SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Friday, April 4, 2014

KUNDI LA MAFIKIZOLO KUWASILI NCHINI LEO KUPIGA SHOO KESHO MLIMANI CITY

Kundi maarufu la muziki wa Kwaito la nchini Afrika kusini, Mafikizolo linatarajia kutua mchana huu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya onesho moja tu linalotarajia kufanyika katika ukumbi wa Mlimani City, kesho, Jumamosi Aprili 5 mwaka huu.

Mafikizolo imekuwa na rekodi nzuri ya kushinda kwenye tuzo mbalimbali za muziki, kutokana na kupiga muziki na kucheza kwa umahiri, hasa mtindo wao maarufu wa Kwaito.

Kundi hilo linaloundwa na wasanii wawili(Nhlanhla Nciza na Tebogo Madingoane pichani juu), kwa sasa linalotamba na vibao kama "Khona" na "Happiness", watawasili nchini kesho mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini.

Akiongea na gazeti hili, mratibu wa onyesho hilo Vinny Magere kutoka kampuni ya Juegacassa, amesema Mafikizollo, wanatarajia kufanya onesho moja tu maalum na la kihistoria litakalodumu kwa muda wa saa nne.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa kundi hili kufika nchini, tangu kuachia wimbo wao wa "Khona", wimbo ambao umesababisha kundi hilo kujizolea umaarufu mkubwa kwenye kumbi za starehe, na hata katika vituo mbali mbali vya redio.

Mafikizolo kwa sasa wanashikilia taji la kundi bora la mwaka, kwa mujibu wa tuzo za muziki za SAMA (South African Music Awards), huku wakiongozwa kwa kutajwa mara nyingi  kwenye tuzo za Ulaya kama kundi bora la muziki kutoka Afrika.

Kundi hilo maarufu kuliko yote yaliyowahi kutokea kusini mwa Afrika liliwahi kutamba pia miaka ya nyuma na nyimbo kama "Ndihamba Nawe", "Ndixolele", "Sebenza", "Ndashata" na "Ndizolila".

Onesho la hilo, linatarajiwa kuanza saa moja usiku ambapo kiingilio kitakuwa shilingi 20,000 kwa watakaolipa kabla ya onyesho, huku mlangoni watalipia shilingi 35,000 za kitanzania.

Kundi hilo mwaka huu, limeingia katika vipengele vinne kwenye kinyanga’anyiro kikubwa cha tuzo za SAMA.

Katika kinyang’anyiro hicho chenye vipengele 28, kundi hilo limepata nafasi ya kuwania vipengele vinne, ambavyo ni Kolabo Bora ya Mwaka, albam Bora ya Pop ya Mwaka, albam ya Mwaka kupitia albam ya Reunited, na kundi  bora la Mwaka.

Kwa mujibu wa tovuti ya destinyconnect, hafla ya ugawaji tuzo hizo itafanyika nchini humo Aprili 28 mwaka huu.

Kundi hili lilianza shughuli za kimuziki tangu miaka ya 1990, albamu yao ya kwanza walitoa mwaka 1996. Tangu hapo wameshatoa albamu sita, baada ya kutoa albamu yao ya tano mwaka 2003 "Kwela". 

Kundi lilianza kutetereka na baadaye mwaka 2013 waliungana tena na kutoa albamu ya sita iliyoitwa "Reunited" na kutoa singo yao ya kwanza "Khona" wimbo ambao umewatambulisha upya.