Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Maridhiano nchini Kenya ajiuzulu kwa muda
Mwenyekiti wa Tume ya Ukweli Haki na Maridhiano nchini Kenya TJRC, Balozi Bethuel Kiplagat amejiuzulu kwa muda ili kutoa nafasi kwa jopo la majaji lililoteuliwa kumchunguza lifanye kazi yake kwa uwazi zaidi. Kiplagat amekuwa chini ya mashinikizo makali kutoka kwa wananchi na makundi ya kijamii kujiuzulu kwa tuhuma kuwa alihusika katika dhulma za miaka ya huko nyuma alipohudumu katika serikali ya Rais Mustaafu Daniel Arap Moi na kwa msingi huo hawezi kuleta maridhiano ya kitaifa nchini humo. Balozi Kiplagat amekuwa akikanusha tuhuma hizo na hivi majuzi alimuomba Jaji Mkuu wa nchi hiyo Evan Gicheru kuteua jopo la majaji kuchunguza madai dhidi yake. Katiba ya Kenya inasema kuwa viongozi wa tume mbali mbali za kitaifa wanapaswa kujiuzulu kwa muda iwapo watakabiliwa na tuhuma zozote hususan iwapo jopo la majaji litaundwa kuwachunguza. Bethuel Kiplagat amepongeza hatua ya kuundwa jopo hilo akisema kuwa shaka ya miaka mingi ya Wakenya kuhusu shaksia yake zitafika mwisho baada ya uchunguzi kukamilika. Wakati huo huo Mahakama ya viwanda jijini Nairobi imewataka wafanyakazi wa kuvuna majani chai walioko mgomoni warudi katika sehemu zao za kazi. Mgomo huo umeendelea kwa takriban majuma mawili na ulitokana na hatua ya makampuni kadhaa ya majani chai kuagiza mitambo ya kuvuna chai jambo ambalo wafanyakazi hao wanahofia huenda likawasababishia kupoteza nafasi zao za kazi.
0 comments:
Post a Comment