Ethiopia yasema imefikia makubaliano ya amani na waasi Ogaden
Serikali ya Ethiopia imedai kuwa mrengo mmoja wa waasi wa eneo la Ogaden
umekubali mapatano ya amani lakini kundi hilo la waasi limekanusha
kuwepo mapatano yoyote.
Harakati ya Ukombozi wa Ogaden ONLF
inapigania kujitenga eneo la Ogaden ambalo lina watu wenye asili ya
Somalia.
Abay Tsehaye mshauri wa usalama wa taifa wa Waziri Mkuu wa
Ethiopia Meles Zenawi amedai kuwa Juni 12 kulifanyika mkutano nchini
Ujerumani kati ya wawakilishi wa serikali na wawakilishi wa mrengo wa
ONLF unaoongozwa na Selahadin Mao. Amesema mrengo huo unaodhibiti nusu
ya wapiganaji wa ONLF umesema utaheshimu katiba. Hatahivyo kundi hilo la
waasi limetoa taarifa na kukanusha kuwepo makubaliano hayo. Eneo la
Ogaden lina utajiri mkubwa wa mafuta na waasi wamekuwa wakihujumu
mashirika ya kimataifa yanayochimba mafuta na gesi katika eneo hilo.
*********************************
Mkutano wa G20 waanza Canada
Nembo ya mkutano wa kundi la G-20 uliofunguliwa rasmi
mjini Toronto, Canada.
Viongozi wa kundi la nchi
zilizoendelea kiviwanda na zile zinazoinukia kiuchumi-G-20 wameanza
mkutano wao wa kilele mjini Toronto, Canada
TORONTO
Viongozi wa kundi la nchi zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia
kiuchumi- G-20 wameanza mkutano wao wa kilele mjini Toronto. Viongozi
hao wa mataifa hayo 20 walilakiwa na mwenyeji wao Waziri Mkuu wa Canada,
Stephen Harper. Canada pia ilikuwa mwenyeji wa mkutano uliomalizika kwa
kundi la nchi nane tajiri duniani- G-8. Katika mkutano huo wa siku
mbili, viongozi hao watajadili mkakati wa kuongeza nguvu harakati za
kufufua uchumi pamoja na mpango tata wa kuyadhibiti masoko ya fedha.
Kundi hilo la G-20 ni kundi jipya, ambalo mkutano wake wa kwanza
ulifanyika mjini Pittsburg, Pennsylvania na linayaleta pamoja mataifa
manane tajiri duniani, pamoja na nchi zinazoinukia kiuchumi kama vile
Australia, Brazil, China na India. Nchi nane tajiri kiviwanda,
Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Japan, Itali, Urusi na Marekani
zilimaliza mkutano wao wa siku mbili jana, kwa kuahidi dola bilioni 7.3
katika miaka mitano ijayo, kupambana na vifo vya watoto walio chini ya
umri wa miaka mitano. Mkutano huo pia uligusia masuala ya usalama,
ikiwemo Iran, Korea Kaskazini, Afghanistan, Pakistan na Mashariki ya
Kati.
0 comments:
Post a Comment