SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Monday, October 14, 2013

Taarifa Kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Kuhusu Ugonjwa na Homa ya Uti wa Mgongo Nchini

 JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
 Utangulizi

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa  kwa umma juu ya kuwepo kwa Ugonjwa wa Homa ya Uti wa Mgongo mkoani Rukwa.  Ugonjwa umedhibitika kuwepo baada ya Vipimo vya Maabara kuonyesha uwepo wa vijidudu vya homa ya uti wa  mgongo kwenye sampuli za wagonjwa waliolazwa kwenye Hospitali ya Mkoa Sumbawanga. Hadi kufikia tarehe 08/10/2013  jumla ya wagonjwa   21 wameripotiwa katika hospitali ya Mkoa na  kati yao  wanne (4) wamefariki dunia


Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi wote, katika mikoa yote ya 
Tanzania hususani mikoa iliyo mpakani na mkoa wa Rukwa na vile vile wasafiri wanaotarajiwa kwenda mkoani Rukwa.

Homa ya Uti wa Mgongo

Homa ya Uti wa Mgongo inasababishwa na bakteria aitwaye Neisseria meningitidis. Bakteria huyu ndiye anayeleta milipuko mikubwa ya Homa ya Uti wa mgongo. Ugonjwa huu hatari unaathiri zaidi meninji na husababisha athari kubwa kwa ubongo. Ugonjwa huu unapatikana kwa binadamu tu. Asilimia 50 za wagonjwa hupoteza maisha iwapo matibabu hayataanzishwa mapema.

Dalili kuu ni Kukakamaa kwa shingo, Homa kali, Kutokupenda mwanga mkali, Kuchanganyikiwa, Kichwa kuuma pamoja na Kutapika. Ugonjwa huu unaweza kuathiri ubongo na kupelekea kupoteza uwezo wa kusikia au kupoteza kabisa uwezo wa kuelewa na kunyambulisha vitu mbalimbali. Iwapo ugonjwa huu utaathiri ubongo na meninje kwa kiasi kikubwa, umauti hutokea. Dalili za ugonjwa ni kati ya siku 2 hadi 10 baada ya kupata maambukizi.

Ugonjwa huu unaenezwa kutoka kwa binadamu kwenda kwa binadamu kwa njia ya hewa au kwa kugusa majimaji/mate kutoka kwa mtu ambaye tayari ni mgonjwa. Ugonjwa huu unaenea kutoka mtu mmoja hadi mtu mwingine kwa urahisi na kwa kasi sana iwapo mtu atakuwa karibu na mgonjwa mwenye maambukizi kwa muda mrefu. Uambukizo unaweza kutokana iwapo mgonjwa atapiga chafya au mate ya mgonjwa huyu kuguswa. Aidha kasi ya maambukizi pia inatokea iwapo mtu ataishi kwa karibu ndani ya nyumba moja na mgonjwa na kushirikiana naye kwa kula chakula kwenye chombo kimoja.

Ugonjwa huu unatibika iwapo mgonjwa atawahi hospitalini na kupewa dawa.

Hatua zinazochukuliwa na Wizara

Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara hususan mikoa inayopakana na Rukwa. Aidha taarifa hii pia imewakumbusha waganga wakuu warejee miongozo yao ya kudhibiti Ugonjwa wa Homa ya Uti wa Mgongo yaani namna ya utambuzi wa mgongwa na, uchukuaji wa sampuli
Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipakani. 

Kutuma Timu ya Taifa ya Maafa ambayo imeenda kuungana na timu za Mkoa na Wilaya za Rukwa katika kukabilana na ugonjwa huu. Aidha timu hiyo imeondoka tarehe 10.10.2013.

Kutuma chanjo pamoja na dawa na vifaa Kinga kwa mkoa wa Rukwa ili kuweza kukabilana na ugonjwa huuElimu ya Afya  inaendelea kutolewa katika maeneo  ambayo yamekumbwa na mlipuko na pia mashuleni, vyuoni, magerezani, nakwenye mikusanyiko na msongamano wa watu. Aidha wananchi wanashauriwa kujenga nyumba bora zenye madirisha yanayoingiza hewa na mwanga wa kutosha.

Kufungua kambi maalamu mkoani Rukwa kwa ajili ya wagonjwa wa Homa ya Uti wa Mgongo.

Wananchi wanashauriwa kutoa taarifa pindi kutoa taarifa kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu mara watakapoona mgonjwa yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Wadau wengine wanaendelea na mikakati ya kuhakikisha ugonjwa huu unathibiwa mkoani Rukwa na kwa mikoa mengine.

Imetolewa na:

Nsachris  Mwamwaja
Msemaji
12 Oktoba 2013

0 comments:

Post a Comment