Mstahiki
Meya wa Manispaa ya Ilala, ambaye pia ni Diwani wa kata ya Gongo la
Mboto Jerry Silaa akiwasili kwenye shule ya sekondari Pugu kwa ajili ya
kukabidhi madawati 300 kwa shule tatu zilizopo manispaa ya Ilala na
kulakiwa na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Jovinus Mutabuzi.
(Picha zote na
Zainul Mzige).
.Ni katika Mpango wa “Mayor’s Ball” “Dawati ni Elimu, Kalisha mmoja, boresha Elimu”.
Na Zainul Mzige
“Kiongozi
hapaswi kutegemea nguvu za Serikali kufanya shughuli za maendeleo” Hayo
ni maneno ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala ambaye pia ni Diwani
wa kata ya Gongo la Mboto, Jerry Silaa katika hafla ya kukabidhi
madawati kwa shule tatu za sekondari zilizopo Manispaa ya Ilala
iliyofanyika Shule ya sekondari Pugu.
Katika
hafla hii, jumla ya madawati 300 yenye thamani ya shilingi milioni 45
za kitanzania yaligawiwa kwa shule 3 zilizopo manispaa ya Ilala ambazo
ni Shule ya sekondari Pugu (107), Shule ya sekondari Ulongoni (93) na
Shule ya sekondari Jangwani (100) kupitia jitihada zake za kuanzisha
mpango wa Mayor’s Ball 2013 ulioanza mwaka jana kupitia kampeni ya
“Dawati ni Elimu, Kalisha mmoja, boresha Elimu”.
Bwana
Silaa alitoa pongezi na shukrani za dhati kwa wote waliotimiza ahadi
zao katika kufanikisha zoezi zima la ununuzi wa madawati mapya na
kufanikisha kampeni yenye lengo la kuinua viwango vya elimu ya sekondari
na msingi Tanzania. Pia, alichukua nafasi kuwaomba wadau waendelea
kujitokeza kuchangia elimu kwani ni mara ya kwanza kwa jambo hili la “Mayor’s Ball” kufanyika nchini.
Mstahiki
Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa, akisaini kitabu cha wageni
katika shule ya sekondari Pugu mara baada ya kuwasili shuleni hapo.
“naomba
nitumie nafasi kuwapongeza wadau wote walioitikia wito huu na naomba
kutoa rai kwa wale wote walioahidi kutimiza ahadi zao ili kufanikisha
lengo la kampeni hii iliyobeba kauli mbiu ya Dawati ni Elimu kalisha
mmoja, boresha elimu”, alisema Mstahiki meya Jerry Silaa.
Katika
hotuba yake, amewaasa wanafunzi kusoma kwa bidii hasa baada ya
kuwaboreshea mazingira ya kusomea kwa msaada wa madawati mapya na ya
kisasa.
Kwa
upande wake Diwani wa Kata ya Gongo la Mboto, Imelda Samjela, ameiomba
serikali kuu kuiangalia shule ya Sekondari Pugu kwa jicho la pili
kutokana na hadhi yake ya kutoa viongozi nchini na kuifanya iwe na hadhi
ya kimataifa. Shule ya sekondari Pugu inajivunia sifa ya kuwa shule
iliyozaa viongozi shupavuTanzania akiwemo Hayati Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere.
Bi.
Imelda aliongeza kuwa kila mwaka tunapoadhimisha Maisha ya Mwalimu
Nyerere basi kufanyike jambo aidha kupaka rangi na kusafisha mazingira
ya shule hiyo iliyobeba historia ya Taifa la Tanzania. Diwani pia alitoa
wito wa kuweka fungu la fedha za kukarabati majengo ya shule hiyo
pamoja na kutokomeza kero ya Kunguni shuleni.
Mwalimu
Mkuu wa Shule ya sekondari Pugu, Jovinus Mutabuzi(mwenye suti nyeusi)
akizungumzia changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo mbele ya
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa. wengine pichani ni wakuu
wa shule za sekondari Ulongoni na Jangwani waliojuika katika hafla hiyo
ya kukabidhiwa madawati.
Kunguni wamekuwa ni kero kubwa kwa wanafunzi hasa wakati wakulala. Alitoa angalizo hili kwa mwenyekiti wa huduma za jamii.
Akitoa
ufafanuzi wa suala la ukarabati wa majengo ya shule hiyo, Mwenyekiti wa
huduma za Jamii Manispaa ya Ilala, Bi. Angelina Nalembeka amesema kuwa
Manispaa ilishatoa shilingi Milioni 50 kwa ajili ya ukarabati na
wanampango endelevu wa kufanya hivyo kila mwaka. Mpango huu si tu kwa
shule ya Pugu bali kwa shule nyingine pia zinazoizunguka manispaa ya
Ilala.
Mwenyekiti
huyo pia alithibitisha kufanyika kwa zoezi la awali la kutokomeza
Kunguni shuleni kwa kunyunyiza dawa na kuwepo kwa mpango endelevu wa
kunyunyiza dawa ili kuondoa kabisa kero hiyo ya Kunguni shuleni.
Mstahiki Meya Jerry Silaa akipitia moja ya mafaili ya taarifa za shule hiyo.
“Mheshimiwa
Diwani amefuatilia suala lenu la Pugu kwa umakini na taarifa zake
tunazo katika Halmashauri. Mwalimu mkuu atakuwa shahidi na tumeshakuja
kupiga dawa na bado mwaka huu tutakuja kupiga dawa tena kuondoa Kunguni”
alisema Mwenyekiti, Huduma za Jamii.
Aidha,
Mwenyekiti wa huduma za Jamii Manispaa ya Ilala aliongeza kuwa suala ya
kero la Maji liko kwenye utatuzi kamati yake ya manispaa yake
ilishatembelea shuleni hapo na kuona kero hiyo.
Amempongeza
Mstahiki Meya kwa juhudi zake za kutatua tatizo la madawati na ameomba
wengine pia ambao ni viongozi wakubwa serikalini waliosoma shuleni hapo
wakumbuke walipotoka na kusaidia kuiweka katika hali nzuri.
Meza
kuu ikipokea heshima ya ukaribisho kutoka kwa wanafunzi wa shule ya
sekondari Pugu (hawapo pichani). Kutoka kushoto ni Kaimu Diwani wa
Upanga Magharibi, Bi. Jokha Lemki, Diwani wa Kata ya Pugu, Imelda
Samjela, Mstahiki Meya, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Pugu, Jovinus
Mutabazi na Mwenyekiti wa Hudama za Jamii Manispaa ya Ilala, Angelina
Malembeka.
Mwalimu
Mkuu wa Shule ya Sekondari Pugu, Jovinus Mutabuzi akielezea furaha yake
ya kupokea madawati 107 yaliyotolewa na mpango wa Mayor’s Ball 2013
kupitia kampeni ya “Dawati ni Elimu” chini ya Mstahiki Meya wa Manispaa
ya Ilala Jerry Silaa.
Diwani
wa Kata ya Pugu, Imelda Samjela, akiwasilisha kero ya shule ya
Sekondari Pugu kwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa
kuhusiana na wadudu aina ya Kunguni kwenye mabweni ya wanafunzi shuleni
hapo ambapo imekuwa kero kubwa wakati wa kulala na kuwasababisha
usumbufu.
Sehemu
ya madawati kati ya 300 yaliyotolewa na mpango wa Mayor’s Ball 2013
kupitia kampeni yake ya “Dawati ni Elimu” inayolenga kutatua uhaba wa
madawati kwa shule zilizomo ndani ya Manispaa ya Ilala.
Mwenyekiti
wa huduma za jamii manispaa ya Ilala, Angelina Nyalembeka akitoa
ufafanuzi kuhusiana na kero za wadudu aina ya Kunguni katika shule hiyo
ambapo amesema mwaka jana walipulizia dawa kwenye mabweni yote ya
wanafunzi na haraka iwezekanavyo ataliwasilisha kero hiyo kwenye vikao
vya Manispaa na kupatiwa ufumbuzi na wanafunzi waweza kukaa kwa amani
bila usumbufu.
Mstahiki
Meya wa Manispaa ya Ilala ambaye pia ni Diwani wa kata ya Gongo la
Mboto, Jerry Silaa, akizungumza na waalimu pamoja na wanafunzi wa shule
ya Sekondari Pugu, kabla ya kukabidhi madawati kwenye hafla fupi
iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Baadhi
ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Pugu wakifuatilia risala ya mgeni
rasmi Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa.
Mstahiki
Meya Jerry Silaa akiteta jambo na mmoja wa wanafunzi wa kidato cha tatu
ambaye ni mlemavu Voster Peter wakati akikabidhi madawati shuleni hapo.
Baadhi ya viongozi wa Kata ya Pugu, Gongo la Mboto na Upanga Magharibi waliohdhuria hafla hiyo.
Mstahiki
Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa akifurahi jambo na Mwalimu Mkuu
wa Shule ya Sekondari Pugu, Jovinus Mutabuzi, wakati hafla fupi ya
kukabidhi madawati 107 kwa shule hiyo. Kushoto ni Mwenyekiti wa huduma za jamii manispaa ya Ilala, Angelina Nyalembeka akifuatiwa na Diwani wa Kata ya Pugu, Imelda Samjela.
Sasa
mtajinafasi wakati wa masomo darasani si ndio..? Mstahiki Meya Jerry
Silaa akimuuliza mmoja wa wanafunzi wa shule ya sekondari Pugu alipokuwa
akikabidhi madawati.
Mwalimu
Mkuu wa Shule ya Sekondari Ulongoni, Bi. Sikitiko Salehe,( wa pili
kulia) akipokea moja ya madawati kati ya 93 kwa niaba ya shule yake
kutoka kwa Mstahiki Meya Jerry Silaa ikiwa ni zao la matunda ya Mayor’s
Ball 2013 iliyoweka kipaumbele kwenye elimu kuhakikisha kila mwanafunzi
anakaa kwenye dawati katika hafla fupi iliyofanyika kwenye shule ya
sekondari Pugu jijini Dar.
Wanafunzi
wa Shule ya sekondari Pugu wakionyesha nyuso za furaha isiyo na kifani
walipokabidhiwa madawati 107 na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry
Silaa.
Mstahiki Meya Jerry Silaa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa ngazi mbalimbali Kata za Gongo la Mboto na Pugu.
Mstahiki
Meya Jerry Silaa akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa
shule ya sekondari Pugu mara baada ya kukabidhi madawati 107 kwa shule
hiyo.
Kaka
mkuu wa shule ya Sekondari Pugu, Nicetas Ndekubali Ndeng’asso, akitoa
shukrani kwa niaba ya wanafunzi wenzake kwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya
Ilala Jerry Silaa.
Kaka
mkuu wa shule ya Sekondari Pugu, Nicetas Ndekubali Ndeng’asso akipeana
mkono na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa.
Mstahiki
Meya Jerry Silaa akiondoka shuleni hapa mara baada ya kumaliza zoezi la
kukabidhi madawati kwa shule hizo za sekondari za manispaa ya Ilala.