Mzee Abdi Nkhambi Lanjui (75) akiwa wodi namba nne katika hospitali ya mkoa mjini Singida. Mzee Lanjui mzaliwa wa kijiji cha Mhintiri tarafa ya Ihanja, aliyekuwa dereva wa kampuni ya mamlaka ya Pamba Mwanza, alipata ajali katikati ya mwaka 1968 na kulazwa katika hospitali ya Sekoture Mwanza na baadaye mwishoni mwa mwaka 1970,alihamishiwa hospitali ya mkoa wa Singida, ambako anaishi hadi sasa. Ajali hiyo ilisababisha kukatika mawasiliano kati ya kuanzia kiunoni na kushuka chini ambako kumepooza na sasa kuna vidonda na sehemu ya mwili juu ya kiuno, bado inafanya kazi.(Picha na Nathaniel Limu).
Na.Nathaniel Limu.
AFISA Maendeleo ya jamii sekretariati ya mkoa wa Singida, Zuhura Kyaria amesema mzee Abdi Nkambi lanjuu (75) aliyeishi wodini kwa zaidi ya miaka 45, ataendelea kubaki kwenye makazi yake hayo hayo ya wodini kwa madai kwamba hana ndugu au mtu ye yote wa kuweza kumhudumia muda wote.
Akifafanua Kyaria amesema kuwa baada ya juhudi kubwa kufanyika za kuwatafuta ndugu zake kijijini kwao Mhintiri tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi kugonga mwamba,walihamishia mawazo yao kumpeleka katika kambi ya watu wenye ukoma ya Sukamahela wilayani Manyoni.
“Baada ya kugonga mwamba huko Mhintiri, basi tukaona pengeni mahali patakapomfaaa mzee Abdi kuishi,ni kwenye kambi ya wakoma ya Sukamahela.Tulipomuuzia mzee Abdi wazo hilo, alikataa kuhamia huko”,amesema.
Kyaria amesema hata wao walipokaa chini na kutafakari juu ya kumpeleka Sukamahela,tulioona kwamba hapatamfaa kwa sasa anahitaji mtu wa kumhudumia wakati wote,…yaani mchana na usiku kwa vile hawezi kukaa kutokana na kupooza sehemu yake ya kuanzia kiunoni hadi chini kwenye miguu.
“Kwa haraka haraka tu,ukiangalia,pale kambi ya Sukamahela ina uhaba mkubwa wa wafanyakazi, pia kuna uhaba wa maji na wakazi wenyewe wa sehemu hiyo,ni watu ambao hawana vidole vya kujihudumia wenyewe, watawezaje kuhudumia mtu mwingine ambaye sio ndugu yao”,amesema na kuongeza;
“Juzi watu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii waliposoma habari za mzee Abdi kwenye gazeti la MWANANCHI, walinipigia simu na nikawaeleza ugumu wa kumhamishia mzee Abdi katika kambi ya watu wa ukoma na wakanielewa”.
Afisa huyo kwa ujumla mzee Abdi ataendelea kuwepo katika hospitali ya mkoa mjini Singida,hadi hapo maisha yake ya duniani yatakapokoma.
Kwa sasa mzee Abdi anachokiomba kwa jamii,serikali,asasi na watu wenye uwezo,ni kumsaidia apate uhakika wa kupata huduma ya chakula kwa mujibu wa mahitaji ya binadamu ye yote,ili aweze kuondokana na adha ya omba omba ambayo inamwezesha kula mlo moja kwa siku.