Rais Jakaya Kikwete
Frank Mvungi-Maelezo
Wabunge wanaowakilisha Tanzania katika
Bunge la Afrika Mashariki wamempongeza Rais Jakaya Kikwete kufuatia
hotuba yake aliyoitoa Bungeni Dodoma tarehe 07/11/2013 kuhusu
Mustakabali wa Jumuiya Hiyo.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa wabunge hao Mh. Adam Kimbisa wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Mh. Kimbisa amesema wabunge hao
wanampongeza Mh. Rais kwa kuchukua fursa ya kuongea na Watanzania
kupitia Bunge na kueleza masuala kadhaa baina ya Nchi wanachama na hali
ya hivi sasa ndani ya Jumuiya.
Akifafanua zaidi Mh. Kimbisa
amesemaMh. Rais amefanya uchambuzi wa kina kuhusu matatizo yaliyoikumba
jumuiya ya Afrika Mashariki kufuatia mikutano mitatu iliyofanywa na nchi
tatu za Kenya,Uganda na Rwanda ikiwatenga Tanzania na Burundi.
Alieleza zaidi kuwa wabunge wa bunge
hilo wanaungana na Watanzania wengi kuhusu kuwepo kwa shirikisho la
Afrika Mashariki lakini wanataka hatua hiyo isifanywe haraka bali kwa
umakini mkubwa,sera ambayo pia Serikali ya Tanzania imeipa kipaumbele.
Pia alisema jambo la msingi ambalo
mkataba wa uanzishwaji wa jumuiya umesema ni kuwa Jumuiya lazima iwe ni
ya wananchi kwa manufaa ya wananchi na isiwe ya viongozi ambapo wananchi
watashirikishwa katika kila hatua na kila ngazi ili waweze kushiriki
kikamilifu kwa ajili ya maslahi yao.
Katika hatua nyingine wabunge hao
waliipongeza Serikali kwa hatua iliyochukua kwa kuwarejesha makwao
wahamiaji haramu kutoka Burundi,Rwanda,Uganda,DRC nchi nyingine ambao
walitishia na kuharibu hali ya usalama na mazingira katika maeneo ya
Mikoa ya Kagera,Geita na Kigoma.
Aidha wabunge hao wameiomba Serikali
iendelee kusimamia suala hilo kwani baadhi ya wahamiaji haramu wameanza
kurejea katika maeneo husika na wananchi wameanza kutoa malalamiko dhidi
ya wahamiaji haramu.
CHANZO: NA MJENGWA BLOG
0 comments:
Post a Comment