Msemaji
Mkuu wa Wizara ya Fedha, Ingiahedi Mduma, akizungumza wakati wa Semina
maalum kwa 'Mablogger', iliyofanyika katika Hoteli ya Kilimanjaro Park,
Misugusugu Kibaha, hivi karibuni. Semina hiyo imeandaliwa na Wizara ya
Fedha kwa lengo la utaratibu wa kutimiza utekelezaji wa Matokeo Makubwa
Sasa (Big Results Now).
******************************
Na Mwandishi Wetu
Serikali
inalenga kushirikiana na sekta binafsi katika kutekeleza miradi ya
kimkakati yenye thamani ya shilingi trioni 6 hadi kufikia mwaka 2015/16
ikiwa ni sehemu ya ukamilishwaji wa mkakati wa “Tekeleza kwa Matokeo
Makubwa Sasa” yaani Big Results Now (BRN), utaratibu unaotumiwa na
Serikali katika kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa baadhi ya
majukumu yake kwa lengo la kupata matokeo makubwa kwa muda mfupi.
Katika
mkuitano wake na wamiliki wa magazeti tando, msemaji mkuu wa wizara ya
Fedha, Bi Ingiahedi Mduma alibainisha kuwa kuna vyanzo vingi vya fedha
ambavyo wizara yake imedhamiria kuvitumia lakini kwa hii ambayo
wanatarajia kushirikisha sekta binafsi ipo miradi mitatu mikuu ambayo
inatarajiwa kutoa muongozo.
Bi
mduma aliitaja miradi hiyo ya awali kuanza kutekelezwa kwa ubia ni
ujenzi wa barabara ya Dar es Salaam hadi Chalinze, uendeshaji wa Mradi
wa Mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam, na ujenzi wa kituo cha
kufua umeme cha Kinyerezi III.
Amesema
ukiachana na miradi hii, Wizara ya Fedha inaendelea kutekeleza jukumu
la kutafuta na kutoa fedha za kugharamia shughuli za BRN zilizoibuliwa
katika maabara zote sita za Elimu, Maji, Kilimo, Uchukuzi, Nishati na
utafutaji na mapato ya serikali.
Bi
Mduma ameelezea pia kwamba katika kipindi cha Julai hadi Disemba, 2013
Wizara ya Fedha imefanikiwa kutekeleza kiashiria hiki kwa kutoa fedha za
maendeleo za ndani kwenye Wizara zinazotekeleza shughuli za BRN.
Amesema
jumla ya shilingi Bilioni 590.5 zimetolewa katika kuhakikisha kwamba
maabara hizi zinaweza kujitegemea katika miradi yake.
Akitaja
viwango nvya fedha ambavyo wizara imetoa, Bi Mduma alisema miradi ya
Elimu imepewa jumla ya shilingi bilioni 8.3, Miradi ya Maji imepewa
shilingi bilioni 86.0, Miradi ya Kilimo shilingi bilioni 10.2, Miradi ya
Uchukuzi shilingi bilioni 146.6 na Miradi ya Nishati imepewa jumla ya
shilingi bilioni 339.4.