MADAKTARI wa Hospitali ya Holy Family (HFH) mjini hapa wanapigania maisha ya mtoto aliyezaliwa Septemba 25, mwaka huu akiwa na sura mbili na uzito wa kilo 3.2.
Kwa mujibu wa taarifa za hospitalini hapo, mtoto huyo mara baada ya kuzaliwa amekutwa ana tatizo la kupumua hivyo kumlisha kupitia mdomo, mpashaji aliliambia Gazeti la The Express Tribune.
Mtoto huyo ni wa tatu kuzaliwa kutoka kwa Bi. Shahida Perveen na mumewe Khalil Ahmed. Msajili wa hospitali hiyo, Dk. Qaisar Aziz ameliambia The Express Tribune kwamba mtoto huyo amehamishiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (Intensive Care Unit) katika wodi ya watoto na atakuwa katika uangalizi wao.
Hata hivyo, madaktari wameonesha kukata tamaa na kusema kuna uwezekano mdogo kwa mtoto huyo kuendelea kuishi na kukua. “Kumlisha kwa kutumia mdomo haiwezekani kwa sasa, tunamlisha kwa kutumia mipira maalum (Naso-gastric tube). Sura hizi mbili zinafanana,” alisema Dk Qaisar.
Mtoto huyo ana macho manne, pua mbili, midomo miwili na masikio manne, kwa maana kwamba ana sura mbili.
Habari zinasema mama wa mtoto huyo alipopimwa na mashine maalum, (Ultrasound) alionekana hana matatizo yoyote na alikuwa na afya njema.
Baadhi ya wananchi waliotoa maoni yao kufuatia tukio hilo, walisema dunia imetikisika kufuatia kuzaliwa kwa mtoto huyo wa ajabu na kuongeza kuwa hiyo ni ishara kwamba imefika mwisho.