Serikali
inaendelea kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ili kuchangia upatikanaji
wa fedha za kusaidia kuimarisha na kuendeleza miradi ya maendeleo
nchini.
Wakala
wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) imekuwa miongoni mwa taasisi za
Serikali ambayo imeanza kukusanya ada zote zitokanazo na huduma inazotoa
kwa njia ya kielekroniki kwa wadau wake kufanya malipo kwa njia ya simu
au benki kabla ya kupata huduma wanayohitaji.
Hayo
yamebainishwa leo Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria,
Dkt. Harisson Mwakyembe alipokuwa akiwasilisha mpango wa makadirio ya
bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
“Tayari
wilaya 114 kati ya 139 zinakusanya maduhuli kwa njia ya kielekroniki na
kwamba ifikapo Juni, 2016 wilaya zote Tanzania Bara zitakuwa zinatumia
njia ya kielekroniki kukusanya maduhuli,” alisema Dkt. Mwakyembe.
Katika
kuongeza mapato, Dkt. Mwakyembe ameongeza kuwa upo mkakati wa kuongeza
kiwango cha usajili wa vizazi na vifo nchini, ambapo RITA imeanzisha
kampeni ya usajili inayoambatana na uboreshaji wa mfumo wa usajili kwa
kuweka mfumo wa kompyuta kila wilaya ambapo kampeni hizo zilifanyika.
Wilaya
ambazo kampeni hizo zimefanyika ni Arusha na Arumeru ambapo jumla ya
watu 49,548 wamesajiliwa na kupewa vyeti vyao vya kuzaliwa.
Zoezi
hilo la usajili linaendelea katika wilaya ya Kahama na baadaye
litaendelea katika wilaya 16 nchini ambazo ni Bariadi, Chato, Dodoma,
Igunga, Kilombero, Kilosa, Lushoto, Maswa, Mbinga, Misungwi, Mtwara,
Muleba, Nzega, Shinyanga, Sumbawanga na Tunduru.
Waziri
Mwakyembe alibainisha kuwa Wizara hiyo kupitia RITA imekusudia kusajili
zaidi ya watu 500,000 katika maeneo hayo na kupatiwa vyeti vya
kuzaliwa.
Kwa
mujibu wa utafiti wa afya uliofanyika 2010, asilimia 16 ya watoto wenye
umri wa miaka mitano ndio wenye usajili na vyeti vya kuzaliwa Tanzania
Bara ikilinganishwa na Tanzania Zanzibar ambapo usajili ulikuwa ni
asilimia 79.
Ili
kukabiliana na hali hiyo, RITA kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) wamebaini mradi wa kusajili watoto
chini ya umri wa miaka mitano uliofanyiwa majaribio wilaya ya Temeke
mwaka 2012 na kuzinduliwa rasmi mwaka 2014 mkoani Mbeya.
Kampeni
hiyo imeonesha mafanikio na tija kwa taifa ambapo usajili umeongezeka
na kufikia asilimia 58 ambapo awali mkoa wa Mbeya usajili ulikuwa
asilimia 8.7.
Kampeni
hiyo ni endelevu kwa nchi nzima ambapo mikoa itakayoanza kufanya
usajili ni Mwanza, Mara, Shinyanga, Simiyu, Geita, Iringa, Njombe,
Tabora, Kagera na Dodoma.
Na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Dodoma
0 comments:
Post a Comment