Mkurugenzi
wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw.
Ephraimu Kwesigabo akitoa taarifa ya mfumuko wa bei nchini kwa mwezi
Agosti, 2014 leo jijini Dar es salaam.
Na. Aron Msigwa-MAELEZO.
Mfumuko
wa Bei wa Taifa kwa mwezi Agosti, 2014 umeongezeka hadi kufikia
asilimia 6.7 kutoka asilimia 6.5 iliyokuwepo mwezi Julai kutokana na
kuendelea kupanda kwa bei ya baadhi ya bidhaa na huduma katika maeneo
mbalimbali nchini.
Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Bw. Ephraim Kwesigabo akitoa taarifa ya ongezeko hilo leo jijini Dar es salaam, amesema
kuwa bidhaa zisizo za vyakula zikiwemo Bia, Sare za shule, mkaa, samani
za nyumbani na bidhaa za vitambaa kwa matumizi ya nyumbani zimechangia kuwepo kwa ongezeko dogo la mfumuko wa bei nchini.
Ameongeza
kuwa kuwepo kwa ongezeko la gharama kwenye huduma ya meno, huduma za
vyakula kwenye migahawa na zile za kulala hotelini katika maeneo
mbalimbali nchini pia zime kumechangia mfumuko wa bei.
Aidha, Bw. Kwesigabo amebainisha kuwa
kuongezeka kwa Fahirisi za bei kwa maana ya kipimo kinachotumika kupima
mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma mbalimbali zinazotumiwa na
sampuli wakilishi ya kaya binafsi nchini hadi 149.31 kwa mwezi Agosti
2014 kutoka 149.16 za mwezi Julai kumechangiwa na kupanda kwa gharama ya
bidhaa zisizo za vyakula.
Kuhusu
mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi kwa mwezi Agosti amesema
kuwa umeongezeka kwa asilimia 0.1 huku uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania
katika kununua bidhaa na huduma za jamii kwa mwezi Agosti, 2014 ukipungua na kufikia shilingi 66 na senti 97.
“ Kuongezeka kwa bei ya baadhi ya bidhaa na huduma katika maeneo mbalimbali kuna athari kwa fedha yetu, hii inamaanisha
kwamba, uwezo wa fedha yetu katika kununua huduma na bidhaa za mlaji
unapungua, mfumuko wa bei unapopanda thamani ya shilingi nayo inashuka”
Kwa upande wa ulinganifu wa
mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki Bw.
Kwesigabo ameeleza kuwa una mwelekeo unaofanana na kuongeza kuwa mfumuko
wa bei nchini Kenya kwa mwezi
Agosti umefikia asilimia 8.36 ikilinganishwa na 7.67 za mwezi Julai huku
Uganda ikiwa na mfumuko wa bei wa asilimia 2.8 mwezi Agosti
ikilinganishwa na asilimia 4.3 za mwezi Julai.
0 comments:
Post a Comment