SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Sunday, November 24, 2013

Taarifa rasmi kwa umma kutoka CHADEMA, Novemba 2013


Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), imemteua Mhe. Tundu Lissu kuwa Mwanasheria Mkuu wa chama hicho. Kamati hiyo ilikaa kikao chake Novemba 20 mpaka 21 katika Hoteli ya Blue Pearl Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam pia imemteua Wakili Peter Kibatala kuwa Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa chama hicho. Ifuatayo ni taarifa iliyosomwa na Mhe. Tundu Lissu kuhusu maamuzi na mipango ya chama.
*******
UTANGULIZI
Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliyokutana Ubungo Plaza, Dar es Salaam kuanzia asubuhi ya siku ya Jumatano ya tarehe 20 Novemba, 2013 hadi alfajiri ya leo Ijumaa tarehe 22 Novemba, 2013 imetafakari na kujadili kwa kina taarifa mbali mbali juu ya hali ya kisiasa ndani na nje ya Chama chetu ambayo kwa muda mrefu imegubikwa na tuhuma kubwa na nzito dhidi ya Chama chetu na viongozi wake wakuu, yaani Mwenyekiti wa Taifa, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (MB), na Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Peter Slaa.
Tuhuma hizi zilikuwa na malengo na athari ya kuwapaka matope na kuwachafua viongozi wakuu wa Chama na Chama chenyewe, kutengeneza mtandao wa siri ndani na nje ya Chama ambao hatimaye ungefanikisha sio tu lengo la kufanya mapinduzi nje ya utaratibu wa kikatiba wa Chama, bali pia ungekipasua Chama vipande vipande na hivyo kuua matumaini ya Watanzania juu ya uwezekano wa kufanya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi na kijamii katika nchi yetu kwa kukiondoa madarakani Chama cha Mapinduzi (CCM).
Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Uchunguzi wa Kamati Kuu umebaini kuwepo kwa mkakati mkubwa wa kutimiza malengo hayo ambao umeandikwa katika  waraka unaoitwa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013.’ Mkakati huu uliandaliwa na kikundi kinachojiita ‘Mtandao wa Ushindi’ ambacho vinara wake wakuu ni wanne, yaani Naibu Katibu Mkuu na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe ambaye kwenye waraka huo anajulikana pia kama ‘MM’ au ‘Mhusika Mkuu’; mjumbe wa Kamati Kuu na mwanazuoni kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitilla Mkumbo ambaye kwenye waraka anajulikana pia kama M1; Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha ambaye kwa sasa amesimamishwa uongozi, Bwana Samson Mwigamba na ambaye kwenye waraka anaitwa M3; na mtu mwingine ambaye hadi sasa jina lake halijajulikana lakini kwenye waraka anajulikana kama M2 na anatajwa kuwa yuko ‘ukingoni kupigwa nje’ katika mageuzi ya kiutendaji yanayoendelea katika Sekretariat ya Chama hapa Makao Makuu.
Kwa mujibu wa waraka wenyewe, “Mkakati huu umeandaliwa kwa pamoja na M2 na M3 na kupitiwa na kurekebishwa na M1 ili upelekwe kwa MM kwa maoni ya mwisho na kuanza utekelezaji.” Mbele ya Kamati Kuu, Dk. Mkumbo alikiri kwamba MM au Mhusika Mkuu ni Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe; M1 ni yeye mwenyewe Dk. Mkumbo na M3 ni Bwana Mwigamba. Dk. Mkumbo alikataa kata kata kumfahamu M2. Aidha, Dk. Mkumbo alikiri mbele ya Kamati Kuu kwamba yote yaliyoandikwa katika ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’ yametoka kwenye ‘Mtandao wa Ushindi’ na hayajabadilishwa.
Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Mkakati wa Mabadiliko 2013 ni mpango wa kuipasua pasua CHADEMA na kuiangamiza kabisa kwenye uso wa siasa za Tanzania. Huu sio mkakati wa kufanya mabadiliko ya kiuongozi ndani ya Chama kwa njia za kidemokrasia na za kikatiba. Ni mpango wa kukiteka nyara Chama na kukiua. Ndio maana watunzi wa waraka huu wamesema kwenye waraka wao: “Tunahitaji kutekeleza mkakati huu kwa siri kubwa ili mkuu aliyepo aendelee kubweteka na ndio maana hata lugha iliyotumika ndani hapa ni ya pekee.” Kamati Kuu inaamini mkakati wenye malengo halali ya kufanya mabadiliko ndani ya Chama kwa njia halali za kikatiba usingependekeza kwamba: “Vikao vyetu na yeye (MM aka Mhusika Mkuu aka Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe) vitafanyika mara chache sana na mahali pa faragha kupita kiasi ikiwezekana hata nchi jirani.” Aidha, Kamati Kuu inaamini kwamba kama mkakati huu ungekuwa na malengo mazuri ya kukijenga Chama na sio kukiteka nyara na kukiua, wanamtandao hawa wasingependekeza utaratibu ufuatao wa utekelezaji wa mpango: “M1 (Dk. Mkumbo) ndiye atakayekuwa anawasiliana na tunayemtaka ambaye ataitwa MM (Mhusika Mkuu). Tumepanga kwamba kusiwe na mawasiliano mengi kati ya kamati na mhusika mkuu kuepuka tracking ya wapinzani wetu. M1 ni mtu wa karibu na MM kwa hiyo mawasiliano yao hayataweza kutiliwa shaka na mtu yeyote hata wangewasiliana mara nyingi kiasi gani. Hata hivyo, linapokuja suala la mkakati huu tunasihi mawasiliano yawe kwa kuonana uso kwa uso ama kwa simu na si sms. M1 ndiye atakayewasilisha mambo yote yanayotoka kwenye kamati ya kitaifa na endapo kuna haja ya MM kukutana na kamati ya kitaifa, mipango yote ya kikao itafanywa na M1 kwa usiri mkubwa.”
Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Mkakati wa Mabadiliko 2013 ni mpango haramu na ambao unaichana chana Katiba ya Chama chetu. Ni mkakati wa vita dhidi ya Chama chetu na utaratibu wetu wa kikatiba.
1. Wakati ibara ya 10.1(iv) ya Kanuni za Uendeshaji Kazi za Chama ambazo ni sehemu ya Katiba ya Chama chetu ya mwaka 2006 inamkataza kiongozi wa CHADEMA asijihusishe na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini, au ukanda ambavyo vina makusudi ya kubaguana ndani ya Chama na miongoni mwa jamii kisiasa au kijamii”, wanaMtandao wa Ushindi wameonyesha wazi kuwa wanaendekeza siasa za udini kwa kusema yafuatayo juu ya waliemwita ‘mtu tunayemtaka’, yaani Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe: “Kwa kuwa ni Mwislamu, hii ni fursa katika kupata kuungwa mkono na wanachama waislamu ambao wamekuwa na kigugumizi wakidhani waislamu hawatakiwi katika uongozi wa taasisi yetu.”
2. Wakati ibara ya 10.1(viii) ya Kanuni za Uendeshaji inamtaka kila kiongozi wa CHADEMA “… kuwa mkweli na muwazi wakati wote … na aachane na vikundi vya majungu na wadanganyifu (rumour mongers) …”, wanaMtandao wa Ushindi wameeleza kwenye waraka wao kwamba mipango yao ya utekelezaji wa Mkakati wa Mabadiliko 2013 ‘itafanyika kwa usiri mkubwa.’
3. Wakati ibara ya 10.1(ix) ya Kanuni za Uendeshaji Kazi za Chama inamtaka “kiongozi asijihusishe na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama au wanachama wake”, wanaMtandao wa Ushindi wamesambaza tuhuma za uongo dhidi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa (ambaye wanamwita kwenye waraka wao kuwa ni ‘Mpinzani wetu’) kuwa “… hana mahusiano mema na mazuri na viongozi wa ngazi za chini kutokana na dharau nyingi anazozionyesha pale anapokutana na viongozi wa ngazi za chini akiwa katika kuijenga taasisi hii…. Hii imemfanya kutopendwa na viongozi wengi wa ngazi za chini hivi sasa na kutoa fursa ya pekee kwa tunayemtaka.”
4. Wakati ibara ya 10.1(x) ya Kanuni za Uendeshaji inamtaka “kiongozi asitoe tuhuma zozote juu ya viongozi wenzake pasipo kupitia vikao halali na kuzingatia taratibu na ngazi zilizowekwa kwenye Kanuni”, tuhuma zote zilizotolewa na wanaMtandao hawa dhidi ya viongozi wakuu wa Chama chetu hazijawahi kutolewa na yeyote kati ya wanaMtandao hawa katika kikao chochote halali cha Chama cha ngazi yoyote.
5. Wakati ibara ya 10.1(xii) ya Kanuni za Uendeshaji inaeleza kwamba “itakuwa marufuku kwa kiongozi wa CHADEMA kukashifu Chama, kiongozi au mwanachama yeyote wa Chama …”, Mkakati wa Mabadiliko 2013 umejaa kashfa kubwa, matusi mengi na udhalilishaji mkubwa wa Chama, viongozi wake wakuu na wanachama kwa ujumla. Hivyo, kwa mfano, Mwenyekiti wa Chama Taifa ametuhumiwa na wanaMtandao hawa kuwa ni mtu mwenye ‘uzalendo unaotia shaka’, mwenye ‘elimu ya magumashi’, ‘mzito kujieleza’, ‘mtu mwenye akili ndogo’, n.k.
Ndugu wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Hakuna chama au taasisi yoyote duniani inayoweza kunyamazia mkakati wa aina hii dhidi yake na viongozi wake wakuu na ikadumu au kubaki salama. Chama au taasisi yoyote inayoendekeza vitendo vya aina hii miongoni mwa viongozi wake wa ngazi yoyote au miongoni mwa wanachama wake wa kawaida inakaribisha kifo na mauti. Chama chetu na viongozi wake wa juu wamekaa kimya kwa muda mrefu sana; wamevumilia mashambulizi na kashfa nyingi sana dhidi yao binafsi na dhidi ya Chama; wamestahimili matusi makubwa sana dhidi yao. Chama chetu kimevumilia yote haya na viongozi wake wamevumilia yote haya sio kwa sababu walitaka Chama chetu kiuwawe na wanaMtandao hawa. Uvumilivu wote huu ulitokana na haja ya kuwapa wanaMtandao wa Ushindi fursa ya kugundua hatari ya siasa zao na kuwapa muda wa kujirekebisha na kujirudi.
Kama ilivyo kwa binadamu au taasisi yoyote ile, uvumilivu wa Chama chetu na viongozi wake wakuu una kikomo. Na hiki ndio kikomo cha uvumilivu wa Chama chetu, viongozi wake na wanachama wake kama wanavyowakilishwa na Kamati Kuu ya Chama chetu. Hivyo basi, katika kikao chake tajwa, Kamati Kuu ya Chama chetu, kwa kutumia mamlaka yake ya kikatiba ya dharura chini ya ibara ya 6.5.2(d) ya Katiba ya Chama, imeazimia yafuatayo kuhusu Mkakati wa Mabadiliko 2013 na hao wanaojiita wanaMtandao wa Ushindi:
(a) Kwamba, kuanzia sasa, viongozi wote waliohusika ama kuhusishwa na mkakati huu, yaani Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe, Mjumbe wa Kamati Kuu Dk. Kitilla Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha Samson Mwigamba wavuliwe nyadhifa zao zote za uongozi ndani ya Chama;
(b) Kwamba timu ndogo ya pamoja ya watendaji wa Sekretariat ya Makao Makuu ya Chama na wajumbe wa Kamati Kuu ifanye uchunguzi wa haraka ili kumtambua mtu anayeitwa M2 na ambaye anadaiwa kuwa mtumishi wa Makao Makuu ya Chama ili hatua stahiki na za haraka zichukuliwe dhidi yake, pamoja na watu wengine wote watakaobainika kuhusika na mpango huu wa uhaini dhidi ya Chama chetu;
(c) Kwamba Kamati ya Chama ya Wabunge inaelekezwa kuchukua hatua za haraka za kuhakikisha Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe anavuliwa madaraka yake yote kama Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, with immediate effect;
(d) Kwamba viongozi waliotajwa katika aya ya (a) waandikiwe hati zenye tuhuma dhidi yao haraka iwezekanavyo na watakiwe kujieleza kwa nini wasifukuzwe kwenye Chama kwa vitendo vyao na wapatiwe fursa kamili ya kujitetea kama inavyotakiwa na ibara ya 6.5.2(a), (b) na (c) ya Katiba ya Chama;
(e) Kwamba mara baada ya utekelezaji wa azimio (d), Kamati Kuu ikutane kwa dharura kwa ajili ya kufanya uamuzi juu ya hatma ya watuhumiwa na hatua nyingine zitakazofuata;
(f) Kwamba waraka wa wanaojiita wanaMtandao wa Ushindi uwekwe hadharani na usambazwe kwa vyombo vya habari vya aina zote ili wananchi wa Tanzania, wanachama na viongozi wa Chama chetu na dunia nzima kwa ujumla iweze kupima uzito wa Mkakati wa Mabadiliko 2013 na uhalali wa maamuzi haya ya Kamati Kuu.
Ndugu wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu Dk. Kitilla Mkumbo waliiomba Kamati Kuu iwaruhusu kujiuzulu nyadhifa zao baada ya Mkakati wao wa kukiteka nyara Chama na kukiangamiza kujulikana mbele ya Kamati Kuu. Kwa kuzingatia uzito wa makosa waliyokifanyia Chama, viongozi wake wakuu na wanachama wake kwa ujumla; na kwa kuzingatia uzito na umuhimu wa nyadhifa kubwa walizo nazo ndani ya Chama; na kwa kuzingatia uelewa wao wa Katiba, Kanuni na taratibu za Chama na uzoefu wao katika safu za juu za uongozi wa Chama, Kamati Kuu ilikataa kwa kauli moja kuridhia maombi hayo ya kujiuzulu. Kufanya hivyo ingekuwa ni sawa na kuwaruhusu wajiondoe kwenye uongozi wa Chama wakiwa na heshima wasizostahili hata kidogo.
Chama chetu ni tumaini pekee la Watanzania wote wanaotaka mabadiliko ya kweli na ya kimsingi katika mfumo wa kiutawala, kiuchumi na kijamii wa nchi yetu. Hii ndiyo sababu kubwa na ya pekee iliyosababisha vita kubwa na chafu inayopigwa dhidi ya Chama chetu na viongozi wetu wakuu. Lengo kuu ni kuwachafua viongozi wakuu, kuleta mgogoro na mgawanyiko ndani ya wanachama, viongozi wake na hivyo kukichafua Chama mbele ya macho ya Watanzania. Chama chetu kikishachafuka kwa mtindo huu, matumaini ya Watanzania wanaotaka mabadiliko yatakufa. Vita hii kubwa haijaanza jana, na haitaisha kesho. Kama ambavyo tumekabiliana nayo na kuishinda siku za nyuma, vivyo hivyo tutakabiliana nayo mara hii na kuishinda. Kama Chama chetu kilivyoibuka na nguvu na heshima kubwa zaidi katika mapambano ya siku za nyuma, vivyo hivyo Chama chetu kitaibuka na nguvu na heshima kubwa zaidi katika awamu hii ya mapambano.
Tunawaomba Watanzania, wanachama na viongozi wetu wasife moyo, bali waendelee kukiunga mkono chama chao cha ukombozi. Tunawaomba Watanzania, wanachama na viongozi wetu waendelee kulilinda tumaini lao pekee la mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Badala ya kukatishwa tama, kila mmoja wetu aongeze bidii maradufu ili kuwashinda wale wanaotaka kuleta majanga katika Chama chetu na kwa Taifa letu.

FREEMAN AIKAELI MBOWE (MB),                       WILBROD PETER SLAA
MWENYEKITI,  TAIFA                                        KATIBU MKUU

NA ANKAL MICHUZI

   

0 comments:

Post a Comment