushirikiano huo kwa kubadilishana uzoefu na kadhalika mara kwa mara kadri inavyowezekana.
Ndugu wanahabari
Nitatutumia uzoefu wangu wa shughuli za kuwasiliana na vyuo vya nje na uzoefu wangu wa kufanya kazi katika mashirika mbalimbali ya nje kama muwakilishi wao hapa nchini, na  kutembea nchi mbalimbali, kuviunganisha vyama vya ndani vya wafanyakazi, kuwa na ukaribu zaidi na vile vya nje, na pia kujenga uwezekano wa viongozi nchini kwenda nje kupitia ushirikiano huo.
Ndugu wanahabari
Hili linawezekana kwa njia mbili, kwanza kama washirika wetu kwa vile tutakuwa tuna mawasiliano ya karibu na aina ya chama ambacho mtu anatoka, kwa mfano kama COTWU, TTU, TALGWU, TUICO, TAMICO, TEWUTA, DOWUTA, TPAWU, RAAWU, TUGHE, CHODAWU, TRAWU. Nahitaji kuona ofisi za vyama vya wafanyakazi nchini zinakuwa za kuvutia kwa kuzipatia vitendea kazi, kuna mashirika nayafahamu, tunaweza kuyatumia kuwasiliana nayo yakatusaidia kama vile Computer Aid International la Uingereza ambalo hutoa misaada ya computer za aina mbalimbali kwa nchi maskini kama Tanzania (www.computeraid.org). Nje ya hiyo nitakuwa na vikao na viongozi wa chama kimoja badala ya kingine kuangalia namna gani tunaweza kuboresha shughuli za utendaji za ndani na nje hasa kuimarisha rasilimali watu na vifaa. Lengo kubwa la kuomba niwe Rais wa TUCTA ni kuangalia namna gani tunaweza kushirikiana na wafanyakazi na viongozi wa vyama katika kuimarisha wafanyakazi, kwani malalamiko ni mengi. Tutaendeleza mali za TUCTA zikiwamo Chuo cha Wafanyakazi Mbeya na maeneo mengine.
                                                                                          
Ndugu wanahabari
NAMNA GANI HAYA YATAWEZEKANA?
Mkakati wa kuondoa kero zote zilizoelezwa juu utafanikiwa kwa majadiliano yenye ukomo (deadline) na Serikali/waajiri, au kufanya chochote ambacho katiba inaruhusu. Sheria ziko wazi, nitahamasisha zifuatwe na zifahamike. Shida kubwa ninayoiona kwa sasa, wafanyakazi wengi hawajui haki zao pia msaada wa vyama katika kuwasaidia wafanyakazi ni mdogo.
Ndugu wanahabari
Hata hivyo mkakati hasa ni kuangalia TUCTA kwa kushirikiana na vyama shiriki vinafanya nini kuondoa changamoto ambazo sisi wenyewe tunaweza kuziondoa. Uongozi siyo kulalamika, bali kuthubutu kuchukua hatua zinazoweza kuondoa shida zilizoko. Tayari nimeanza kuwasiliana na vyama mbalimbali vya wafanyakazi katika mataifa ya nje ili kuangalia namna gani tunashirikiana kwa maana ya kubadilishana uzoefu nk.
Ndugu wanahabari
Ofisi nyingi za vyama vya wafanyakazi zimechakaa, naangalia uwezekano wa kushirikiana nao katika hili kwa njia ya kutafuta wafadhili wa nje au kubuni miradi itakayosaidia kuondoa hali hiyo; nataka pia maisha ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi kwa ujumla yabadilike kwa kutumia jitihada hizo nilizozieleza juu, nafahamu vizuri namna ya kusaka wafadhili, kwani ni shughuli ambayo nimekuwa nikifanya kwa muda mrefu kupitia taasisi yangu ya Global Source Watch, niliyoianzisha toka mwaka 2001 ambayo imekuwa ikifanya kazi ya kuwaunganisha watu na vyuo zaidi ya 78 vya nje kama Marekani, Canada, Greece, India, Malaysia nk.
Ndugu wanahabari
Nafahamu kuna vyama vina miradi ya maendeleo, vinawasaidiaje wanachama wao? Nahitaji niwe Rais ili nishirikiane na vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi kwa ujumla kuleta tija kwa Watanzania. Tusiwe watu wa kunyoosheana vidole…kila mtu awe chanzo cha mabadiliko anayotaka kuyaona Tanzania! Naamini kila mtu akifanya kazi zake vizuri…Tanzania itakuwa na maendeleo kwa kasi. Wafanyakazi wanahitaji mambo mengi zaidi ya kuhamasishwa migomo, lakini kama tutaamua kugoma, tunapaswa kugoma kwa kumaanisha, hatupaswi kuogopa kutekeleza yaliyo haki yetu.
Ndugu wanahabari
Kwa nafasi nitakayokuwa nayo nitaanzisha semina, makongamano, mijadara itakayokuwa ya wazi na kutoa elimu ya kutosha juu ya haki za wafanyakazi na wajibu wa waajiri kwa wafanyakazi. Hii itasaidia kupunguza migogoro na wafanyakazi watatambua haki zao.
Ndugu wanahabari
Tunatakiwa kuwa sauti ya wafanyakazi hapa Tanzania, TUCTA imelala, tunataka kuikimbiza mchakamchaka,, kuna mambo mengi yanatokea dhidi ya wafanyakazi hapa nchini lakini TUCTA haitoi hata matamko au kutetea wafanyakazi,
Ndugu wanahabari
Natambua changamoto za wafanyakazi, tunataka kuwa na
TUCTA Mpya
Nguvu Mpya
Uongozi Mpya
Sauti Mpya
Umoja Mpya
Maendeleo Mapya
Kwa pamoja tunaweza.
Mungu awabariki!
Dismas Lyassa
Mgombea nafasi ya Urais-TUCTA
simu 0754 49 89 72
--------------------------------------------------------------------------------------------------
HOTUBA FUPI KUTOKA KWA JEBRA KAMBOLE, Wakili wa Dismas Lyassa anayefanya Kampuni ya Uwakili ya Law Guards Advocates ya Jijini Dar-es-salaam kwa Waandishi wa Habari.
Ndugu waandishi wa Habari wa vyombo vyote vya Habari,
Ndugu watanzania wengine mliopo hapa,
Shukrani
Tunashukuru sana kwa kuitikia wito wetu, Mungu awabariki sana, Tunamshukuru mwenyezi mungu kwa kutupa afya na sia njema,
Ndugu waandishi wa Habari
Kuna mambo muhimu manne tunataka kuwaeleza watanzania wote, hasa wafanyakazi na viongozi wa vyama vyote vya wafanyakazi
Moja, Ndugu anatimu iliyojipanga makini kuhakikisha TUCTA inarejea na kuwa na Nguvu zaidi, Ni kijana makini mwenye malengo ya kuleta maendeleo ya haraka na kufufua uhai wa TUCTA.
Ndugu Waandishi wa Habari
Napenda kuchukua fursa hii kutoa onyo kwa wanaopanga kutoa rushwa kwenye huu uchaguzi wa TUCTA kuwa tuko makini na hili tumejipanga, tutachukua hatua za haraka za kisheria dhidi yao, ikiwa ni pamoja na kuwaripoti kwenye vyombo husika, Rushwa si kipaumbele utapinga kwa nguvu zetu zote.
Ndugu Waandishi wa Habari
Ndugu Dismas Lyasa pia atasaidia kuanzisha kituo au kushirikiana na mashirika mengine kutoa masaada wa kisheria kwa wafanyakazi wanaofukuzwa makazini kinyume cha sheria. Wafanyakazi wengi wakikumbwa na matatizo wafanyakazi wenzao wanawatenga, vyama vyao vinawatenga, Dismas atahakikisha kuwa TUCTA ni kimbilio lao.
Ndugu Waandishi wa Habari
Ndugu Dismas Lyasa atasaidia kutoa mafunzo ya kisheria kwa wafanyakazi ili waweze kutambua haki zao za msingi, kwa kuendesha semina, makongamano na mijadara itakayotoa elimu na kuibua mijadara kwa wafanyakazi.
CHAGUA DISMAS LYASA KWA TUCTA MPYA, Mabadiliko ni sasa,,,Asanteni

0 comments:

Post a Comment