SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Monday, July 28, 2014

Abdallah Bin Klebu (kushoto) akiwa na Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji. Picha ya Maktaba.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu mkuu wa Yanga, Beno Njovu alisema uamuzi wa kuvunja Kamati ya Utendaji na kuteua wajumbe wapya ni kwa mujibu wa azimio namba nne la mkutano wa wanachama kuhusiana na mabadiliko ya katiba yaliyofanyika Januari 20, 2013.   Njovu alisema katika mkutano huo, wanachama wa Yanga walimpa mamlaka mwenyekiti na makamu wake kuvunja au kuteua wajumbe wa Kamati ya Utendaji na kamati nyingine za klabu hiyo.
Alisema wajumbe wa sasa wa Kamati ya Utendaji watamaliza muda wao Julai 31 na wapya wataanza kazi Agosti Mosi.  “Uamuzi huu ni kwa mujibu wa Ibara ya 28 kifungu kidogo cha kwanza cha katiba ya klabu. Hivyo ni uamuzi sahihi ambao mwenyekiti na kamati yake wameupitisha. Tunawashukuru wajumbe waliotumikia klabu hiyo kwani bado ni wanachama wetu,” alisema Njovu.   Wajumbe wapya walioteuliwa na Manji na Sanga ni Abubakari Rajabu, ambaye amepewa kazi ya kusimamia mradi wa Jangwani City, Sam Mapande (sheria na utawala bora), George Fumbuka (uundwaji wa shirika), Wazir Barnabas (vibali vya hatimiliki na mahusiano na wafadhili) na Abbas Tarimba, ambaye atashughulikia mipango na uratibu.
Wengine katika orodha ya wajumbe wapya ni Isaac Chanji na Seif ‘Magari’ Ahmed (uendeshaji wa michezo), Musa Katabalo (mauzo ya bidhaa), Mohamed Bhinda (ustawishaji matawi), David Sekione (uongezaji wa wanachama) na Mohamed Nyenge, ambaye atashughulikia masuala ya utangazaji wa habari, taarifa na matangazo.  Njovu alifafanua kuwa wajumbe wa kamati hiyo mpya pia watakuwa na kazi ya kusimamia kamati ndogo ndogo za klabu hiyo. Alisema Mapande atasimamia Kamati ya Maadili, Nidhamu na Uchaguzi wakati Fumbuka na Barnabas watasimamia Kamati ya Uchumi na Fedha, huku Seif Magari na Isaac Chanji wakisimamia Kamati ya Mashindano, Soka la Vijana na Wanawake na Ufundi.  Akizungumzia kutoswa kwake katika Kamati ya Utendaji ya Yanga, Bin Kleb alisema miezi miwili iliyopita aliwaomba viongozi wasimteue kwenye Kamati ya Utendaji.
Habari kwa hisani ya http://www.mwananchi.co.tz/

0 comments:

Post a Comment