Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolas Mgaya.
Dar na mikoani.
Wakati Rais Jakaya Kikwete akitarajiwa kuhutubia wafanyakazi katika kilele cha Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), limeitaka Serikali kupandisha kima cha chini hadi kufikia Sh750,000.
Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolas Mgaya alisema jana kuwa wanahitaji kuona wafanyakazi wakipata kiwango cha mshahara kinachokidhi mahitaji.
Alisema kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi na mfumuko mkubwa wa bei uliopo kwa sasa, kiwango hicho angalau kinaweza kukidhi mahitaji muhimu ya wafanyakazi wa kima cha chini, ikiwamo malazi, mavazi, chakula na mahitaji ya afya.
“Katika hali halisi, tunaona namna bei za vitu muhimu ikiwamo umeme, maji, mafuta, gharama za vifaa vya ujenzi, nyumba vyakula na gharama nyingine za maisha zimekuwa zikipanda maradufu katika miaka ya karibuni, lakini hakuna namna inayofanyika kuleta unafuu kwa wafanyakazi.
Kimsingi kima cha chini lazima kiongezwe ili kikidhi mahitaji ya maisha ya wakati huu,” alisema.
Dar mwenyeji
Akizungumzia sherehe hizo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alisema kabla ya Rais Kikwete kulihutubia taifa, atapokea maandamano ya wafanyakazi yatakayoanzia Viwanja vya Mnazi Mmoja saa 1:00 asubuhi.
Alisema maadhimisho ya mwaka huu yenye kaulimbiu ya ‘Utawala Bora utumike kutatua kero za wafanyakazi’, yatatoa fursa kwa wafanyakazi kujumuika pamoja na wenzao duniani.
Sherehe Pwani
Mwenyekiti wa Tucta Mkoa wa Pwani, Paulo Msilu alisema maadhimisho hayo yanafanyika huku Serikali ikiwa bado si sikivu kwa kushindwa kutekeleza ahadi mbalimbali kwa wafanyakazi.
“Licha ya kuwekwa bayana, lakini yamekuwa hayatekelezwi zaidi ya ahadi za kupatiwa ufumbuzi,” alisema.
Aliyataja baadhi ya madai ya msingi ya wafanyakazi kuwa ni stahili za walimu ikiwamo malimbikizo ya likizo, na kupandishwa madaraja... “Tunakwenda kwenye Mei Mosi lakini wafanyakazi wamekata tamaa,” alisema Msilu.
Iringa Mei Mosi
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Christine Ishengoma anatarajiwa kuongoza maadhimisho hayo kwenye Viwanja vya Kanisa Katoliki, Isimani.
Mratibu wa maadhimisho hayo Mkoa wa Iringa, Hillary Kitipwi alisema mwaka huu, sherehe hizo zitafanyika kimkoa katika Tarafa ya Isimani yakishirikisha viongozi wote wa vyama vya wafanyakazi kutoka katika matawi mbalimbali na wanachama wao.
Alisema sherehe hizo zitatanguliwa na maandamano ambayo yatapokewa na Mkuu wa Mkoa kabla ya kutoa zawadi kwa wafanyakazi bora kutoka katika sekta mbalimbali.
Imeandikwa na Andrew Msechu (Dar), Fina Lyimo na Daniel Mjema (Moshi), Geofrey Nyang’oro (Iringa) na Julieth Ngarabali (Pwani).
(CHANZO: MWANANCHI)