Pakistan yataka kushirikiana na India kuangamiza ugaidi
Shah Mehmood Qurashi, waziri
wa mambo ya kigeni wa Pakistan
Pakistan hii leo imeihimiza India
ishirikiane katika kubadilishana habari za ujasusi ili kukabiliana na
ugaidi kwenye mkutano muhimu uliofanyika leo mjini Islamabad
Mkutano wa mjini Islamabad umelenga kuyafufua mazungumzo ya amani
yaliyovunjika na kurejesha uhusiano wa kawaida baada ya uhusiano kati
ya nchi hizo mbili kuingia doa kufuatia mashambulio ya kigaidi ya mwaka
2008 katika mji wa Mumbai.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Pakistan, Shah Mehmood Qureshi na
mwenzake wa India, S M Krishna wameanza rasmi mazungumzo yao kwa kipindi
maalum cha upigaji picha katika wizara ya kigeni ya Pakistan mjini
Islamabad hii leo. Afisa wa wizara hiyo amesema mkutano kati ya mawaziri
hao umefanyika katika mazingira ya kirafiki na kwamba yapo matumaini ya
kupiga hatua mbele katika juhudi za kuufufua mchakato wa kutafuta amani
kati ya India na Pakistan.
Mkutano huo ni wa kwanza wa aina yake kuwahi kufanyika kutafuta
maridhiano na kurejesha uhusiano wa kawaida kati ya India na Pakistan
tangu mashambulio ya kigaidi dhidi ya mji wa Mumbai mnamo mwaka 2008.
Mazungumzo kati ya India na Pakistan yamekuwa yakikabiliwa na vikwazo
tangu miaka mingi kwa sababu pande zote mbili zina mawazo tofauti kuhusu
masuala yanayotakiwa kujadiliwa. Huku Pakistan ikiuona mzozo wa jimbo
la Kashmir kuwa ufunguo wa uhasama kati yake na India, India kwa upande
wake inataka kujadili jukumu la Pakistan katika kudhamini mashambulio ya
kigaidi na harakati za makundi ya wanamgambo nchini India.
Mtaalam wa uhusiano kati ya India na Pakistan, mjini New Delhi, Suba
Chandran, anasema, "Mazungumzo jumla ni mapana. Makubaliano yaliyofikiwa
mwaka 1998 yanatoa msingi mzuri wa mazungumzo yoyote katika siku za
usoni. Nitafurahi kama nchi zote mbili zitayazingatia makubaliano hayo
kwa kuwa yanatoa muelekeo kuzungumzia masuala yote kuhusu nyuklia na
biashara."
Waziri wa mambo ya kigeni wa India, SM Krishna amekutana pia na
waziri mkuu wa Pakistan, Yousuf Raza Gilani na rais Asif Ali Zardari
katika neo lililo chini ya ulinzi mkali la "Red Zone" ambako ni makao ya
afisi za serikali na balozi za nchi za kigeni katikati ya mji mkuu,
Islamabad.
SM
Krishna, waziri wa mambo ya kigeni wa India
India inalilaumu kundi la Lashkar-e-Taiba (LeT) la nchini Pakistan
kwa mashambulio yaliyofanywa na wanaume 10 waliowaua watu zaidi ya 160
na kusitisha mchakato wa miaka mitano wa kutafuta amani kati ya nchi
hizo mbili za Asia Kusini ambazo zimepigana vita mara tatu tangu
zilipojipatia uhuru wao kutoka kwa Uingereza mnamo mwaka 1947.
Pakistan imekiri kwamba mashambulio ya Mumbai kwa sehemu fulani
yalipangwa katika ardhi yake na kuwatia mbaroni washukiwa wasiopungua
saba, akiwemo kiongozi aliyeyaongoza mashambuo hayo, Zakiur Rehman
Lakhvi. India inaitaka Pakistan iwajumulishe washukiwa zaidi kwenye
uchunguzi wake, akiwemo Hafiz Saeed, anayedhaniwa kuwa muasisi wa kundi
la LeT, ambaye alikamatwa na baadaye kuachiwa huru kwa kukosekana
ushahidi wa kutosha.
Suba Chandran, mtaalam wa uhusiano kati ya India na Pakistan, mjini
New Delhi, anasema mazungumzo ya leo mjini Islamabad hayatafua dafu
katika kuyafufua mazungumzo ya amani kwa kuwa Pakistan inasita
kushirikiana.
"Hakuna uwezekano wa Pakistan kuwawasilisha washukiwa hao kwa kuwa ni
suala la kisiasa. India imeeleza wazi msimamo wake na inaungwa mkono na
jumuiya ya kimataifa. Hakuna kinachoweza kufanyika. India inatakiwa
kuzungumza na jirani yake."
Mazungumzo ya leo yamegusia pia mzozo wa jimbo la Kashmir, ambalo
India na Pakistan zinadai ni himaya yake. Mkutano umegubikwa na madai ya
waziri wa mambo ya ndani wa India, GK Pillai kwamba shirika la ujasusi
la Pakistan lilihusika katika shambulio la mjini Mumbai, kwa kusimamia
na kuratibu mipango yote tangia mwanzo hadi mwisho. Pillai amenukuliwa
akisema ushahidi ulijitokeza wakati alopihojiwa mshukiwa wa ugaidi,
David Headley, raia wa Marekani ambaye anazuiliwa na maafisa wa
Marekani.
http://www.dw-world.de/
http://www.dw-world.de/
0 comments:
Post a Comment