Bi.
Shella Mbita, Mtoto wa Balozi Hashim Mbita nae pia alikuwa mmoja wa
wajumbe waliohudhuria warsha ya amani na usalama jijini Arusha (Picha
zote na Rosemary Malale)
=======
Na. Ally Kondo, Arusha
Warsha
ya siku tatu kuhusu Amani na Usalama Barani Afrika iliyoandaliwa na
Umoja wa Afrika (AU) imehitimishwa jijini Arusha siku ya Alhamisi tarehe
23 Oktoba 2014. Warsha hiyo ambayo kaulimbiu yake ilikuwa “Silaha
zisitumike kuuwa watu Barani Afrika ifikapo mwaka 2020” ilimalizika kwa
wajumbe kutoa Rasimu ya Tamko la Arusha (Arusha Declaration).
Katika
Tamko hilo, kumebainishwa asili ya migogoro inayohusu nchi moja au
baina ya nchi na nchi nyingine, vitu vinavyochochea migogoro na ukosefu
wa utulivu Barani Afrika, wanaochochea na kudhamini migogoro pamoja na
athari za maendeleo ya dunia kwa Bara la Afrika.
Aidha,
Tamko hilo limeainisha juhudi zinazofanywa katika kukabiliana na
vitendo vya siasa kali, uhalifu wa kimataifa na athari za mabadiliko ya
tabianchi katika amani na usalama.
Tamko
limebainisha pia kuwa migogoro mingi katika nchi za Afrika
inasababishwa na ukosefu wa utawala bora katika Serikali, uwajibikaji,
uwazi, uongozi shirikishi pamoja na kushindwa kutatua changamoto za
umasikini na ukosefu wa usawa.
Kwa
mujibu wa Tamko hilo, wajumbe kwa kauli moja walikubaliana na hoja kuwa
ili nchi za Afrika ziondokane na matatizo hayo, hazina budi kutekeleza
miongozo na maamuzi yanayotolewa na AU kuhusu amani, usalama na uongozi.
Walisema kuwa maamuzi hayo yanatoa dira nzuri ya namna ya kukabiliana
na changamoto za usalama Barani Afrika, isipokuwa nchi za Afrika hazina
utamaduni wa kuyatekeleza.
Hivyo,
wajumbe walisisitiza umuhimu kwa nchi wanachama wa AU kutekeleza
maamuzi yote yanayofanywa na kuridhiwa na AU, Jumuiya za Kikanda na
wadau wengine.
Aidha,
walitoa wito kwa nchi wanachama wa AU, Kamisheni ya AU, Jumuiya za
Kikanda, Baraza la Amani na Usalama la AU na wadau wengine kulipa
kipaumbele suala la kuweka utaratibu wa kufanya tathmini ya utekelezaji
wa maamuzi hayo.
Sanjari
na hayo, wajumbe walipongeza mabadiliko chanya yanayotokea Barani
Afrika ikiwa ni pamoja na kupungua kwa migogoro ya kutumia silaha,
kuongezeka kwa chaguzi za kidemokrasia, kukua kwa uchumi na ongezeko la
kasi ya kupambana na vitendo vya ufisadi katika nchi nyingi za Afrika.
Licha
ya maboresho hayo, wajumbe walielezea wasiwasi wao kuhusu tishio
linalotokana na changamoto mpya katika amani na usalama wa Bara la
Afrika. Walihimiza umuhimu wa kutumia mbinu za kibunifu kukabiliana na
changamoto hizo ambazo ni; uhalifu wa kimataifa kama vile ugaidi,
uharamia, biashara haramu ya binadamu, biashara ya silaha na dawa za
kulevya na biashara ya fedha haramu.
Wakati
wa kufunga warsha hiyo ambayo iliwakutanisha Mabalozi, wasuluhishi,
wajumbe maalum, wawakilishi wa Jumuiya za Kimataifa na wasomi
mbalimbali, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Mnasa Nyerembe alielezea
matumani yake kuwa, washiriki walipata fursa nzuri ya kujadili kwa kina
chanzo cha migogoro Barani Afrika na kupendekeza njia muafaka za
kukabiliana nayo. Alisisitiza umuhimu wa mapendekezo hayo kuingizwa
katika sera za kitaifa, kikanda na kimataifa ili yaweze kuwa na manufaa.
-Mwisho-
|
0 comments:
Post a Comment