Na Frank Geofray wa Jeshi la Polisi, Moshi.
Jeshi la Polisi Nchini litaendelea
kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na vitendo vya mauaji
yanayosababishwa na Imani za kishirikina kwa kuendelea kutoa elimu kwa
jamii juu ya madhara ya vitendo hivyo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Jeshi la
Polisi Nchini IGP Ernest Mangu katika mkutano mkuu wa maofisa wakuu
waandamizi unaoendelea katika chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi (MPA)
ukiwa na kauli mbiu isemayo “Zingatia Weledi katika Kutoa Huduma bora
kwa jamii”.
IGP Mangu alisema kuna baadhi ya
jamii zinafanya vitendo hivyo kama tamaduni zao hivyo wao kwa kuliona
hilo wataendelea kutoa elimu kwa njia mbalimbali kwa kushirikiana na
Taasisi nyingine ili kuhakikisha kuwa vitendo hivyo vinakomeshwa hapa
nchini. “Tuendelee kutoa elimu kwa jamii lakini pia tutaenelea kuchukua
hatua kwa wote wanaofanya makosa hayo kwa kuwa huo ni uhalifu kama
ulivyo uhalifu mwingine” Alisema IGP Mangu.
Naye Kamishna wa Operesheni na
Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja amewataka Makamanda wa Polisi
wa mikoa kushirikiana na Taasisi nyingine za Serikali katika kutatua
migogoro ya Ardhi ili kuipatia ufumbuzi mapema kabla ya vurugu kutokea
jambo ambalo litaendeleza usalama hapa nchini.
Alisema ni vyema Taasisi husika
kushirikiana mapema katika kutatua migogoro katika jamii kabla haijaleta
madhara kwa kuwa iwapo hilo litafanyika itaepusha uharibifu na gharama
ambazo hutumika katika kutatua mgogoro unapokuwa mkubwa na kusababisha
vurugu. Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Jamii nchini Mussa Ali Mussa
alisema wataendelea kutumia dhana ya Polisi Jamii katika kupambana na
uhalifu kabla haujatokea kwa kuwa wananchi wameonyesha mwitikio mkubwa
tangu kuanzishwa kwa dhana hiyo.
Alisema kwa Mujibu wa Utafiti
uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam kwa ufadhili wa COSTEC umeonyesha kuwa Asilimia 70 ya watanzania
wamekubali dhana ya Polisi Jamii na wameonyesha kuikubali kwa kuwa
imesaidia kupambana na uhalifu unaotokea katika maeneo yao.
Mkutano huo unaoendelea katika Chuo
cha Taaluma ya Polisi Moshi una lengo la kujadili na kufanya tathmini ya
mafanikio yaliyofikiwa mwaka 2013 pamoja na changamoto zilizopo katika
kupambana na uhalifu na kuzipatia ufumbuzi kwa mwaka 2014.
CHANZO:MTAA KWA MTAA
0 comments:
Post a Comment