Katibu
Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Bi. Theresia Mmbado akifunga mafunzo ya
siku 3 ya matumizi ya Fomu za OMR kwa walimu wakuu 254 wa shule za
Msingi za mkoa wa Dar es salaam yaliyofanyika katika shule ya Sekondari
Shaaban Robert.
Afisa
Elimu wa mkoa wa Dar es salaam Bw. Raymond Mapunda akitoa ufafanuzi kwa
walimu wakuu wa shule za Msingi za mkoa wa Dar es Salaam kuhusu namna
mkoa ulivyojipanga kutatua changamoto za elimu.
Baadhi
ya Walimu wakuu wa shule za Msingi jijini Dar es salaam wakifuatilia
michango mbalimbali iliyokuwa ikiwasilishwa kuhusu maboresho ya matumizi
ya mfumo wa OMR.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Matumizi
ya mfumo mpya wa kufanya mitihani kwa kutumia karatasi maalum za
OMR (Optical Mark Reader) na usahihishaji wa mitihani hiyo kwa njia ya
kompyuta umeonyesha mafanikio jjini Dar es salaam mara baada ya vitendo
vya udanganyifu na wizi wa mitihani ya shule ya msingi kudhibitiwa.
Katibu
Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Bi. Theresia Mmbado ametoa kauli hiyo
leo jijini Dar es salaam wakati akifunga mafunzo ya siku 3 ya matumizi
ya Fomu za OMR kwa walimu wakuu 254 wa shule za Msingi za mkoa wa Dar
es salaam.
Amesema
matumizi ya karatasi maalum za OMR yamefanikiwa kudhibiti vitendo vya
udanganifu na kurahisisha utoaji wa matokeo na kuipunguzia serikali
gharama ya kusahihisha mitihani hiyo ambayo hapo awali ilikua ikichukua
muda mrefu na kuchelewesha matokeo ya wanafunzi.
“
Nikiwa mwenyekiti wa usimamizi wa mitihani wa mkoa wa Dar es salaam kwa
mwaka 2013 nakiri kuwa mkoa wetu umepata fomu mafanikio makubwa katika
usimamizi wa mitihani na kupunguza udanganyifu kwa sababu ya hizi”
amesema.
Amesema
kuwa zipo changamoto ambazo mkoa unaendelea kuzifanyia kazi ili
kurahisisha matumizi ya mfumo huo kwa walimu na wanafunzi kuwa ni pamoja
na uchakavu wa meza za kufanyia mitihani ambazo huchangia karatasi za
OMR kujikunja na wakati mwingine kuchakaa na kupoteza sifa ya
kusahihishwa na kompyuta.
Pia
ameeleza kuwa ipo changamoto ya baadhi ya shule binafsi ambazo walimu
wakuu wake wamekwishapatiwa mafunzo hayo lakini wamekuwa wakihama
kutoka eneo moja hadi jingine hivyo kuathiri mafunzo kwa wanafunzi na
waalimu kuhusu namna ya kuweka vivuli kwenye karatasi hizo.
“
Natoa rai kwa baadhi ya wamiliki na walimu wakuu hasa wa shule binafsi
wasiotoa ushirikiano na kushindwa kuleta walimu wao katika mafunzo kama
haya tutaanza kuwafuatilia, ikibidi watumie gharama zao wenyewe
kuhakikisha walimu wao wanapata mafunzo haya muhimu kwa mustakabali wa
taifa letu na maisha wanafunzi wetu” amesisitiza.
Amewataka
wakuu hao waliopata mafunzo hayo kuwa mabalozi kwa wengine ambao
hawakupata mafunzo hayo kwa kuonyesha utofauti ili gharama iliyotumika
wakati wa mafunzo hayo iweze kuzaa matunda na kuleta faida kwa wananchi.
Amesema
Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) limekwishatoa kiasi cha shilingi
milioni 138 kwa ajili ya mafunzo ya walimu wa kuendelea kusimamia zoezi
la matumizi ya fomu za OMR katika uendeshaji wa mitihani ya kumaliza
elimu ya msingi na kuongeza kuwa takribani walimu 7,105 wameshapatiwa
mafunzo kwa ngazi ya kata.
Kwa
upande wake Afisa Elimu wa mkoa wa Dar es salaam Bw. Raymond Mapunda
ameeleza kuwa mkoa wa Dar es salaam licha ya kukabiliwa na changamoto
mbalimbali umekuwa ukifanya vizuri katika matokeo ya shule za msingi
kitaifa.
“Mkoa
wa Dar es salaam ni miongoni mwa mikoa inayopokea wanafunzi wengi kila
mwaka mathalani mwaka 2013 tumesajili wanafunzi 63,000 na mwaka huu 2014
tunatarajia kupokea wanafunzi 68,000 kiwango ambacho kinazidi kupanda
kilinganishwa na miundombinu iliyopo”
Kuhusu
matumizi ya fomu za OMR, Bw. Mapunda ameeleza kuwa ameeleza kuwa
zimepunguza makosa ya kibinadamu na gharama za usahihishaji na kuongeza
kuwa baadhi ya changamoto za baadhi ya karatasi kujikunja, kuchafuka na
kutoboka na pia baadhi ya wanafunzi kushindwa kuweka vivuli kwenye
vyumba husika vya majibu waliyochagua zinaendelea kufanyiwa kazi katika
maeneo husika.
Kuhusu
umuhimu wa mafunzo hayo amesema kuwa yamewajengea uelewa walimu hao juu
ya namna ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza na pia
kubadilishana uzoefu ikiwa ni sehemu ya kutekeleza Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN).
Aidha
katika hatua nyingine Bw. Mapunda amesema mkoa wa Dar es salaam unaandaa
maonyesho maalum ya wiki ya Taaluma ambayo itazihusisha shule za
Binafsi na zile za sekondari ambapo washindi katika wiki hiyo watapewa
zawadi mbalimbali.
Naye
mwenyekiti wa waliu wa shule za Msingi mkoa wa Dar es salaam Mwalimu
Rehema Ramole akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake amesema kuwa
tayari wamejipanga kuhakikisha kuwa wanaondoa makosa yote yatokanayo na
mfumo wa matumizi ya karatasi za OMR katika mkoa wa Dar es salaam.
0 comments:
Post a Comment