Waziri
Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye jana aliamua kutoa ya moyoni wakati
alipobainisha kuwa kujengwa kwa kiwango cha chini kwa miradi mingi,
kunatokana na wakubwa kupewa 'pasenti' za rushwa na kampuni zinazoshinda
zabuni hizo.
Sumaye,
ambaye amekuwa kimya kwa muda mrefu, alisema hayo jana katika Chuo cha
Benki Kuu jijini Mwanza wakati akizindua kikundi cha vijana kinachoitwa
Tanzania Youth Development Centre (TYDC), tawi la Mwanza.
"Hii ni
rushwa ya ulafi. Hii wananchi wanaweza wasiione moja kwa moja, lakini
ina maumivu makali na mabaya ya muda mrefu kwa nchi," alisema mtendaji
huyo mkuu wa zamani wa serikali.
"Hii ni
rushwa ya wakubwa wanaotoa uamuzi kwa miradi mikubwa ya taifa na
muhusika anawekewa asilimia zake fulani za gharama za mradi kama fedha
zake binafsi na fedha hizi au chochote walichokubaliana wakapeana kwa
utaratibu wowote watakaokubaliana," aliongeza Sumaye.(P.T)
"Hapa
lazima mradi husika utajengwa chini ya kiwango kwa sababu kubwa mbili;
kwanza, sehemu ya fedha za mradi zimeingia mfukoni mwa mtu kwa hiyo ili
zilizobaki, ni lazima zitakuwa za kurashiarashia mradi; pili; ambaye
angesimamia mradi huo anafumbwa macho, haoni tena, amezibwa masikio
hasikii tena na amefungwa mdomo hasemi tena.
"Rushwa
hii ina gharama kubwa kwa uchumi kwa sababu miradi tunayokopea fedha
nyingi au hata kama ni fedha zetu, inashindwa kukamilika kwa wakati au
inakamilishwa tu, lakini haina maisha marefu kama ambavyo ilitegemewa."
Sumaye ambaye hakuweka bayana miradi hiyo, alisema:
"Hasara
nyingi ni kuwa zile kampuni zenye uwezo wa kufanya kazi bila rushwa
haziwezi kupata kazi kwa sababu ya kuzidiwa ujanja na watoa rushwa. Hili
nalo ni la hatari sana kwa uchumi wetu."
Dawa za kulevya
Akizungumzia
dawa za kulevya, Sumaye, ambaye ni waziri mkuu mstaafu pekee aliyeshika
wadhifa huo kuanzia mwaka 1995 hadi 2005, alisema biashara ya dawa za
kulevya hufanywa na watu wazito ama kwa fedha zao au kwa madaraka yao.
Alisema kwa sasa Tanzania inaonekana kuwa kituo muhimu cha kupitishia dawa hizi kwenda na kutoka nchi nyingine.
"Hii siyo
sifa nzuri kwa nchi yetu... ukiachilia mbali madhara ya kupitishia
nchini mwetu, dawa hizi huathiri vijana na kuwageuza mazezeta kwa baadhi
ya wanaotumia."
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment