--
WAZIRI Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msingwa amemtaka Rais Jakaya Kikwete kumchukulia hatua kali za nidhamu Waziri wa wizara hiyo, Balozi Khamis Kagashehi kutokana na kuonyesha udhaifu kiutendaji.
Hatua hiyo inatokana na taarifa za kukamatwa kwa kontena mbili za pembe za ndovu zenye thamani ya Sh5.4 bilioni.
Pembe hizo zilikamatwa na maofisa forodha wa Hong Kong zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Tanzania na Kenya.
Pembe hizo zilikuwa vipande 1,209 vyenye uzito wa tani nne zilikamatwa wiki iliyopita nchini China, zikiwa kwenye kontena mbili ambazo ziliwekwa alama kuwa zimebeba plastiki chakavu na maharage aina ya Roscoco.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mchungaji Msigwa alisema ufisadi wa kusafirisha Twiga nje ya nchi hadi kwenye wizi wa pembe za ndovu, ni mwendelezo wa kutokuwapo kwa ufanisi katika wizara hiyo.
Alisema tangu kutokea kwa taarifa hizo za kukamatwa kwa pembe za ndovu Waziri ameshindwa kuueleza umma wa watanzania kuhusu hatua ambayo ameichukua akiwa kama mtendaji mkuu wa wizara.
“Katika bunge la bajeti nilitoa rai, nikimtaka Waziri Kagasheki na Serikali kuchukua hatua kuokoa maliasili na utajiri huu wa taifa, lakini hakuna kinachoendelea,” alisema Mchungaji Msingwa.
“Uwendawazimu ni kufanya jambo lilelile kwa njia ileile huku ukitegemea matokeo tofauti, hivyo umefika wakati kwa Rais Kikwete kumchukulia hatua Waziri Kagasheki,” alisema.
Alisema serikali imewachukulia hatua kali viongozi wadogo na kuwaacha majangili wakubwa wakiendeleza wimbi la kuihujumu rasilimali ya Watanzania.
“Tukumbuke Mwalimu (Julius) Nyerere aliwahi kusema serikali ‘Currupt’ hukimbizana na watu wadogowadogo tu, Serikali ‘corrupt’ haiwezi kuwachukulia hatua watoa rushwa wakubwa,” alisema Mchungaji Msingwa.
Jitihada za kumpata Balozi Kagasheki kuzungumzia suala hilo jana, hazikufanikiwa kutokana na simu yake ya mkononi kutokuwa hewani muda wote
0 comments:
Post a Comment