Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini (Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango), Bi Joyce Mkinga (katikati)
akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati alipokuwa akitoa
taarifa ya kupitiwa upya kwa Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu. Pamoja nae ni
Mchambuzi Mkuu wa Sera (Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango), Bw. Edwin Ninde
(Kushoto) na Afisa Habari wa Idara ya Habari, Bibi Georgina Misana (Kulia).
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini (Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango), Bi Joyce Mkinga (katikati) na
Mchambuzi Mkuu wa Sera (Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango), Bw. Edwin Ninde
(Kushoto) wakiandika maswali yaliyokuwa yakiulizwa na wanahabari (hawapo
pichani).
Mchambuzi Mkuu wa Sera (Ofisi ya Rais,
Tume ya Mipango), Bw. Edwin Ninde (Kushoto) akitoa ufafanuzi juu ya umuhimu wa
kufanyiwa mapitio kwa Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu. Katikati ni Mkuu wa
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoks Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bi
Joyce Mkinga na Afisa Habari wa Idara ya Habari, Bibi Georgina Misana (Kulia).
****************
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Sera
ya Taifa ya Idadi ya Watu Kufanyiwa
Mapitio
1. Utangulizi:
Sera ya Taifa ya
Idadi ya Watu kwanza ya iliandaliwa mwaka 1992 ambapo ilifanyiwa na kuandaliwa
upya mwaka 2006 kwa azma ya kuratibu na
kushawishi sera za sekta nyingine, mikakati na program za maendeleo kuhakikisha
zinajumuisha masuala ya maendeleo endelevu ya watu, kukuza usawa wa kijinsia, uwezeshaji
wa wanawake, haki za watoto, na makundi mengine yenye uwezekano wa kuathiriwa kwa
urahisi.
Tangu mwaka 2006 hadi
sasa, maendeleo mapya yametokea kitaifa na kimataifa yenye uhusiano wa moja kwa
moja na masuala ya idadi ya watu na maendeleo, mfano masuala ya mabadiliko ya
tabia nchi, Magonjwa yasiyo ya kuambukiza, nk. Kimataifa kumekuwepo na msukumo mpya wa
kuimarisha maendeleo endelevu ya masuala ya idadi ya watu mfano masuala ya
diaspora, mabadiliko ya tabia nchi, uhaba wa chakula duniani, nk.
2. Malengo ya Sera ya Taifa ya Idadi
ya Watu:
Lengo kuu la Sera ya
Taifa ya Idadi ya Watu ya mwaka 2006 ni kuiwezesha Tanzania kufikia kiwango cha
maisha bora ya watu wake. Vipengele muhimu vya ubora wa maisha ni pamoja na
afya na elimu bora, chakula cha kutosha na makazi bora, mazingira bora, usawa
wa kijinsia na usalama wa watu binafsi.
Sera ina malengo ya kuelekeza ubunifu
wa sera za kisekta, mikakati na mipango mingine inayohakikisha maendeleo ya
watu. Malengo mahususi ya sera ya mwaka 2006 ni pamoja na:
i.
Maendeleo endelevu na kuondoa
umaskini;
ii.
Kuongeza na kuboresha upatikanaji na
ufikiaji wa huduma bora za kijamii;
iii.
Kuwa na mgao sawa, usawa wa kijinsia,
uwezeshaji wa wanawake na maendeleo kwa wote; na
iv.
Mpangilio mzuri baina ya idadi ya
watu, matumizi ya rasilimali na mazingira.
3. Viashiria vya idadi ya watu:
Sensa ya Taifa ya
Watu na Makazi ya 2012 inaonesha maendeleo na mabadiliko ya viashiria vya idadi
ya watu ambavyo ni vizazi, vifo na uhamiaji, hivyo kuwepo haja ya kufanya
mapitio katika Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu 2006 ili kuendana na mabadiliko
hayo.
Uchambuzi wa takwimu
za awali za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 unaonesha viashiria vingi vya
idadi ya watu na maendeleo vimebadilika hivyo kuhitajika sera na mikakati mipya
ya kutekeleza mipango mbalimbali ya idadi ya watu na maendeleo.
Sera ya Idadi ya
Taifa ya Idadi ya Watu ya mwaka 2006 iliandaliwa wakati Watanzania walikuwa
wanakisiwa kuwa takiribani milioni 38. Hata hivyo, idadi ya Watanzania
kulingana na Sensa ya Idadi ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inaonesha kuwa
Tanzania ina jumla ya watu milioni 44,928,923 ambapo Tanzania bara ni
43,625,354 na Tanzania Visiwani ni watu 1,303,569.
Taarifa hizo
zinaonesha kuwa idadi ya vifo vya akina mama na watoto vimepungua kutoka 529
mwaka 1990 hadi kufikia 454 mwaka 2010, kwa kila vizazi hai 100,000 (Tanzania Demographics and Health Survey
2010 (TDHS 2010), kasi ya ongezeko la watu imepungua kutoka asilimia 2.9 (kwa
mujibu wa sensa ya mwaka 2002) hadi kufikia 2.7 kwa mwaka 2012.
Vile vile, kasi ya
uhamiaji imeongezeka maradufu ambapo kumekuwepo na wimbi kubwa la watu kuhama
kutoka vijijini kwenda mijini au kijiji kimoja kwenda kijiji kingine (rural
–rural migration). Aidha, kumekuwepo na suala la uhamiaji kutoka nchi moja na
kwenda nchi nyingine kutokana na sababu mbalimbali za kiuchumi, kijamii na hata
kiusalama, hii inajitokeza sana katika maeneo yanayozunguka maziwa makuu.
Kutokana na
mabadiliko haya Serikali inaona kuna haja ya kufanya mapitio ya Sera ya Taifa
ya Idadi ya Watu ya mwaka 2006 na Mkakati wake wa utekelezaji ili kuendana na
mabadiliko hayo.
4. Mapitio ya sera:
Ofisi ya Rais, Tume
ya Mipango kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itafanya mapitio ya Sera hiyo
ili kuendana na taarifa mpya ambazo zimepatikana baada ya kukamilika kwa sensa,
mapitio yanatarajia kufanyika katika kipindi cha mwaka 2014/15.
Sera ya Taifa ya
Idadi ya Watu inalenga kuratibu na kuhusisha sera, mikakati na programu
nyingine ili kuhakikisha maendeleo endelevu ya watu na kukuza usawa wa kijinsia
na uwezeshaji wanawake.
Vile vile Sera ya
Idadi ya Watu inatoa fursa na maelekezo kwa sera zingine za kisekta kuweka
kipaumbele masuala ya idadi ya watu na maendeleo katika kupanga mipango ya
kisekta.
Katika mapitio hayo,
tunatarajia Sera ya Taifa ya Idadi ya Watu iweke msisitizo katika kupanga na
kutekeleza masuala yafuatayo;
i)
Ukosefu wa ajira kwa vijana, wanawake
na makundi maalum;
ii)
Elimu kwa kuzingatia ngazi zote
(awali, msingi, sekondari, hadi elimu ya juu) kwa makundi yote ya jamii;
iii)
Uwezeshaji kiuchumi kwa kuzingatia
makundi yote katika jamii;
iv)
Umiliki wa rasilimali ardhi – nini
kifanyike katika kuhakikisha kuwa jamii inashiriki katika kumiliki
ardhi/mgawanyiko wa rasilimali za nchi kwa kuzingatia idadi ya watu na makundi
mbalimbali katika jamii;
v)
Miundombinu kwa kuweka kipaumbele
mahitaji ya watu wenye mahitaji maalum, kuweka miundombinu rafiki katika
kutunza mazingira na maendeleo ya binadam kwa ujumla;
vi)
Maendeleo ya miji na vijiji;
vii)
Afya ya uzazi kwa kuzingatia mila,
desturi, taratibu, sheria na kanuni zilizopo – kuweka msisitizo wa elimu kwa
wote kama moja ya mikakati ya kuboresha afya ya uzazi; na
viii)
Kuimarisha haki za binadamu.
5. Hitimisho:
Kwa ujumla
unapozungumzia maendeleo unazungumzia watu na hivyo, katika kupanga tunapanga
kwa ajili ya watu; kujua wako wangapi, wako wapi, na wanafanya nini.
Imetolewa na Ofisi ya
Rais, Tume ya Mipango
Tarehe 04/04/2014