JIJI la Dar es Salaam leo linaanza kuzizima kutokana na ugeni wa watu
zaidi ya 1,000 kutoka nchi 85 wanaowasili kushiriki mkutano wa Uchumi
wa Dunia kuhusu Bara la Afrika (WEF).
Jamii ya wakazi wa Dar es Salaam imekuwa katika nafasi ya kuufahamu
mkutano huo, hususan baada ya kutangazwa uamuzi wa kufunga baadhi ya
barabara kwa ajili ya kupisha shughuli za mkutano huo ambao umetajwa
kuwa na manufaa makubwa kwa nchi.
Tangu ilipotangazwa juzi kwenye televisheni juu ya uamuzi wa
kufunga kwa muda baadhi ya barabara, zimekuwapo hoja kutoka watu
mbalimbali juu ya kile kinachoelezwa, kwamba hatua hiyo itaongeza
msongamano wa magari katika Jiji.
Hata hivyo akizungumza jana na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, William Lukuvi, aliwaondolea wasiwasi wakazi hao kwamba
barabara hizo hazitafungwa moja kwa moja isipokuwa katika muda maalumu.
Lukuvi alisema hata wakati wa msafara, magari ya dharura yakiwamo
ya zimamoto na ya wagonjwa yataruhusiwa kupita. Alisema pia magari ya
wanafunzi na wafanyakazi yataruhusiwa kupita wakati utakapopatikana
upenyo.
Kwa mujibu wa Lukuvi, barabara hizo zitaanza kufungwa kuanzia leo hadi Jumamosi; mkutano utakapofungwa.
“Barabara hizi zilizoteuliwa, zitakuwa zinafungwa na kufunguliwa
mpaka mkutano uishe na hii itasimamiwa na polisi wetu, hivyo wananchi
watarajie usumbufu kidogo,” alisema.
Barabara zitakazofungwa ni ya Nyerere kutoka Uwanja wa Ndege hadi
katikati ya Jiji ambayo itatumiwa na wageni wanaokuja kuhudhuria
mkutano huo unaofunguliwa rasmi kesho.
Kesho hadi Ijumaa, kuanzia saa moja mpaka saa tatu asubuhi,
barabara ya Ali Hassan Mwinyi itatumika kusafirisha wageni kwenda
kwenye kumbi za mikutano zilizopo kando ya barabara ya Sam Nujoma.
Mkuu wa Mkoa alifafanua, kwamba barabara hizo zitafungwa kutokana
na wageni wengi kulala katika hoteli zilizo katikati ya Jiji na kwamba
baadaye zitafunguliwa kwa matumizi ya kawaida.
Itakapofika saa 9 alasiri, barabra hizo zitafungwa tena hadi saa
moja usiku kwa ajili ya washiriki wa mkutano kurudi katika hoteli
walimofikia.
Wakazi wa Sinza, Kijitonyama, Mwenge na wote wanaotumia barabara ya
Ali Hassan Mwinyi, wanashauriwa kutumia barabara ya Morogoro huku
wakazi wa Mbezi, Mikocheni, Kawe, Msasani wameshauriwa kutumia barabara
ya Old Bagamoyo ili kuepuka usumbufu.
Aidha, wananchi wanaopata huduma katika maduka ya Mlimani City
wameshauriwa kutumia barabara ya Chuo Kikuu cha Ardhi, kwani barabara
ya Sam Nujoma, itakuwa ikitumika kwa shughuli za mkutano huo.
Hata hivyo, Lukuvi aliomba radhi wananchi kwa usumbufu
utakaojitokeza kwa kipindi chote cha mkutano huo ambao unatarajiwa
kuinufaisha nchi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa WEF, tangu taasisi yake ianze kuandaa
mikutano ya aina hii, haijawahi kupata washiriki wengi kama ilivyo
katika mkutano huu unaofanyika nchini.
Katika hatua nyingine, wanaharakati kutoka zaidi ya nchi 10 za Afrika, wamejiandaa kuandamana katika barabara ya Sam Nujoma.
Katika barabara hiyo, ndiko uliko ukumbi wa Mlimani City, ambako
mkutano huo utafanyika, na wanaharakati hao wana lengo la kuwasisitiza
viongozi wa nchi mbalimbali kukumbuka majukumu yao ya kupambana na
matatizo yakiwamo ya kiafya.
Taarifa ya Jonathan Rousse, ambaye ni Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa
Jamii, Masoko na Maendeleo wa Umoja wa Watetezi wa Haki na Mapambano
dhidi ya Ukimwi Afrika Kusini (Arasa), ilisema maandamano hayo
yatafanyika kuanzia saa 4 asubuhi.
Katika mkutano kama huo uliofanyika Cape Town, Afrika Kusini mwaka
jana, wanaharakati hao waliandamana huku wakibeba puto mfano wa jicho
likiwa limeandikwa ‘We Are Watching – Fund the fight against HIV and TB
(Tunaona – Fadhilini mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi na Kifua
Kikuu)’.
Lengo lilikuwa ni kuwakumbusha viongozi wa Dunia ahadi zao za
kufadhili na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya katika kuzuia
maambukizi ya virusi, tiba na huduma.
Maandamano ya mwaka huu kwa mujibu wa Rousse, ni kuwakumbusha
viongozi hao jinsi walivyoshindwa kutekeleza ahadi zao katika
kuhakikisha huduma hiyo inapatikana, kwani hali hiyo imekuwa pigo kwa
Waafrika, kwani uchumi wa nchi zao hauwezi kukua kama wananchi hawana
huduma nzuri za kiafya.
“Mamia wanatarajiwa kushiriki maandamano haya, wakiwa wamebeba
maputo mithili ya macho, ili kuwakumbusha viongozi kwamba tunaona na
tunapanga kuwawajibisha kutokana na ahadi zao katika sekta ya afya,”
alisema Rousse katika taarifa yake.
Alisema risala inayozungumzia malalamiko ya jamii, itawasilishwa
kwa Mkurugenzi wa Uhusiano wa Nje wa Mfuko wa Kupambana na Ukimwi,
Kifua Kikuu na Malaria, pia Kamishna wa Afya wa Serikali ya Tanzania,
ambaye atasambaza ujumbe huu kwenye mkutano huo wa uchumi.
Tuesday, May 4, 2010
Dar es S alaam kuzizima kwa ugeni mkubwa
Posted by
Ally Shaaban Mgido's
at
Tuesday, May 04, 2010
Email This
BlogThis!
Share to X
Share to Facebook
0 comments:
Post a Comment