Shirikisho la
Soka Duniani FIFA limeisifu Afrika Kusini kwa usimamizi mzuri wa Kombe
la Dunia huku duru ya pili ya mashindano hayo ikianza.
Katibu Mkuu wa
FIFA Jerome Valcke amesema Afrika Kusini imefanikiwa kukabiliana na
changamoto za kuandaa Kombe la Dunia na kuongeza kuwa hakuna tatizo
lololote la kimsingi lililoshuhudiwa hadi sasa. Valcke amesema kama
mambo yataendelea ilivyo hivi sasa basi Afrika Kusini itakuwa kati ya
nchi zitakazopewa fursa ya kuandaa Kombe la Dunia siku za usoni iwapo
nchi iliyoteuliwa kuandaa michuano ya kombe hilo itashindwa kufanya
hivyo. Wakati huo huo FIFA imeionya vikali serikali ya Ufaransa kuwa
isijaribu kuingiza masuala ya siasa katika usimamizi wa soka nchini
humo. Onyo hilo la FIFA linafuatia matamshi yaliyotolewa hivi karibuni
na Rais Sarkozy wa Ufaransa baada ya timu ya taifa ya nchi hiyo
kuondolewa mapema katika mashindano ya kombe la dunia. Katibu Mkuu wa
FIFA amesema serikali ya Ufaransa haina haki ya kumtaka mkuu wa
shirikisho la soka nchini humo Jean-Pierre Escalletes ajiuzulu. Timu ya
taifa ya Ufaransa iko chini ya mashinikizo makali ya kisiasa kufuatia
fedheha ya kuondolewa mapema katika Kombe la Dunia.
0 comments:
Post a Comment