Jamaa hana hata wasisi juu ya mtoto wake yee anasema ni mipango ya mungu tu
Mtoto jinsi ya kiume aliyefahamika kwa jina la Suleiman Kolineli(miezi kumi) mkazi wa kijiji cha Igundu Kata ya Sangambi Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya aliyezaliwa na ulemavu wa mdomo(mdomo sungura)amefikishwa Hospitali ya Rufaa Mbeya ili kupatiwa matibabu.
Mtoto huyo ambaye alifichwa na wazazi wake baada ya kuzaliwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya na kutakiwa kurudi Hospitali hiyo baada ya miezi sita ili afanyiwe upasuaji kurekebisha sura yake lakini wazazi wake walishindwa kumpeleka Hospitali wakidai huo ni mpango wa Mungu.
Baba mzazi wa mtoto huyo Kolineli Mushi(34) amesema hakuwa tayari kumpeleka Hospitali kwa kuwa ulemavu huo umetokana na Mungu na kwamba akitibiwa nyumbani kwao watapata matatizo au kutokea kitu ingawa hakuwa tayari kubainisha matatizo hayo.
Kwa upande wake mama mzazi wa mtoto Yohana Kolineli(37)amesema licha ya kutakiwa kumpeleka mtoto Hospitali ya Wilaya ya Chunya alikosa nguvu kutokana na mume wake kukataa kata kata kushughulikia suala hilo kwa kisingizio cha kuwa ni mpango wa Mungu.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Chunya Frank Ngalla amekiri kuzaliwa na tatizo kwa mtoto huyo na kawaida watoto wadogo huanza kufanyiwa upasuaji miezi sia baada ya kuzaliwa na mtoto awe na uzito usiopungua kilo 5 hivyo walimtaka mzazi kurudi na mtoto kwa kipindi cha muda huo lakini hawakutokea Hospitali.
Mtoto huyo ambaye hula na kupumua kwa shida hivi sasa ana uzito wa kilo8.6 anahitaji msaada wa upasuaji haraka ili kumfanya ale vizuri na kupumua vizuri kwani mama mzazi hupata shida wakati wa kulsha na chakula kuwa hatarini kuingia kati koo la hewa kutokana na uwazi kati ya pua na mdomo.
Afisa Ustawi wa jamii Hospitali ya Rufaa Mbeya Anna Geleta amesema matibabu ya ugonjwa huo ni bure na wakati mwingine hufanywa na Madaktari bingwa wa Hospitali ya Rufaa Mbeya au Hospitali ya CCBRT ya Dar es Salaam na kubainisha kuwa maandalizi yamefanyika ili mtoto huyo asafirishwe kwenda kutibiwa CCBRT.
Mtoto huyo amegunduliwa na waandishi wa Habari wa Mbeya yetu waliokuwa wametembelea Kijiji cha Igundu ambapo Mwenyekiti wa Kijiji hicho Emmanuel Mbughi aliridhia mtoto kupatiwa matibabu na kwamba mtoto mwenye ulemavu kama huo hayupo na hakupata taarifa za ulemavu huo.
Katibu wa Hospitali ya Rufaa Mbeya Aisha Mtanda amesema taratibu za kumsafirisha mtoto na mama yake zimekamilika na kutoa wito kwa wazazi na walezi kutowafungia ndani watoto wenye ulemavu wowote,aidha amewataka pia wanawake wanaosumbumbuliwa na ugonjwa wa Fistula wajitokeze katika Hospitali Rufaa ili kutibiwa bure.
Mtanda amesema Madaktari bingwa nchini wataanza kuwahudumia wagonjwa wa Fistula kutoka mikoa ya nyanda za juu kusini kuanzia Mei 12 hadi Mei 23 mwaka huu bila gharama zozote hivyo wagonjwa wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwani Fistula inatibika.
Na Mbeya yetu
|