SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Sunday, March 30, 2014

Wajumbe wa Bunge Maalum wasusia Bunge

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Esther Bulaya ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) akipiga kura ya siri juzi wakati Bunge hilo lilipokuwa likipitisha utaratibu wa kupiga kura za aina mbili ya siri na wazi.
Picha na Salim Shao 

Dodoma/Dar. Wakati Bunge Maalumu la Katiba linatarajia kuanza kujadili Rasimu ya Katiba kesho, baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo wameanza kuondoka bungeni, kupinga mwenendo wa Bunge hilo.


Hatua hiyo ya wabunge hao inakuja wakati Bunge Maalumu la Katiba juzi lilipitisha azimio la kutumia kura ya siri na wazi katika kuamua vifungu vya rasimu.

Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samia Saluhu alisema baada ya kupitishwa kwa utaratibu wa kupiga kura za siri na wazi katika Bunge hilo, kuanzia Jumatatu wataanza kujadili sura ya kwanza na sita ambayo inahusu Muundo wa Muungano.

Katika sura ya kwanza, mambo ambayo yanatakiwa kujadiliwa ni Jina, Mipaka, Alama, Lugha na Tunu za Taifa wakati sura ya sita mambo ambayo yanapaswa kujadiliwa ni Muundo wa Muungano.

Lema atangaza kurudi jimboni Arusha

Mjumbe wa Bunge hilo, Godbless Lema alisema anakusudia kuondoka bungeni, kutokana na kutoridhishwa na maridhiano ya kupiga kura za siri na wazi katika kufikia uamuzi katika Bunge hilo.


Akizungumza na Mwananchi jana, Lema alisema hakubaliani na utaratibu uliopitishwa, kwani unalenga kulazimisha kila jambo ambalo chama tawala kinalitaka lipitishwe.

“Huu utaratibu wa kura kupigwa kwa wazi na siri katika kitu kimoja, haupo sehemu yoyote duniani. Sasa sisi kukubali ni kuwasaliti wananchi, kwani hata Dodoma tunaandaa rasimu ya Katiba ya wananchi wote siyo ya CCM pekee,” alisema Lema.

Alisema pia hakubaliani na utaratibu wa kujadili rasimu ya Katiba, ambao umetolewa na Kamati ya Uongozi kwa kuanza na sura ya kwanza na ya sita, kwani vinalenga kufumua Rasimu ya Jaji Warioba.

“Hapa CCM wanataka kulazimisha Serikali mbili kwa kujadili kwanza vifungu hivi, kama vitapita basi watakuwa na uwezo wa kubadili rasimu yote kitu ambacho mimi siwezi kukaa kwenye Bunge hili na kusaliti wananchi waliotoa maoni kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba,” alisema Lema.

Jussa atabiri Bunge kuvunjika.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mjimkongwe, Ismail Jussa, alisema uchaguzi wa vifungu hivyo ambavyo ndivyo vinabeba Rasimu ya Katiba, vinaashiria kuvunjika kwa Bunge hilo katika hatua za awali.

“CCM msimamo wao ni Serikali mbili na sisi ni Serikali tatu na tunaanza kujadili vipengele vinavyobeba Katiba na hakuna atakayekubali kuachia msimamo wake na hapo ndipo Bunge litakapovunjika,” alisema.

Kuhusu utaratibu wa kupiga kura za wazi na siri, Jussa alisema utaratibu huo utaleta mgawanyiko mkubwa, kwa sababu ya msimamo wa CCM ni kura za wazi na hivyo hakuna mjumbe wa chama hicho atakayethubutu kupiga kura ya siri.

Mnyika

Naye mjumbe mwengine wa Bunge hilo, John Mnyika, alisema, CCM ina mpango wa kubadili rasimu kutoka Muungano wa Serikali tatu kuwa wa Serikali mbili ili kufanikisha msimamo wao na maelekezo ya Rais kwenye hotuba yake bungeni.

Mnyika alieleza kuwa kwa mazingira hayo, Ukawa unahitajika kutetea maoni ya wananchi na kwamba CCM wakiendelea na njama zao wakati wa kujadili sura ya kwanza na ya sita, itawalazimu kurudi kwa wananchi ambao ndiyo wenye nchi.

“Hatua ya kurejea kwa wananchi inatarajiwa kuchukuliwa kabla ya kuendelea na sura zingine mbili za Rasimu ya Pili ya Katiba,” alisema Mnyika.

Mnyika alisema mpango huu ulianza kwa wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka CCM wakati wa kujadili rasimu ya kanuni waliwasilisha majedwali ya marekebisho kutaka ibara zipangwe mbili mbili zinazofanana.

Katibu wa Bunge

Hata hivyo, Katibu wa Bunge Yahya Khamis Hamad akizungumzia kuondoka kwa baadhi ya wabunge alisema, suala hilo amelipata jana kupitia Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge lakini si msimamo wa kundi.

“Taarifa hii tulipata kwenye kamati, lakini tukaulizana kama kuna kundi linataka kuondoka, ikabainika hakuna kundi.”

Kuhusu uamuzi wa kuanza kujadili sura ya rasimu ya kwanza na sita alisema tayari yalifikiwa na Kamati ya Uongozi na kwamba kwa mujibu wa kanuni ya 58 kifungu kidogo cha tatu, Kamati ya Uongozi ndiyo yenye jukumu la kupanga utaratibu wa kujadiliwa rasimu.

Kuhusu CCM kuwa na rasimu yake

Akizungumzia taarifa kuwa CCM ina rasimu yake ambayo ndiyo wanataka ijadiliwe alisema hakuna suala hilo.

“Mimi binafsi sijalisikia hilo na sitegemei kuwapo, kwani wajumbe watajadili rasimu iliyo mbele yao ambayo ni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema Hamad.

Wasomi

Wasomi nchini wamesema mfumo wa kupiga kura ya wazi na siri uliopitishwa na Bunge Maalumu la Katiba, hautapunguza nguvu ya mijadala katika Bunge hilo katika vipengele muhimu ikiwa ni pamoja na aina ya muundo wa Serikali.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wasomi hao walisema kuwa badala yake mfumo huo utawalazimisha baadhi ya wajumbe wasiokubaliana na misimamo ya vyama vyao kupiga aina ya kura wasiyoitaka.

Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho alisema mjadala mkali unatarajiwa kuendelea bungeni hasa katika hoja ya aina ya muundo wa Serikali, kwa kuwa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete iliashiria kutotaka muundo wa Serikali tatu.

Profesa Shumbosho alisema kuwa kuna baadhi ya wajumbe wa CCM hawakubaliani na muundo wa Serikali mbili, lakini watalazimika kupiga kura ya wazi ili kukiridhisha chama chao.

“Kuna watu hawana ujasiri. Ndani ya CCM wapo wanaopenda Serikali tatu lakini wanaogopa,” alisema Profesa Shumbusho.

Pia, alisema kuwa kwa namna hali inayoonekana kuendelea bungeni, kuna dalili kuwa maoni ya rasimu ya CCM kuhusu Katiba ndiyo yatakayopita na hivyo kurudisha mambo mengi yaliyopo katika Katiba ya sasa.

Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Gaudence Mpangala alisema kuwa upigaji kura wa wazi au siri hautazuia wajumbe kuendelea na misimamo yao na kwamba badala yake mjadala utakuwa mkali zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

Alisema ingawa yapo baadhi ya mambo ambayo wajumbe wanaweza kukubaliana bila kupiga kura, suala la Muungano litakuwa na mvutano kwa kuwa tayari hotuba ya Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na Rais Kikwete bungeni, zimeshaleta ‘msuguano’.

“Mjadala utakuwa mkali, suala lenyewe tu limeanza kuwa kali tangu mwanzo. Warioba alieleza Serikali tatu, Rais Kikwete akapinga,” alisema Profesa Mpangala.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria, Hamad Salim alisema suala la kupiga kura ya siri au wazi limechukua muda mrefu kujadiliwa bila sababu za msingi.

Akifafanua, Salim alisema kuwa wanaotaka kura ya wazi wanajenga hoja kuwa wanataka masuala yote yawe wazi kwa wananchi, lakini wanashindwa kusema ni lini walipewa maoni hayo na wananchi.

“Sikubaliani na kura ya wazi, hawakutumwa na wananchi, walitakiwa kuridi kwao na kuwauliza aina gani ya kura wanataka,” alisema Salim na kuongeza:

“Kwa muda mrefu upigaji kura ulikuwa wa siri, sasa imekuwaje leo wanataka kura ya wazi?”

Sendeka

Mjumbe wa Bunge hilo, Christopha Ole Sendeka alisema matokeo ya kura za kupitisha kanuni ya 37 na 38 ya upigaji kura yamewashangaza Ukawa, lakini muhimu kwao ni kukaa bungeni na kujenga hoja.

“Matokeo ya jana (juzi) yamewakatisha tamaa kwa ushindi wa idadi nzuri ya kura, walidhani CCM haina theluthi mbili, lakini licha ya wabunge wengi hatohudhuria tumeshinda,” alisema Sendeka.

Alisema wingi wa CCM siyo ndani ya Bunge tu, kwani hata nje wengi wanakiunga mkono chama hicho.

“Vizuri wangekaa tu kwani CCM inaweza kupitisha mambo kwa kura nyingi zaidi, lakini wakiwepo tunaweza kufikia maridhiano katika baadhi ya mambo,” alisema Sendeka.

Umoja wabunge Wanawake

Naye Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wabunge, (TWP), Suzan Lyimo alisema utaratibu wa kura za wazi na siri utaleta vurugu na utekelezaji wake ni mgumu.

“Utaratibu huu ni mgumu kutekelezeka sasa sijui wanaopiga kura za wazi watakaa upande wao na wale wa siri upande wao, lakini ni mgumu kutekelezeka na hakuna nchi ambayo umeshawahi kutumika,” alisema.

Akizungumza na vyombo vya habari kwa niaba ya wabunge wanawake kutoka vyama vya upinzani, Suzan Lyimo alisema hotuba ya Rais Jakaya Kikwete imeleta madhara makubwa kwa wananchi hasa wale ambao hawana itakadi za vyama.

“Hotuba hiyo imeleta mpasuko mkubwa miongoni mwa Watanzania..., sisi kama wajumbe wa Bunge hili tunawahakikishia wananchi kwamba tutajadili Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayotokana na maoni ya wananchi,” alisema.

Kwa upande wake, Sabrina Sungura alisema mchakato huo wa Katiba unaweza usifike mwisho na kwamba mtu wa kwanza wa kulaumiwa ni Rais Kikwete ambaye alitoa hotuba ya kuwagawa wabunge.

“Tulipaswa kuambiwa kuwa Rais anatumia nafasi yake kama sehemu ya Bunge kuleta maoni yake na si kulizindua Bunge kama tulivyoambiwa katika ratiba,” alisema.

Naye Moza Abeid ametaka kurekebishwa upungufu uliojitokeza katika mchakato wa Katiba ili wananchi waweze kupata Katiba waitakayo.

Mussa Juma,Sharon Sauwa na Edith Majura, Goodluck Eliona.

Chanzo: mwananchi