Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya
Kilombero, Hassan Masala, akifungua mafunzo ya matumizi ya simu kwa
habari katika ukumbi wa Mazingira Kibaoni, Ifakara 03 Februari 2014
yanayolenga kukuza taaluma ya upashaji habari kwa kutumia simu. Kushoto
ni Afisa Tawala wa Wilaya ya Kilombero Bi. Christa Njovu na Kulia ni
Mkufunzi kutoka UNESCO Mama Rose Haji Mwalimu.
Na. Mwandishi wetu
Demokrasia vijijini itapatikana
iwapo vyombo vya habari jamii vitatumika kikamilifu na kutekeleza wajibu
wake wa kupasha habari kwa kutumia teknolojia mpya.
Akifungua mafunzo ya wiki moja
katika Ukumbi wa Mazingira, Kibaoni Ifakara yanayowashirikisha
wanahabari jamii kutoka Pemba, Unguja, Pangani, Ifakara na Kyela, Mkuu
wa Wilaya ya Kilombero Hassan Masala amesema mbinu za kisasa
zinahitajika kuelimisha jamii na mambo gani yafanyike ili kupata uongozi
bora vijijini na taifa kwa ujumla.
Mkufunzi wa Teknolojia ya simu
kwa habari kutoka Chuo Kikuu Bibi Faith Shayo akifafanua jinsi simu za
“SMART” zinavyoweza kutumika kwa habari mbalimbali, picha na maoni
kutoka na kwenda katika jamii kupitia maelekezo husika yaliyomo katika
simu.
Bwana Masala amesema pamoja na
changamoto zilizoko vijijini, Redio Jamii Pambazuko iliyoko Ifakara, ina
mchango mkubwa katika kuelimisha na kukuza demokrasia katika wilaya ya
Kilombero kwa kuwa inafika sehemu kubwa ambako serikali haifiki kwa
urahisi.
Amesema kutokana na miundo mbinu
mibovu ya usafiri, mafunzo ya matumizi ya simu kwa kiasi kikubwa
yataongeza ujuzi katika taaluma ya upashaji habari.
Mafunzo hayo yaliyofanyika
kuanzia tarehe 3 hadi 7 mwezi Februari 2014 yanalenga kutambua uwezo wa
simu katika kutafuta na kutoa habari, kujifunza jinsi Tehama
inavyorahisisha mawasiliao kwa njia ya simu aina ya “SMART” na kuboresha
mbinu za upatikanaji na utoaji wa habari.
Mafunzo ya Tehama kwa redio
jamii ni mwendelezo wa mradi wa kuzipatia uwezo redio hizo kwa kutumia
teknolojia mpya unaofadhiliwa na UNESCO kwa ushirikiano na Shirika la
Maendeleo la Sweden (SIDA).
Mkufunzi na Mtaalamu wa Masuala
ya Redio Jamii Mama Rose Haji Mwalimu kutoka UNESCO, akieleza madhumuni
ya mafunzo kwa washiriki, katika Ukumbi wa Mazingira Kibaoni, Ifakara.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya TEHAMA kutumia simu kwa mawasiliano wakifanya kazi za vikundi.
Washiriki katika vikundi kazi wakitumia simu zao kufanya mazoezi kutokana na mafunzo waliyopata kwa mawasiliano rahisi vijijini.
Mgeni rasmi akiwa katika picha ya
pamoja na wakufunzi pamoja na washiriki wa Redio Jamii kutoka Pangani,
Pambazuko, Kyela, Pemba na Unguja.
0 comments:
Post a Comment