Na Grace Michael, Dodoma
MKAGUZI na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bw. Ludovick Utouh
amesema kuwa ofisi yake imebaini kuwa sh. bilioni 67.4 zimetumika bila
kupitishwa na bunge.
Mbali na hiyo pia amesema kuwa deni la Taifa limeongezeka kutoka sh. trilioni 6.4
hadi kufikia sh. trilioni 7.6 katika mwaka wa fedha 2007/08 hadi 2008/09.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Bw. Utouh alisema kuwa ongezeko hilo ni sawa na
asimilia 18, huku madeni ya ndani ambayo yalitakiwa yawe yamelipwa
katika mwaka wa fedha uliopita ni sh. bilioni 107 ambazo ni asilimia 50
ikilinganishwa na
madeni yasiyolipwa ya mwaka uliopita, hali itakayoathiri bajeti ya mwaka unaofuata na kuongeza gaharama ya riba.
Bw. Otouch ambaye ripoti yake imewagawanyika katika maeneo mawili
ambayo ni fedha na ufanisi, kwa upande wa fedha ripoti hiyo imejikita
katika ukaguzi wa Serikali Kuu, Serikali za Mtaa na Mashirika ya
Umma na kwa upande wa ufanisi imeelezea kuhusu ufanisi na thamani ya fedha kwenye sekta ya barabara.
Akizungumzia Serikali Kuu, alisema kuwa kwa upande wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), mambo yaliyojitokeza ni pamoja na
kutoshughulikiwa kwa madeni ya nyuma yenye thamani ya sh. bilioni 95.7
pamoja na dola za Marekani milioni 47.9.
Alisema kuwa makusanyo ya mamlaka hiyo kwa Tanzania Bara yamekuwa
na upungufu wa sh. bilioni 426 huku kukiwa na utata kwenye makusanyo
yanayokusanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwa mengine
hayaingizwi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kama sheria inavyotaka.
Hata hivyo, alisema kuwa TRA ingeweza kukusanya fedha nyingi zaidi ya kiasi kilichokusudiwa
endapo kusingetolewa misamaha katika taasisi mbalimbali na watu
binafsi yenye thamani ya sh. bilioni 752.3, hivyo akapendekeza serikali
kuangalia upya sera ya misamaha ya kodi.
Mkaguzi huyo pia liitaka serikali kuepuka kufanya maazimio
yatakayosababisha kuongezeka kwa madeni kutokana na madeni
yanayotarajiwa ambayo hadi kufikia mwaka Juni 30, mwaka jana yalifikia
sh. bilioni 42 yaliyohusisha wizara saba na mikoa miwili.
Kwa upande wa hesabu za Serikali za Mtaa, alisema kuwa kutokana na
halmashauri kutokagua mara kwa mara hati za malipo ya mishahara, jumla
ya sh. milioni 792.9 zililipwa katika benki za wafanyakazi hewa,
wakiwamo waliostaafu, waliotoroka, walioacha kazi na waliofukuzwa kwa
kuwa majina yao hayakuondolewa.
Alisema kuwa jumla ya sh. bilioni 1.4 ya mishahara ya wafanyakazi
hao ilibaki kwenye akaunti za halmashauri bila ya kurejeshwa Hazina na
kutokana na mambo hayo, CAG, ameagiza kufanyika kwa ukaguzi maalumu
katika Halmashauri ya Rombo.
Alisema kuwa ukaguzi huo ulibaini ukiukwaji wa sheria ya manunuzi ambapo Halmashauri 26
zilinunua vifaa vya sh. milioni 111.5 lakini havikuingizwa kwenye madaftari ya vifaa na matumizi yake hayakufahamika.
Alisema kuwa Halmashauri nyingi zilionekana kuwa na udhaifu katika
ukusanyaji wa mapato na uingiaji wa mikataba, kutoa taarifa
zinazotofautiana kwa ajili ya kuwasilisha katika taasisi moja, kuandaa
taarifa ambazo hazizingatii hali halisi ya miradi na hivyo kupotosha
ukweli kwa kuwa zinaandaliwa ofisini bila ya kuangalia hali halisi ya
utekelezaji wa mieadi.
Kwa upande wa Mashirika ya Umma, alisema kuwa kuna haja ya kuwa na chombo madhubuti ambacho
kitasimamia mashirika ili kukidhi matarajio ya watanzania.
Alisema kuwa kuna mgongano wa maslahi kwa wabunge kutokana na kuwa
wajumbe wa Bodi za wakurugenzi wa mashirika ya umma na taasisi
mbalimbali hivyo akasema kuwa utaratibu huo ni kinyume cha Utawala
Bora, hivyo akaitaka serikali kutoa waraka
ambao utawazuia wabunge kuwa wajumbe wa bodi.
Alisema kuwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi inadaiwa jumla ya sh.
bilioni 58 ilizokopa kutoka PSPF chini ya udhamini wa serikali mwaka
2006 lakini marejesho yake yamekuwa hayaridhishi kwa wanafunzi hao.
Tuesday, May 4, 2010
Bil. 67/-zatumika bila idhini ya bunge
Posted by
Ally Shaaban Mgido's
at
Tuesday, May 04, 2010
Email This
BlogThis!
Share to X
Share to Facebook
0 comments:
Post a Comment