Waziri Mkuu Mizengo Pinda
****
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda
anaondoka Dar es Salaam leo mchana (Jumanne, Oktoba 15, 2013)
kwenda China kwa ziara ya kikazi ya
siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo inayotarajiwa kuanza kesho,
Oktoba 16.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, lengo la ziara ya Waziri
Mkuu ni kutangaza fursa za uwekezaji hapa nchini, fursa za biashara, za utalii
na kutafuta mitaji kwa ajili ya sekta zilizo chini mpango wa matokeo makubwa ya
haraka (Big Results Now Initiative).
Akiwa China, Waziri Mkuu atakuwa na
mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Mhe. Li Keqiang na viongozi wa Serikali
ya China katika katika sekta za uchukuzi, mawasiliano, viwanda, madini na
nishati.
Atatembelea mji wa Beijing na majimbo
ya Shenzen, Chengdu na Guangzhou ambako atakutana na Makamu wa Rais wa China,
Rais wa Benki ya Exim ya China, Rais wa Benki ya Maendeleo ya China, wakuu wa
mashirika makubwa na kampuni kubwa nchini China na kufanya nao mazungumzo.
Waziri Mkuu Pinda ataungana
na Wakuu wa Nchi watano kwenye ufunguzi wa maonyesho ya kibiashara ya magharibi
mwa China (Western China International Fair – WCIF) ambako atahutubia washiriki
wa maonyesho hayo. Pia atatembelea maeneo kadhaa ya uwekezaji na kufungua
Kongamano la Uwekezaji baina ya Tanzania na China litakalofanyika Guangzhou.
Vilevile, Waziri Mkuu
anatarajiwa kufungua mafunzo ya siku 10 kwa maafisa 20 kutoka idara na taasisi
za serikali za hapa nchini yanayoendeshwa kwa pamoja baina ya Chuo cha Uongozi
cha China na Taasisi ya Uongozi ya Tanzania. Mafunzo hayo ni sehemu ya mpango
wa Serikali kuboresha utendaji wa Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje
(EPZ).
Waziri Mkuu ambaye
anafuatana na Mawaziri wanne, wabunge wawili, wakuu wa mikoa watatu, wakuu wa
taasisi wa Serikali na wawakilishi kutoka sekta binafsi, anatarajiwa kukutana
na Watanzania waishia China huko Beijing na Guangzhou.
Tanzania imekuwa na uhusiano na ushirikiano wa karibu
na China, nchi kubwa ya Bara la Asia, tangu mwaka 1964.
China yenye ukubwa wa kilometa za
mraba 9,596,961 ina wakazi wapatao 1,349,585,838. Kwa
mujibu wa takwimu za Shirika Fedha la Kimataifa (IMF) nchi hiyo ni ya pili kwa
uchumi mkubwa duniani.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
JUMANNE, OKTOBA 15, 2013
0 comments:
Post a Comment