Timu
ya Taifa ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania imetwaa ubingwa wa Dunia wa
Watoto wa Mitaani baada ya jana (Aprili 6 mwaka huu) kuilaza Burundi
mabao 3-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa jijini Rio de Janeiro,
Brazil.
Mshambuliaji
Frank William alifunga mabao matatu katika mechi hiyo iliyochezwa
uwanja mkongwe na maarufu wa klabu ya Fluminense huku mgeni rasmi akiwa
Waziri wa Fedha wa Uingereza, George Osborne.
Tanzania
ilipata tiketi ya kucheza fainali baada ya kuitandika Marekani mabao
6-1 ambapo hadi mapumziko ilikuwa mbele kwa mabao 4-0.
Burundi ilipata tiketi ya kucheza fainali baada ya kuifunga Pakistan mabao 4-3 katika mechi ya nusu fainali ya pili.
Timu
ya Tanzania inarejea nchini Alhamisi (Aprili 10 mwaka huu) ambapo
itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 10
jioni kwa ndege ya Emirates.