Mhe.
Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa akiongea na waandishi wa habari mapema jana kwenye ukumbi wa
mkutano wa Wizara ya Mambo ya Nje, jijini Dar es Salaam. Kulia ni Balozi Rajabu Gamaha, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje.
Mhe.
Waziri Membe akifafanua ombi la Kenya kuhusu uhalali wa kuwafikisha
Viongozi Wawili wa juu wa Serikali ya Kenya kwenye Mahakama ya Kimatafa
(ICC) kujibu Makosa ya Jinai. Kulia ni Balozi Rajabu Gamaha na kushoto ni Balozi Vincent Kibwana, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Wakurugenzi wakisikiliza kwa makini maswali mbalimbali yaliyokuwa yakiulizwa na waandishi wa habari (hawapo pichani). Kulia ni Bw. Mndeme, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, na Bw. Ligaganya, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango.
Kwenye Mkutano pia alikuwepo Bw. Kaaya (wa pili kulia), Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa
Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje ukijumuisha Balozi Irene Kasyanju (kushoto), Mkurugenzi wa Kikengo cha Sheria, Balozi Simba Yahya (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Balozi Mbelwa Kairuki (wa tatu kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia na Balozi Dora Msechu (wa nne kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika.
Wengine waliohudhuria Mkutano huo ni Bw. Mkubwa Ally (kushoto), Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali cha Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Thobias Makoba (katikati) na Bw. Togolani Mavura (kulia), Wasaidizi wa Mhe. Waziri Membe.
Mmoja wa waandishi kutoka gazeti la The Citizen, Bw. Mkinga Mkinga akiuliza swali kwa Mhe. Waziri Membe.
Waandishi wa habari waliokusanyika kumsikiliza Mhe. Waziri Membe.
Mhe.
Waziri Membe akihojiwa na Bw. Erick David Nampesya,
Mwandishi/Mtangazaji wa Shirika la Habari la BBC.Picha Zote na Tagie
Daisy Mwakawago-Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
****
Na TAGIE DAISY MWAKAWAGO
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe
(Mb), akutana na waandishi wa habari jana kujadili uhalali wa kuwafikisha
Viongozi Wawili wa juu wa Serikali ya Kenya kwenye Mahakama ya Kimatafa
kujibu Makosa ya Jinai. Mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa
mikutano wa Wizara ya Mambo ya Nje, jijini Dar es Salaam.
Waziri
Membe alikuwa akielezea yaliyojiri kwenye Kikao cha dharura cha Viongozi
Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (UA) kilichomalizika mjini Addis
Ababa, nchini Ethiopia jana tarehe 12 Oktoba, 2013. Kikao hicho
kilihudhuriwa pia na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Mfalme Mswati wa III, Rais wa Swaziland, na
Viongozi Wakuu na Watendaji Wakuu wa Serikali barani Afrika.
Kikao hicho
kiliitishwa kutokana na ombi la Serikali ya Jamhuri ya Kenya ya kutaka
UA kujadili mahusiano yaliyopo kati ya nchi za Afrika na Mahakama ya
Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) na iwapo ni sahihi kwa Viongozi Wakuu
wa Nchi za Afrika kufikishwa katika Mahakama hiyo kujibu mashtaka
wakati wakiwa madarakani.
“Viongozi
hao wa Afrika waliazimia mambo makuu matano,” alieleza Waziri Membe,
huku akiyataja mawili kuwa hakuna Kiongozi yoyote kutoka barani Afrika
atakayepelekwa ICC au Mahakama yoyote kujibu mashtaka wakati akiwa
madarakani hata akiwa anashika nafasi ya kukaimu.
Mengine ni
kuwa mashtaka yanayomkabili Kiongozi yoyote barani Afrika yasubiri hadi
Kiongozi huyo atakapomaliza muda wa uongozi wake. Aidha, Mhe. Waziri
alieleza kusikitishwa kwa Viongozi wa Afrika na namna Mahakama ya ICC
inavyoendesha shughuli zake kwa kile walichokiita “kuwaandama Viongozi
wa Bara la Afrika kuliko Viongozi wa Mataifa mengine hata pale
panapokuwa na ushahidi wa Viongozi hao wengine kufanya makosa ya Jinai.”
Waziri
Membe alihoji inakuwaje kwamba kati ya kesi 30 zilizopelekwa ICC tangu
mwaka 2004, ishirini na saba (27) zinatoka barani Afrika. “Haya yote
yalijadiliwa kwa kina, pamoja na pendekezo la kujitoa kwenye uanachama
wa Mahakama ya ICC,” aliongeza Waziri Membe.
Alisema
suala la kujitoa uanachama wa ICC limeachiwa kila nchi kuamua, ingawaje
linategemewa kujadiliwa tena katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje
na Mawaziri wa Sheria wa nchi wanachama wa mahakama hiyo
kitakachofanyika tarehe 29 Novemba mwaka huu nchini Uholanzi. Hivi sasa
kuna nchi thelathini na nne (34) barani Afrika ambazo ni wananchama wa
Mahakama hiyo.
Akiendelea
kuzungumza katika Mkutano wake wa leo na waandishi wa habari ambao pia
ulihudhuriwa na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Waziri Membe amesema kuwa Umoja wa Afrika umepeleka ombi lake
rasmi kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kuahirisha
kesi inayowakabili viongozi hao wa Kenya.
Wakati huo
huo, Mhe. Waziri Membe alitumia fursa ya mkutano wake na waandishi wa
habari kutoa salamu za pole kwa Bibi Ufoo Saro, Mwandishi/Mtangazaji wa
kituo cha televisheni ITV, na familia yake, kufuatia taarifa
iliyomfikia kuwa Bibi Saro amelazwa hospitali akiwa mahututi baada ya
kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya. Mama yake mzazi, Anastazia Saro na
mtoto wake waliuwawa katika shambulio hilo. Taarifa zinasema mtuhumiwa
ni mchumba wa Bibi Saro, ambaye anadaiwa kufyatua risasi kwa familia
hiyo na hatimaye kujipiga risasi na kufa.
Sambamba na
taarifa hiyo, Mhe. Waziri Membe pia aliwatakiwa wananchi sikukuu njema
ya Kumbukumbu ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,
ambayo itaadhimishwa Kitaifa kesho tarehe 14 Novemba 2013.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment