Kampuni ya Ndege Nchini (ATCL), leo inaanza kurusha ndege zake huku serikali ikiitahadharisha kuwa ihakikishe inafanya biashara kwa faida na kuweza kujiendesha yenyewe ikiwemo kumudu kulipa mishahara ya wafanyakazi wake.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa wadau wa sekta ya uchukuzi, Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu, alisema serikali imeipatia kampuni hiyo fedha za kutosha kwa ajili ya kuiwezesha kuanza kufanya biashara ingawa hakusema ni kisia gani.
Hata hivyo, Nundu alisema awamu hii serikali haitarajii kuona ATCL inafanya biashara kwa hasara na kuendelea kutegemea serikali kulipa mishahara ya wafanyakazi wake.
ATCL inatarajia kuanza safari zake kwa kutumia ndege yao moja huku nyingine ikiwa inafanyiwa matengenezo hapa nchini kati ya mikoa wa Tabora, Kigoma na Dar es Salaam.
Alisema kampuni hiyo itaanza kwa kwa kishindo safari ili kupunguza tatizo la usafiri katika mikoa hiyo.
Alisema ndege ya pili itakapokamilika kufanyiwa matengenezo, nayo itaanza safari katika maeneo mengine ambayo yatabainishwa hapo baadaye.
Katika harakati za kuifufua kampuni hiyo mwanzoni mwa mwaka huu, Serikali ililipa fedha za matengenezo ya ndege moja ya ATCL iliyopelekwa Afrika Kusini kwa ajili ya matengenezo ambapo pia baada ya muda ilipelekwa ndege nyingine na malipo kufanyika.
ATCL ilibinafsishwa na Serikali Novemba mwaka 2002 kwa kuuza asilimia 49 ya hisa zake kwa Shirika la Ndege la Afrika Kusini na kuunda ATCL, ambapo ubia wa mashirika hayo ulisitishwa Agosti 2006, baada ya utendaji wake wa kusuasua.
Mwaka 2007, kampuni ilikabidhiwa kwa Bodi na Menejimenti ya Watanzania ambapo huduma zake ziliendelea kudorora hadi kushindwa kutoa huduma kabisa
CHANZO: NIPASHE





0 comments:
Post a Comment