Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL), Kapteni Milton Lusajo Lazaro.
---
Na Mwandishi wetu
IKIWA ni siku mmoja tu baada ya kuteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL), Kapteni Milton Lusajo Lazaro amesema shirika hilo linanafasi kubwa ya kupata mafanikio iwapo litaendelea kutekeleza mpango wake wa maendeleo wa miaka mitano.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana, Lusajo alisema atatumia uzoefu wake alioupata katika sekta ya usafiri wa anga kuleta mabadiliko katika shirika hilo na kuliwezesha kushindana sambamba na kampuni nyingine za ndani na nje ya nchi.
Kpt. Lusajo, rubani anaeheshimika katika sekta ya usafiri wa anga si kwa Afrika Mashariki pekee ila Afrika kwa ujumla ana rekodi ya kuendesha ndege kwa saa zaidi ya elfu kumi na mbili, pia amewahi kushika nyadhifa mbali mbali katika Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) pamoja na ATCL kabla ya kuteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL.
“Napenda kutoa shukrani zangu kwa Waziri Mwakyembe na viongozi wengine wa Wizara kwa kuwa na imani nami. Nimekubali uteuzi wake na nitafanya kazi aliyonipa kwa moyo mmoja.
Ninaahidi kuwa nitautumia uzoefu wangu wa zaidi ya miaka 35 katika sekta ya usafiri wa anga na kuipa ATCL uwezo kushindana kibiashara. Natoa wito kwa wafanyakazi wenzangu kutoa ushirikiano ili tuweze kusonga mbele. ” Alisema.
Lazaro alisema Shirika lake litaendelea kutoa huduma kama kawaida na kuongeza kuwa safari zote za Shirika zitaendelea kama ilivyopangwa na ratiba licha ya mabadiliko ya uongozi.
“Hakuna sababu ya wananchi kuwa na wasi wasi. Kilichotokea ni mabadiliko ya uongozi tu lakini mipango na shughuli zote za Shirika zinaendelea kama ilivyopangwa,” alisema.
Lazaro aliongeza kusema, kuwa jukumu kubwa alionalo mbele yake ni kuongeza idadi ya ndege za shirika hilo aidha kwa kukodi au kuingia ubia na mashirika mengine katika jitihada za kuimarisha nafasi ya kampuni yake ili iweze kushindana Kitaifa na Kimataifa katika miaka michache ijayo.
“ATCL haiwezi kupata mafanikio bila kuwa na ushirikiano mzuri na Serikali pamoja na wananchi kwa ujumla. Nawaomba wananchi waendelee kuonyesha ushirikiano na uzalendo waliouonyesha katika wiki chache zilizopita baada ya kuanza kwa huduma za kampuni yetu.
“Nawahakikishia wateja wetu na wananchi kwa ujumla kuwa kampuni yangu itaendelea kutoa huduma na bidhaa bora zilizo katika bei za kiushindani ukilinganisha na makampuni mengine yanayotoa huduma hii katika soko,” alisema.
0 comments:
Post a Comment